Meneja Mradi wa Test & Treat (Kupima na Kutibu) kutoka Shirika la Doctors With Africa (CUAMM), Flora Manyanda akizungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari Bariadi na kuwataka kutojihusisha na vitendo vya ngono wawapo shuleni ili kutojiharibia ndoto zao za mbeleni.
Na Damian Masyenene, Shinyanga Press Club Blog
SHIRIKA la Doctrors with Africa (CUAMM) limeendelea na siku ya pili ya kutembelea vituo vya tiba na matunzo kwa kukutana na watoa huduma za afya ngazi ya jamii ambao hufanya zoezi la kupima, kushauri na kufanya ufuatiliaji lengo likiwa ni kuwatia moyo na kuwahamaisha kuzidi kuisaidia jamii hususan.
CUAMM imefanya utembeleaji huo leo Novemba 30, 2020 kwa kushirikiana na Msanii wa Hiphop nchini, Fareed Kubanda maarufu kama Fid Q aliyeambatana na mke wake, Mama Cheusi Dawa, ambapo walivitembelea vituo vya afya Mwamapalala wilayani Itilima, Songambele wilayani Bariadi, Old Maswa (Bariadi) na kukutana na kuzungumza na wanafunzi wa shule ya Sekondari Bariadi.
Wakiwa katika kituo cha afya Mwamapalala walikutana na timu za upimaji na kliniki kwa ajili ya watu wanaoishi na VVU, ambapo Mratibu wa Upimaji VV ngazi ya Jamii kutoka Shirika la Doctors With Africa, Edith Kwezi amesema tangu walivyoanza mradi wa TEST & TREAT mwaka 2017 hali imebadilika jamii imepata elimu, unyanyapaa umepungua japo haujaisha, lakini bado waganga wa kienyeji wanawahamisha (kuwatorosha) kwenye dawa wagonjwa.
“Mfano hapa tunao wagonjwa watatu wamepotea wiki mbili wamehamishwa na waganga wa kienyeji, kwahiyo tunahitaji kuzungumza na waganga kuwajenga kifikra ili wawarudishe. Bado kuna hitaji la muhimu la kuendelea kutoa elimu ili kubadilisha fikra,” amesema.
“Sasa hivi hatusubiri watu waje kupima, bali tunawafuata kwenye jamii kupitia watoa huduma ngazi ya jamii ambao wanawafahamu zaidi kupitia klabu zao na tukiwaibua watu katika maeneo ambayo hawafikiwi tunasaidia kuzuia maambukizi mapya,” ameongeza.
Dk. Kwezi amebainisha kuwa uzuri wa kutumia dawa kwa ufasaha miezi sita mfululizo unakuwa salama (vinakuwa chini) na huna uwezo wa kuambukiza mtu, ambapo amewaomba wasanii akiwemo Fid Q kushirikiana na wataalam hao kufikisha ujumbe kwa jamii, kuhamasisha watu kupima na kutumia dawa.
FID Q, ambaye amekuwa balozi wa masuala ya Ukimwi tangu mwaka 2020, amesema amepata elimuya kutosha kupitia ziara hiyo na kwamba kama wasanii wanayo nafasi kubwa ya kusaidiana na makundi mbalimbali katika jamii kuhakikisha wanapeleka ujumbe na kuelimisha jamii katika upimaji na utumiaji dawa kwa usahihi.
Fid Q amelipngeza shirika la CUAMM kwa namna inavyolishughulikia suala la Virusi Vya UKIMWI kwa kuwafuatilia wahanga, ambapo ameahidi kushirikiana na kuona namna ya kupaza sauti kama mwana jamii, huku mke wake (Mama Cheusi Dawa) mradi huo wa Doctors With Africa wa TEST & TREAT ni ubunifu wa aina ya kipekee kwa kuwafuata wenye uhitaji na kuwapa msaada, ambapo amesema atapaza sauti na kuiunga mkono kadri ya uwezo wake.
“Matembezi haya katika vituo na zahanati zinazofanya kazi kwa kushirikiana na CUAMM kusaidia upimaji, utumiaji dawa na ufuatiliaji wa watu wanaoishi na VVU umeniongezea ufahamu ambao sikuwa nao awali kuhusu mambo ya Ukimwi, hii elimu itanisaidia kupaza sauti nikiwa na ufahamu zaidi wa mambo hayo, pia nawapongeza wahudumu wote wa afya wanaojitolea kwa dhati kufanikisha hili kwa kushirikiana na CUAMM,” amesema.
Wakiwa katika kituo cha Afya Songambele ambacho kipo Kata ya Nkololo halmashauri ya Wilaya ya Bariadi mkoani Simiyu, Mkurugenzi wa kituo hicho, Stephano Mabula amesema tatizo la UKIMWI bado ni kubwa na kuhimiza jamii kutumia maadhimisho ya Desemba Mosi kuwaokoa na kuwasaidia wenye tatizo hilo na wadau waendelee kujitokeza kusaidia mapambano hayo,huku akilishukuru CUAMM kwa kujitokeza na kutoa mchango ambao unasaidia kuifikia jamii.
Mratibu wa shughuli za Kijamii Shirika la Doctors with Africa (CUAMM), Gasaya Msira, amebainisha kuwa amewashukuru na kuwapongeza wahudumu wa afya ngazi ya jamii wanaofanya kazi na shirika hilo katika kufanikisha mradi wa Test & Treat (Kupima na Kutibu) kwani wameleta urahisi katika kuwafikia wanaohitaji huduma, awataka kuendelea kuchapakazi ili kufikia malengo ya Serikali ya 95 95 95.
Mkuu wa Kituo cha Upimaji, Tiba na Matunzo cha Old Maswa, Stanley Mrefu amesema kuwa wanajihusisha na kupima VVU kwa hiari katika jamii, kuwaunganisha na vituo vya huduma na tiba waanze kutumia vidonge vya kufubaza makali na kutoa elimu, ambapo wanafanya kazi kazi zote kwa kushirikiana na idara mbalimbali za serikali, wahudumu wa afya ngazi ya jamii na serikali ngazi za mitaa.
Ziara hiyo ya maofisa wa Doctors With Africa, Msanii Fid Q na Mkewe mkoani Simiyu imehitimishwa katika Shule ya Sekondari Bariadi kwa kuzungumza na wanafunzi ambao pia walionyesha vipaji vya kuimba, kuigiza na kucheza, huku Mwalimu Mkuu wa shule hiyo , Ally Simba akieleza kuwa wanao wanafunzi 1250 wa kidato cha kwanza hadi sita na walimu 40.
Ameongeza kwa kueleza kuwa shule hiyo imekuwa ikifanya vizuri kitaaluma, ambapo kwa matokeo ya kidato cha sita mwaka huu ilikuwa ya kwanza kimkoa na ya 26 kitaifa na wanafunzi wote kupata nafasi ya kwenda chuo kikuu, huku akibainisha kuwa malengo ni kuona shule inaendelea kufanya vizuri na kuingia 10 bora kitaifa.
Msanii Fid Q na Mke wake (kushoto) wakiwasili katika kituo cha afya Mwamapalala na kupokelewa na Mratibu wa Upimaji VV ngazi ya Jamii kutoka Shirika la Doctors With Africa, Edith Kwezi (kulia).
Fid Q akimbeba mtoto mchanga katika wodi la akina mama alipotembelea kituo cha afya Mwamapalala wilayani Itilima
Mke wa Fid Q,Mama Cheusi (kushoto) akimbeba mtoto na kupiga picha na mama wa mtoto huyo baada ya kutembelea wodi la akina mama katika kituo cha afya Mwamapalal leo.
Msanii Fid Q na mke wake wakiwa katika picha ya pamoja na maafisa wa shirika la Doctors With Africa baada ya kutembelea kituo cha afya Mwamapalala
Wahudumu wa afya ngazi ya jamii kutoka maeneo mbalimbali ya wilaya ya Itilima wakiwa katika picha ya pamoja na msanii Fid Q na mkewe baada ya kufika kituo cha afya Mwamapalala kuzungumza nao
Watumishi wa kituo cha afya Mwamapalala wakiwa katika picha ya pamoja na msanii Fid Q aliyeambatana na mke wake walipofika kituoni hapo kujionea shughuli mbalimbali za utoaji huduma za afya.
Msanii Fid Q akiteta jambo na Mkurugenzi wa kituo cha afya Songambele wilayani Bariadi, Stephano Mabula baada ya kukitembelea kituo hicho.
Mmoja wa madaktari katika kituo cha afya Songambele, akimpa maelezo ya huduma mbalimbali zitolewazo kituoni hapo, Msanii Fid Q.
Maofisa wa Shirika la Doctors With Africa pamoja na msanii Fid Q wakimsikiliza mmoja wa madaktari katika kituo cha afya Songambele juu ya huduma mbalimbali zitolewazo kituoni hapo.
Fid Q akiteta jambo na mmoja wa madaktari kituoni hapo
Fid Q akichangia damu katika kituo cha afya Songambele
Mratibu wa shughuli za Kijamii Shirika la Doctors with Africa (CUAMM), Gasaya Msira akiandaliwa ili kuchangia damu kituoni hapo
Msanii Fid Q akiendelea na ukaguzi wa maeneo mbalimbali katika kituo cha afya Songambele
Fid Q akizungumza na wahudumu wa afya ngazi ya jamii na watumishi idara ya ushauri nasaha wanaofanya kazi kwa kushirikiana na shirika la Doctors With Africa katika kituo cha afya Songambele
Mkurugenzi wa kituo cha afya Songambele, Stephano Mabula (kushoto), Msanii Fid Q wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya maafisa wa CUAMM na watumishi wa kituo hicho
Watumishi wa kituo cha afya Songambele idara ya ushauri nasaha, wahudumu wa afya ngazi ya jamii na maofisa wa Doctors with Africa wakiwa katika picha ya pamoja na msanii Fid Q
Wanafunzi wa shule ya sekondari Bariadi wakisikiliza ujumbe kutoka kwa ugeni wa shirika la Doctors with Africa na Msanii Fid Q waliofika shuleni hapo
Mkuu wa Shule ya Sekondari Bariadi, Ally Simba (kushoto) akizungumza na kuwakaribisha wageni shuleni hapo.
Meneja Miradi Shirika la Doctors With Africa, Flora Manyanda akizungumza na wanafunzi juuya umuhimu wa kutojihusisha na ngono katika umri wao.
Mratibu wa shughuli za kijamii kutoka shirika la Doctors With Africa, Gasaya Msira akizungumza na wanafunzi hao
Msanii Fid Q akizungumza na wanafunzi hao
Msanii Fid Q, Maafisa kutoka shirika la Doctors with Africa wakiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya walimu wa shule ya sekondari Bariadi, akiwemo Mkuu wa shule, Ally Simba (wa tatu kushoto)
Baadhi ya wanafunzi wakionyesha vipaji na uwezo wa kuimba na kurap