Na Tume ya Madini
Leo tarehe 16 Novemba, 2020 Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Profesa Idris Kikula ameongoza kikao cha kazi cha Tume ya Madini kilichofanyika jijini Dodoma lengo likiwa ni kupokea na kujadili taarifa ya utekelezaji wa majukumu ya Tume kwa kipindi cha robo mwaka.
Akizungumza katika
kikao hicho, Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya
ameeleza mafanikio ya Tume ya Madini ikiwa ni pamoja na uanzishwaji wa
masoko ya madini 38 na vituo vya ununuzi wa madini 39.
Katika
hatua nyingine Profesa Manya amesema kuwa ili kuhakikisha watanzania
wanashiriki kikamilifu kwenye Sekta ya Madini Tume ya Madini imekuwa
ikitoa elimu kuhusu ushirikishwaji wa watanzania kwenye Sekta ya Madini
(local content) ambapo mpaka sasa kampuni za uchimbaji wa madini nchini
zimeanza kutangaza fursa kwa ajili ya kutoa huduma kwenye shughuli za
utafutaji na uchimbaji wa madini na wananchi kushiriki.
Wakati huohuo kamisheni imeipongeza Tume ya Madini kwa kuvuka lengo la ukusanyaji wa maduhuli ambapo kwa robo ya kwanza ya mwaka wa fedha 2020-2021 imekusanya Sh Bilioni 65.294 sawa na asilimia 125 ya lengo la kipindi husika.
Kikao hicho kimeshirikisha Makamishna wa Tume ya Madini ambao ni pamoja na Katibu Mkuu wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Mary Makondo, Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Dkt. Evaristo Longopa na mwakilishi kutoka Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Daniel Barago.
Makamishna wengine ni pamoja na Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji wa Madini Tanzania (FEMATA), Haroun Kinega na Dkt. Athanas Macheyeki.
Pia kikao hicho kimeshirikisha viongozi kutoka Tume ya Madini ambao ni pamoja na Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Profesa Shukrani Manya, Mkurugenzi wa Huduma za Tume William Mtinya, Mkurugenzi wa Ukaguzi wa Migodi na Mazingira, Dkt. Abdulrahman Mwanga, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini, Venance Kasiki pamoja na maneja na watendaji wengine.