Rais wa Tanzania, Dk. John Magufului
Na Damian Masyenene
LEO Desemba 9, 2020, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli amewaapisha Mawaziri 21 na Manaibu 22 aliowateua hivi karibuni, katika hafla iliyofanyika Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma.
Akizungumza baada ya kuwaapisha viongozi hao, Rais Dk. Magufuli amesema kazi ya kuwachagua ilikuwa ngumu kwani
wabunge wote walikuwa wanafaa kupewa uwaziri au unaibu waziri, huku akibainisha kuwa ipo orodha ndefu ya akiba (reserve) kwahiyo ni kubandika tu na kubandua na kuwataka kwenda kufanya kazi.
JPM amesisitiza kwa kuwataka kila mmoja katika wizara yake akafanye yanayotakiwa, huku akiwaeleza kuwa siyo kwamba walioteuliwa ni wazuri sana, kuna vidosari viodogo vidogo wanavyotakiwa kuvirekebisha kwani yaliyopita si ndwele bali wagange yajayo kwa kutatua kero za Watanzania.
Hata hivyo, Rais Magufuli ameonesha kukerwa na kitendo cha baadhi ya viongozi anaowateua kushindwa kufanya maamuzi kwa kile wanachodai kuogopa kuonekana wabaya mbele ya macho ya watu, ambapo sasa amewapa mtihani viongozi hao wapya kwenda kufanya maamuzi wanayopaswa kutekeleza mara moja.
Miongoni mwa waliopewa mtihani huo, Ni Waziri wa Ofisi ya Rais -Tamisemi, Seleman Jaffo ambaye ametakiwa kumsimamisha kazi Mkurugenzi wa Halmashauri ya mji wa Geita kutokana na matumizi mabaya ya fedha za Serikali Sh Milioni 400 zilizolenga kuhudumia wananchi lakini akanunua gari la kutembelea.
"Ni vizuri kufanya uamuzi mbaya kuliko kutofanya uamuzi, kwa sababu tatizo letu tulilonalo watu hawataki kufanya maamuzi kwa kuogopa kuonekana wabaya.
"Jaffo, Tamisemi kuna changamoto nyingi sana, umefanya vizuri sana kuzunguka lakini kusimamia pesa bado sana. Kuna Mkurugenzi (Geita) kanunua gari la Sh Milioni 400, unakuta shule haina madawati, Mkuu wa Mkoa hana hilo gari, wakati fedha zimetolewa kuhudumia wananchi. Nataka kazi yako ya kwanza iwe kumfukuza huyo Mkurugenzi," amesisitiza Rais Magufuli.
Pia Rais Magufuli amemtaka Waziri wa Madini, Dotto Biteko kuongeza kasi ya uwajibikaji kwa kudhibiti utoroshaji wa madini ambao bado unaendelea kufanyika katika wilaya ya Chunya na madini ya Tanzanite.
Vilevile, amewapa mtihani Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Innocent Bashungwa na Naibu wake, Abdallah Ulega kutobweteka kwa kile kinachotajwa kuwa wamepata wizara nyepesi, ambapo amependekeza kuona uwezekano wa kuunda timu ya taifa ya soka isiyofungamana na timu za Simba na Yanga.
"Wizara zote ni muhimu, hakuna wizara ndogo wala kubwa, nawapongeza wote kachapeni kazi muwatumikie watanzania, naamini mtafanya makubwa sana.....Wizara ya michezo usione kama umepata wizara nyepesi, haiwezekani tukawa tu na Simba na Yanga, tunahitaji kushinda, inawezekana tukatengeneza timu ya taiofa isiyo na mahusinao na Simba na Yanga ikatuletea manufaa. mkifanya mchezo inawezekana ukaondoka mara moja wewe na naibu wako," ameagiza.
Kwa upande wa Wizara ya Elimu, Rais Magufuli amemuagiza Waziri Profesa Joyce Ndalichako kuhakikisha historia ya Tanzania inafundishwa kwenye shule kuliko mazoea ya kufundisha historia za mataifa ya nje, pia kuangalia uwezekano somo hilo kuwa la lazima.
Hata hivyo, Dk. Magufuli ameeleza sababu za kumpelea wizara ya biashara na uwekezaji aliyekuwa katibu mkuu wizara ya maji, Prof. Kitila Mkumbo, huku akibainisha kuwa hakufanya vizuri kwenye wizara hiyo, lakini kutokana na umahiri wake wa kuandaa maandiko na kuzungumza amempeleka kwenye uwekezaji ili avutie wawekezaji wengi.
MAWAZIRI, MANAIBU KUTOELEWANA
Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amekemea tabia ya mawaziri kujivika madaraka yote na kuwaacha manaibu wao wamekaa ofisini bila kazi, huku akiwataka manaibu hao kuchapa kazi na kuchangamka ili waonekane.
"Naomba mshirikiane, wakati mwingine mawaziri hamuwapangii kazi manaibu waziri wanakuwepo tu ofisini hawana kazi, nyinyi mmejibebesha majukumu yote, manaibu waziri msiogope kufanya kazi, msipofanya kazi hamtaonekana, ndiyo maana wengi wamepunguzwa waliaacha mawaziri wakafanya kazi zote.
USIRI SERIKALINI
Pia, Rais Magufuli amekemea tabia ya watumishi wa serikali kutokuwa na maadili na kuweka nyaraka za serikali kwenye makundi ya mitandao ya kijamii ikiwemo WhatsApp, kwani kitendo hicho huvujisha siri za serikali.
"Ukifanya kazi utajulikana tu....siri ndani ya serikali zinavuja kwa sababu viongozi wanatuma nyaraka za serikali kwenye magroup....hii ni kwa wote kuanzia mawaiziri, makatibu wakuu hadi makatibu tarafa.
"Saa nyingine naingia kwenye magroup yenu kusoma yaliyomo unashangaa tu, hadi kuna magroup ya polisi...tufanye kazi kwa uadilifu mkubwa na kuzingatia siri za serikali. Nimefurahi nimewateua wote kwa moyo mwema kabisa, trumeangalia mikoa yote walau kila mkoa kuwe na mwakilishi," amebainisha