TUME YA MADINI KUTOA MAFUNZO KWA WACHIMBAJI WADOGO JUU YA USALAMA NA USIMAMIZI WA MAZINGIRA



Tume ya Madini kupitia Kurugenzi ya Ukaguzi wa Migodi na Mazingira inatarajia kufanya mafunzo ya siku tatu kwa wachimbaji wadogo wa madini kwa mikoa ya kimadini ya Mbeya, Chunya na Songwe ambapo yanatarajiwa kufanyika mjini Chunya Mkoani Mbeya.

Akizungumza jijini Dodoma leo tarehe 16 Novemba, 2020 Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Dkt. Abdulrahman Mwanga amesema kuwa mafunzo hayo yanayotarajiwa kuanza tarehe 19 hadi tarehe 21 Novemba, 2020 yanalenga kuwapa wachimbaji wadogo wa madini uelewa mpana kuhusu masuala ya usalama, afya, utunzaji wa mazingira na usafirishaji na matumizi sahihi ya baruti kwenye shughuli za uchimbaji wa madini.

“Aidha elimu kuhusu sheria ya madini pamoja na kanuni zake itatolewa kwa wachimbaji wa madini kupitia wataalam waliobobea kutoka Makao Makuu ya Tume ya Madini,” amesisitiza Dkt. Mwanga.

Dkt. Mwanga ameeleza kuwa mafunzo husika yanatarajiwa kufunguliwa na Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Chalamila na kusisitiza kuwa mafunzo hayo ni mwendelezo wa mafunzo kama haya yaliyofanyika katika mikoa ya Singida, Katavi na Manyara ambapo yataendelea kutolewa katika mikoa mingine ya kimadini. 

Picha na Tume ya Madini
 

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464