JPM: ALIYESHINDWA KUAPA NAFASI YAKE KUTEULIWA MWINGINE, ASAMEHE WAFUNGWA 3,316, WENGINE 256 WA KUNYONGWA WABADILISHIWA ADHABU

Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli

Na Shinyanga Press Club Blog
Katika moja ya matukio yaliyojiri leo wakati wa hafla ya kuwaapisha Mawaziri na Manaibu waziri Ikulu ya Chamwino, Dodoma, ni Naibu Waziri wa Madini, Ndulane Francis Kumba kushindwa kuapa, ambapo kitendo hicho hakijamfurahisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli ambaye amesema nafasi hiyo atateuliwa mtu mwingine mwenye uwezo wa kuapa na kusimamia kazi.

Katika hali isiyo ya kawaida, Ndulane Kumba alishindwa kuapa mbele ya Rais Magufuli kwa kushindwa kusoma vyema maneno ya kiapo.

Akizungumza baada ya kuwaapisha Mawaziri na manaibu waziri, Rais Magufuli amesema nafasi ya Kumba atatafutwa mtu mwingine, kwani hawezi kwenda na watu wasioweza kuwa hata na ujasiri wa kula kiapo.

Katika hatua nyingine, Rais Dk, John Magufuli amewapunguzia adhabu ya kunyongwa wafungwa 256 waliokuwa wamehukumiwa adhabu ya kunyongwa hadi kufa, ambapo amewabadilishia adhabu hiyo na sasa watafungwa kifungo cha maisha na kushiriki katika kufanya kazi.

Pia Rais Dk. Magufuli amesamehe wafungwa 3,316 wenye makosa madogo na wale waliotumikia kifungo kwa muda mrefu na kubakiza siku chache ambapo wamepunguziwa adhabu na kusamehewa.

Rais Magufuli amechukua hatua hiyo ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha Siku ya Uhuru wa Tanganyika ambayo huadhimishwa kila mwaka Desemba 9.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464