RAIS UTPC ATETEA KITI CHAKE KWA KISHINDO

Mkurugenzi wa UTPC, Abubakar Karsan akimlisha keki Rais wa UTPC, Deogratias Nsokolo ikiwa ni ishara ya kumpongeza baada ya kuchaguliwa kwa kishindo na wajumbe wa muungano huo kutetea nafasi hiyo kwa mara nyingine.

Na Shinyanga Press Club Blog
RAIS wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC), Deogratias Nsokolo ametetea nafasi hiyo kwa mara nyingine baada ya kushinda kwa kishindo katika uchaguzi uliofanyika jana Novemba 17, 2020 mkoani Morogoro.

Nsokolo ameshinda nafasi hiyo kwa kura 72 dhidi ya 11 za mshindani wake, Edwin Soko, huku uchaguzi huo ukifuatiliwa kwa karibu na wadau mbalimbali wa habari nchini.

Wajumbe waliopiga kura kwenye uchaguzi huo ni 83 na hakukuwa na kura yoyote iliyoharibika.

Kwa upande wa nafasi ya Makamu wa Rais wa UTPC, wagombea walikuwa wawili, ambapo Pendo Mwakyembe kutoka Mara aliibuka mshindi wa kiti hicho akipata kura 65 na kumuacha mbali mpinzani wake Lulu George kutoka Tanga aliyeambulia kura 18.

Katika nafasi za wajumbe wa bodi kutoka kundi la wanaume, wagombea walikuwa tisa ambao ni Ali Omary Mbarouq, Robinson Wangaso, Novatus Lyaruu, Hamis Kasapa, Bahati Nyakiraria, Musa Yusuph, Cloud Gwandu, Frank Leonard na AbdulrahmanMfaume.

Ambapo washindi wanne ni Musa Yusuph (51), Cloud Gwandu (61), Frank Leonard (64) na Abdulrahman Mfaume (69).


Katika wagombea wa nafasi za wajumbe wa bodi kutoka kundi la wanawake, walioshinda ni Paulina David, Salma Abdul, Lilian Lucas na Khadija Omary.

Wakati, Mgombea mmoja kundi la wataalamu wa masuala ya fedha aliyeshinda ni Eliaza Mafuru ambaye alipata kura zote 83 za wajumbe wa uchaguzi huo.
Rais Mteule wa Muungano wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) Deogratias Nsokolo akikata keki maalum ya kumpongeza baada ya kushinda nafasi hiyo kwa mara nyingine.
Rais wa UTPC, Deogratias Nsokolo (kushoto) akimlisha keki Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC), Greyson Kakuru
Rais Nsokolo (kushoto) akimlisha keki Katibu Mtendaji wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC), Ali Lityawi







Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464