ZIMAMOTO SHNYANGA YAKAGUA SHULE 30, YASEMA CHUKI NA MIGOGORO NI CHANZO CHA MAJANGA YA MOTO


Na Damian Masyenene –Shinyanga 
JESHI la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Shinyanga limefanya ukaguzi na kutoa ushauri kwa shule 30 tangu Oktoba, mwaka huu ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini, John Masunga na yale ya Wizara ya Mambo ya Ndani yaliyolitaka jeshi hilo kufanya ukaguzi kwenye shule zote za kutwa na bweni na kutoa mapendekezo ya namna ya kuzuia majanga ya moto.

Akizungumza na Shinyanga Press Club Blog ofisini kwake jana Novemba 16, 2020, Kamanda wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji mkoa wa Shinyanga, SF George Mrutu amesema ukaguzi huo ulianza kutekelezwa Oktoba, mwaka huu na unaendelea, ambapo lengo ni kufikia Desemba, mwaka huu wawe wamemaliza na kuzifikia shule zote na kuandaa ripoti itakayowasilishwa kwenye mamlaka husika.

Katika ukaguzi huo, shue 16 za sekondari (11 za bweni na tano za kutwa), saba za msingi (nne za kutwa na tatu za bweni) na saba za wilayani Kahama zilikaguliwa, huku ratiba ya mitihani ya mwisho wa mwaka na ile ya kitaifa ikielezwa kuchelewesha ukaguzi huo, huku akishauri shule kuwatumia mafundi umeme wenye taaluma, kwani mara nyingi shule zimekuwa zikiwatumia wanafunzi kama mafundi umeme ili kukwepa gharama.

“Mapendekezo mengine ni kwa shule kufanya ukaguzi wa mara kwa mara kwenye mabweni kama wanafunzi wanamiliki vifaa vya kutumia umeme, kuweka fensi kuzuia wapiti njia kufanya matukio, wasiweke ‘swith socket’ kwenye mabweni na pia kuwe na ulinzi wa usiku katika mabweni ili kuzuia hujuma zinazoweza kufanywa ili kuteketeza shule.

"Pia tumefanya ukaguzi kwenye viwanda, makampuni, taasisi na sehemu za biashara na kutoa mapendekezo mbalimbali yakiwemo kuweka ving’amuzi moshi (smoke detector) vitakavyobaini moshi katika hatua ya awali kabisa, kuawa na vizima moto na mfumo wa kutambua moto.....ukaguzi huu huisaidia Serikali kutokupata hasara kwani janga la moto linapotokea muathirika wa kwanza ni Serikali,” amesema.

KUFUATIA kuwepo kwa matukio ya mara kwa mara ya kuzuka kwa moto na kuteketeza majengo ya taasisi hususan shule za bweni za binafsi na makazi ya watu katika mazingira ya kutatanisha, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji limeshauri jamii kutatua migogoro na chuki binafsi zilizopo baina ya wanajamii ili kuepusha majanga hayo ambayo yanaelezwa kuwa yanachochewa na tatizo hilo. 

Amesema katika kaguzi nyingi zinazofanywa kwenye taasisi, makampuni, viwanda na makazi ya watu ambako moto unazuka imekuwa ikibainika kwamba wakati mwingine chuki binafsi na migogoro ndiyo chanzo. 

Kauli hiyo ya Kamanda Mrutu inakuja huku kukiwa na uchunguzi wa tukio la moto wa ajabu uliozuka wiki kadhaa mjini Kahama mkoani Shinyanga, ambapo moto huo hujiwasha wenyewe na kuunguza vitu vya ndani katika makazi ya watu kitongoji cha Hongwa mtaa wa Shunu Mjini humo. 

Kamanda Mrutu amesema kuwa wamekuwa wakitoa elimu kwa viongozi na wamiliki wa shule kukaa na watumishi na wanafunzi kuwauliza mahitaji yao na wawasikilize ili kuepusha majanga ya moto kwenye shule. 

“Kuna baadhi ya matukio ya moto shuleni husababishwa na Migogoro, unakuta labda wafanyakazi wana chuki na uongozi, ama wanafunzi hawasikilizwi na kuulizwa mahitaji yao. Kwahiyo tunashauri taasisi na makampuni yawe yanajitahidi kumaliza Migogoro ili kusije kuzuka matatizo hayo ya moto,” amesema. 

Kwa upande wake Mkuu wa Zimamoto Wilaya ya Kahama, Inspekta Hanafi Mkilindi, akabainisha kuwa kutokana na kasi ya ujenzi na ukuaji wa mji wa Kahama, Jeshi hilo limekuwa na wajibu wa kusoma ramani za majengo zinazoletwa katika halmashauri na kutoa mapendekezo ya vitu vya kuweka ili kuzuia majanga ya moto na pale yatakapotokea yadhibitiwe katika hatua ya awali. 


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464