Meneja Mradi wa KUPIMA na KUTIBU (Test & Treat) kutoka Shirika la Doctors With Africa, Veronicaa Censi (kushoto) akikabidhiwa cheti cha ushiriki mkubwa na mchango chanya katika mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi, kutoka kwa Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga (wa pili kulia) wakati wa maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani kwenye uwanja wa Halmashauri mjini Bariadi.
Na Damian Masyenene, Bariadi
SHIRIKA la Doctors With Africa (CUAMM) linalotekeleza mradi wake wa 'KUPIMA na KUTIBU (Test & Treat) katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu, leo Desemba Mosi, 2020 limeshiriki katika maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani kwa mkoa wa Simiyu yaliyofanyika katika Uwanja wa Halmashauri mjini Bariadi yakibebwa na kaulimbiu ya 'Twende pamoja na Jumuiya ya Kimataifa kutokomeza VVU na Ukimwi Simiyu'.
Katika maadhimisho hayo ambayo yalihudhuriwa na wadau mbalimbali wa sekta ya afya hususan inayohusiana na masuala ya VVU na Ukimwi, Shirika la Doctors With Africa liliendesha shughuli za ushauri nasaha, upimaji Virusi Vya Ukimwi na kutoa elimu ya lishe bora.
Ambapo maadhimisho hayo yalipambwa pia na burudani kutoka kwa Msanii wa HipHop nchini, Fareed Kubanda, huku Shirika la Doctors With Africa (CUAMM) likitunukiwa cheti kwa mchango wake chanya na ushiriki mkubwa katika mapambano ya VVU na Ukimwi.
Akizungumzia hali ya maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi Mkoa wa Simiyu, Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa huo, Dk. Khamis Kulemba kwa mujibu wa tafiti za mwaka 2016 na 2017 mkoa huo ulikuwa na maambukizi ya aasilimia 3.9, huku wilaya ya Maswa ikiwa kinara kwa asilimia 3.3, lakini kwa takwimu za mwaka huu jumla ya watu 237,739 wamepima na kutambua hali zao na 6,613 awa na asilimia 2.7 wana maambukizi.
Ameongeza kwa kubainisha kuwa kwa takwimu za Julai - Septemba, 2020 watu 64,820 waliandikishwa huduma za tiba na matunzo, 56,469 sawa na asilimia 87% wanatumia dawa za kufubaza makali ya VVU (ARV), miongoni mwa watu wote wanaotumia ARV, watoto ni 3991 sawa na asilimia 7.1.
"Moja ya mikakati tuliyonayo ni kwamba hivi karibuni huduma za watu kujipima (self test) zitaanza kutolewa mkoani kwetu, kujipima ni njia ya awali ya kutambua majibu, lakini tunashauri baada ya kujipima waende vituoni kupata vipimo vya uhakika na ushauri.
"Tunatoa pia huduma za tiba na matunzo kwa watu wenye VVU, kwa sasa vituo hivyo vinavyotoa huduma hizo bure ni 106, Pia huduma za tohara zinaendelea kutolewa, ambapo hadi mwaka huu jumla ya wanaume 194,704 walitailiwa na kufanya kuwa miongoni mwa mikoa iliyotekeleza vyema programu hiyo," amesema.
Kwa upande wake, Mgeni rasmi wa maadhimisho hayo, Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa mkoa, amesema siku hiyo ni muhimu kwa wadau wote kuhamasisha umma namna ya kuepukana na maambukizi mapya ya Ukimwi.
"Janga hili halitoweza kutoka kama hakutakuwa na matu walio mstari wa mbele, tunapaswa kushirikiana wenyewe kuanzia ngazi ya kaya hadi kimataifa...Kila mmoja akapime, ajitambue aishi kwa furaha na aanze dawa mapema.
"Tuache mila potofu zinazohamasisha maambukizi haya mfano kuwa na wenza wengi, kutoroka dawa na kwenda kuombewa kanisani na waganga wa jadi. Miujiza pekee ni kupima na kutumia dawa," amesisitiza.
Wanafunzi wa shule ya Sekondari Bariadi wakiwa kwenye maandamano wamebeba bango la maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani kwa mkoa wa Simiyu, wakati wakiingia katika uwanja wa halmashauri yalikofanyika maadhimisho hayo
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga na Kaimu Mganga Mkuu wa mkoa wa Simiyu, Dk. Khamis Kulemba (aliyevaa suti) wakitembelea na kukagua mabanda mbalimbali uwanjani hao
Baadhi ya wafanyakazi wa kitengo cha upimaji wakitoa maelezo kwa mgeni rasmi namna wanavyotimiza majukumu yao
Wananchi wakiendelea kupata huduma katika mabanda ya Shirika la Doctors With Africa
Wananchi wakipata huduma ya ushauri, vipimo na elimu ya lishe katika banda la Shirika la Doctors With Africa
Huduma mbalimbali zikiendelea kutolewa katika mabanda ya shirika hilo
Huduma zikiendelea kutolewa kwa wananchi katika banda la Doctors With Africa
Mmoja wa wananchi waliofika katika banda la Shirika la Doctors With Africa akipata elimu ya lishe
Mkuu wa Wilaya ya Bariadi, Festo Kiswaga ambaye alikuwa mgeni rasmi wa maadhimisho hayo, akizungumza na wananchi na wadau mbalimbali, ambapo amesisitiza kila mmoja kutimiza wajibu wake katika mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi
Wawakilishi wa Doctors With Africa wakiwa ni sehemu ya wadau wa heshima katika maadhimisho hayo
Baadhi ya maafisa wa CUAMM wakifuatilia kwa makini maadhimisho hayo
Mgeni rasmi akimkabidhi cheti cha kutambua mchango wao katika mapambano dhidi ya VVU na Ukimwi, mwakilishi wa Shirika la Doctors With Africa (CUAMM), Veronica Censi
Msanii wa HipHop, Fareed Kubanda (Fid Q) akitumbuiza katika maadhimisho hayo
Fid Q akiendelea kutoa burudani
Wawakilishi wa Shirika la Doctors With Africa (kulia) wakiwa ni sehemu ya meza kuu pamoja na mgeni rasmi
Viongozi wa meza kuu katika picha ya pamoja na baadhi ya viongozi wa kamati ya ulinzi na usalama ya mkoa
Wakurugenzi wa halamshauri katika mkoa wa Simiyu wakiwa katika picha ya pamoja na meza kuu
Meza Kuu katika picha ya pamoja na wawakilishi wa mashirika
Baadhi ya wahudumu wa afya ngazi ya jamii wakiwa katika picha ya pamoja na meza kuu
Wafanyakazi wa Doctors With Africa (CUAMM) wakiwa katika picha ya pamoja na Msanii wa HipHop, Fid Q ndani ya ofisi za shirika hilo mjini Bariadi
Wafanyakazi wa Shirika la Doctors With Africa (CUAMM) wanaosimamia mradi wa Test and Treat katika mikoa ya Shinyanga na Simiyu wakiwa katika picha ya pamoja kwenye ofisi ya shirika hilo iliyopo mjini Bariadi.