Muonekano wa baadhi ya mitaro katika mji wa Kahama baada ya watu wasio waamini na wanaokiuka masharti na maelekezo ya wataalam wa afya, kutapisha vyoo wakati wa mvua na kuleta kero kwa wananchi
Na Salvatory Ntandu, Kahama
Wakazi wa mjini Kahama Mkoa wa Shinyanga wameiomba Serikali kuwachukulia hatua za kisheria baadhi ya watu wanaotapisha vyoo katika mitaro ya barabara pindi mvua zinaponyesha ili kuzuia kutokea kwa magonjwa ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Shinyanga Press Club Blog jana, baadhi ya wananchi akiwemo Zabloni Michael ambaye ni mkazi wa Mtaa wa Majengo mjini hapa, alisema kuwa kumekuwa na tabia ya watu kutapisha vyoo vya vilivyojaa pindi mvua zinaponyesha ili kuepuka gaharama za kupeleka maji taka katika sehemu iliyotengwa.
Alisema kuwa endapo hatua stahiki zisipochukuliwa inaweza kusababisha madhara kwa wananchi kutokana na vinyesi kusambaa katika makazi ya watu pindi mitaro hiyo inapofurika maji husasani katika kipindi hiki cha mvua za Masika zinazoendelea kunyesha ili kudhibiti uchafuzi wa mazingira.
“Hatua kali za kisheria zichukuliwa kwa watu wanaotiririsha maji taka kwenye mitaro ili watoto wetu wasiendelee kuchezea maji yaliyochanganyikana na vinyesi, hali hii sio nzuri inaweza kusababisha mlipuko wa magonjwa,”alisema Michael.
Nyae Tabu Bilago Mkazi wa Mtaa wa Sokola mjini hapa, alisema kuwa awali viongozi wa mitaa kwa kushirikiana na maafisa afya na mazingira walikuwa wanatembelea kila kaya kuangalia ubora wa vyoo lakini kwa sasa suala hilo halifanyiki hali ambayo inawapa mwanya watu kutapisha vyoo pindi mvua zinapoanza kunyesha.
“Watu wanashindwa kulipia gharama za kusafirisha maji taka ambazo zimefikia shilingi elfu 60 hadi 80 kutoka kwa kampuni zinazofanya kazi hiyo na kuamua kutapisha pindi mvua zinaponyesha bila kujua madhara yake kwa afya za watu na mazingira,”alisema Bilago.
Kwa upande wake, Afisa Mazingira wa Halmashauri ya Mji Kahama, Johaness Mwebesa alisema kuwa hatua za kisheria zinaendelea kuchukuliwa kwa watu wanaobainika kutirisha maji taka katika mitaro ya barabara pindi mvua zinaponyesha na kuwataka wananchi kutoa taarifa kwa pindi wanapoona vitendo hivyo vikifanyika.
“Mpaka sasa zaidi ya watu 50 wameshachukuliwa hatua za kisheria ikiwemo kutozwa faini kwa kutirisha maji taka, niwaombe wananchi kuzingatia suala la usafi wa mazingira ili kuzuia kutokea kwa mlipuko wa magonjwa hususani katika msimu huu wa mvua za masika,”alisema Mwebesa.
Mwebesa alisema kuwa kwa siku halmashauri hiyo inazalisha taka ngumu zaidi ya tani moja, hivyo kuwataka wananchi kuendelea kushirikiana na vikundi vinavyozoa taka katika maeneo yao sambamba na kuhakisha wanakuwa na vipokelea taka katika nyumba zao (Dust bin) ili kuendelea kuweka mazingira safi ya Mji wa Kahama.
“Uzalishaji wa Taka katika Mji wa kahama ni mkubwa na unahitaji umakini katika utunzaji wa taka hizi niwaombe wananchi watoe ushirikiano kwa kampuni za uzoaji taka ili kurahisisha zoezi hilo na kuepuka kusambaa au kaa kwa muda mrefu taka katika vizimba,” alisema Mwebesa.
Moja ya mitaro ukiwa na maji machafu ambayo ni matokeo ya watu wasio waaminifu kutapisha vyoo wakati wa mvua
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464