KATAMBI AKAGUA UJENZI WA MADARASA JIMBONI, ACHANGIA SH MIL 23 KUKAMILISHA VYUMBA 24 OFISI 3

Naibu Waziri wa Wizara ya Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Patrobas Katambi (aliyeshika koleo), akishiriki katika kuondoa udongo kwenye msingi wa chumba kimoja cha darasa unaojengwa katika shule ya msingi Msufini iliyopo Kata ya Ndala Manispaa ya Shinyanga, leo wakati wa ziara yake ya kukagua ujenzi wa madarasa katika jimbo lake

Na Damian Masyenene –Shinyanga 
NAIBU Waziri wa Nchi ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Ajira, Patrobas Katambi ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo la Shinyanga Mjini (CCM), leo amefanya ziara ya kikazi jimboni humo kwa kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa ili kuhakikisha shule zitakapofunguliwa Januari mwakani wanafunzi wote waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza na wanaoanza darasa la kwanza waende shule. 

Katambi amefanya ziara hiyo katika kata nane za jimbo hilo ambazo ni Chamagua, Ndembezi, Ngokolo, Ibinzamata, Ndala, Kitangiri, Masekelo na Mwasele, huku akiambatana na Mstahiki Meya wa halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila na Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Geofrey Mwangulumbi pamoja na watumishi wa idara ya elimu na madiwani. 

Shule za msingi na sekondari zilizokaguliwa na Katambi katika ziara hiyo ni shule ya msingi Ushirika, Ndala A, Ibinzamata, Neghezi na Msufini, huku akizitembelea shule za sekondari za Mazinge, Ngokolo, Town, Mwasele, Busulwa, Ibinzamata, Masekelo na Ndala. 

Naibu Waziri Katambi amechangia jumla ya Sh Milioni 23 kwa ajili ya Kukamilisha ujenzi wa vyumba 24 vya madarasa na ofisi tatu za walimu katika shule 13 alizozitembelea kwenye kata nane za jimbo hilo. 

Akizungumza katika Ziara hiyo, Katambi ameeleza kuwa ujio wake ni msisitizo na utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa la kutaka ujenzi wa vyumba vya madarasa umalizwe ifikapo Februari 28, mwakani na kuhakikisha kwamba hakuna mwanafunzi anakosa nafasi ya kwenda shule kwa sababu ya upungufu wa madarasa. 

Naibu Waziri huyo amewashukuru wananchi wa jimbo hilo kwa ushirikiano mkubwa waliouonyesha wa kuchangia nguvu katika ujenzi wa vyumba hivyo wakisaidia kwa kuchanga fedha, kuchimba misingi, kusomba kokoto na maji pamoja na kusaidia kazi za ufundi kwa gharama nafuu, huku akibainisha kuwa fedha alizoahidi zitakabidhiwa kupitia ofisi ya Mkurugenzi wa manispaa. 

Kwa upande wake, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila, ambaye alichangia Sh 100,000 na mifuko mitano ya saruji katika shule ya sekondari Mazinge, amesema kuwa halmashauri imewaelekeza wataalam wajipange ujenzi huo uwe mpango endelevu utakaosaidia kumaliza changamoto ya upungufu wa madarasa. 

“Kwa sasa kila shule inafanya harakati za kumaliza ujenzi wa madarasa yanayohitajika kwa uharaka ili watoto waweze kuripoti shuleni kwa muda unaohitajika. Tulivyojipanga baada ya kumaliza hili jambo la haraka, tutaendelea kujenga madarasa ili yawepo muda wote yatakapohitajika,” amebainisha. 

Naye Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Geofrey Mwangulumbi amesema kuwa halmashauri ilitoa walau Sh Milioni 5 kwa baadhi ya shule zenye uhitaji mkubwa na zingine Sh Milioni 2.5 kwa ajili ya utekelezaji wa agizo hilo, huku akiweka wazi kuwa kwa sasa wanao upungufu wa vyumba 100 vya madarasa vikiwemo 34 kwa shule za sekondari na 66 kwa Shule za msingi. 

Ambapo jumla ya Sh Bilioni 2 zinahitajika kwa ajili ya ujenzi wa vyumba hivyo, hivyo akaomba ushirikiano kwa wadau wote na kwamba Kamati ya fedha ya manispaa hiyo ikiongozwa na Mstahiki Meya ilibuni mikakati kadhaa ikiwemo kuchangisha wananchi na wadau wengine wa maendeleo. 

Vile vile, Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abubakari Gulam ameahidi kutoa mifuko 10 ya Saruji itakayokabidhiwa wiki ijayo katika shule ya Sekondari Ngokolo kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa, aahadi hiyo imetolewa baada ya Kaimu Mtendaji wa Kata ya Ngokolo, Salum Soud kuelezea kuwa wanao upungufu wa vyumba 8 vya madarasa, vikiwemo vya haraka vinne, ambapo tayari wameanza na vitatu.

TAZAMA MATUKIO KATIKA PICHA
Naibu Waziri Patrobasi Katambi (kushoto aliyekaa) akisaini kitabu cha wageni baada ya kufika katika shule ya msingi Ushirika iliyopo kata ya Chamagua kwa ajili ya kuanza ziara yake ya kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa
Mheshimiwa Katambi pamoja na viongozi wengine wakikagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya Msingi Ushirika
Afisa Elimu Kata ya Chamagua, Fransisca Msindu akitoa taarifa ya maendeleo ya ujenzi wa madarasa katika kata yake
Mh. Katambi akizungumza na viongozi mbalimbali baada ya kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya sekondari Ngokolo


Afisa Elimu Kata ya Mwawaza, Jacob Sallu akisoma taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa katika kata hiyo
Naibu Waziri Katambi akishiriki kubeba mchanga kwa ajili ya kuujaza kwenye msingi unaojengwa chumba kimoja cha darasa katika shule ya Msingi Neghezi
Naibu Waziri Katambi na Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Shinyanga Mjini, Abubakar Gulam wakishiriki kujaza udongo kwenye msingi unaojengwa kwa ajili ya vyumba viwili vya madarasa katika shule ya sekondari Town
Naibu Waziri Katambi (aliyebeba tofali) akimsaidia fundi kuweka tofali kwenye msingi unaojengwa kwa ajili ya vyumba viwili vya madarasa katika shule ya Sekondari Masekelo 
Naibu Waziri Katambi akishiriki katika kuchimba msingi kwenye shule ya Msingi Msufini
Naibu Waziri Katambi akichota mchanga na Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Geofrey Mwangulumbi akitega ndoo kwa ajili ya kuweka mchanga huo wakati wa ziara yao ya kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa katika shule ya Sekondari Town
Katambi (aliyesimama kushoto) akifurahia jambo na mafundi wanaojenga madarasa katika shule ya Sekondari Mwasele, baada ya kufika shuleni hapo kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa
Naibu Waziri Katambi akikaribishwa na baadhi ya wanachama wa CCM katika Kata ya Ndembezi alipowasili katika shule ya Sekondari Mazinge kukagua ujenzi wa vyumba vya madarasa
Mheshimiwa Katambi akimkabidhi fundi ndoo yenye mchanga kwa ajili ya kuumwaga katika msingi unaojengwa vyumba viwili vya madarasa katika shule ya sekondari Town
Naibu Waziri Katambi akikaribishwa na baadhi ya wanachama wa CCM alipowasili katika shule ya sekondari Ibinzamata
Mheshimiwa Katambi akisalimiana na baadhi ya akina mama waliofika kwenye ziara yake katika shule ya msingi Msufini
Naibu Waziri Katambi akizungumza na baadhi ya wanafunzi wa shule ya msingi Ibinzamata
Katambi akizungumza na wanafunzi wa shule ya sekondari Ibinzamata
Jengo lenye chumba kimoja cha darasa linalojengwa katika shule ya sekondari Ngokolo
Jengo la chumba kimoja cha darasa na ofisi ya mwalimu mkuu linalojengwa katika shule ya sekondari Busulwa iliyopo Kata ya Kitangiri
Jengo la vyumba viwili vya madarasa na ofisi ya walimu ambalo limefikia katika hatua ya umaliziaji linalojengwa katika shule ya msingi Ibinzamata 

Mkuu wa shule ya sekondari Ndala, Iman Chambulilo (kulia) akisoma taarifa ya ujenzi wa vyumba vya madarasa shuleni hapo
Mh. Katambi akitoa maelekezo mbalimbali kwa viongozi baada ya kufanya ukaguzi katika shule ya sekondari Ngokolo
Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Geofrey Mwangulumbi akitoa maelezo mbele ya Naibu Waziri Patrobas Katambi wakati wa ziara yake katika shule ya msingi Ndala A

Mkuu wa shule ya msingi Town, Jason Rwegasira akisoma taarifa ya utekelezajiwa ujenzi wa vyumba vya madarasa shuleni hapo
Kaimu Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Ndala A,Rajabu Khamsini akisoma taarifa 
Mafundi wakichimba msingi kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa  katika shule ya msingi Msufini
Mafundi wakiendelea na kazi ya kuchimba msingi katika shule ya msingi Neghezi
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila akiwa amebeba ndoo yenye mchanga kwa ajili ya kuujaza katika msingi wa chumba kimoja cha darasa katika shule ya msingi Neghezi
Mkurugenzi wa Manispaa ya Shinyanga, Geofrey Mwangulumbi (aliyeshika karatasi) akitoa maelezo kwa Naibu Waziri Patrobas Katambi wakati wa ziara yake katika shule ya sekondari Mazinge
Msingi wenye vyumba viwili vya madarasa katika shule ya sekondari Mazinge
Msingi wenye vyumba viwili vya madarasa katika shule ya sekondari Mwasele
Mafundi wakiendelea na shughuli za ujenzi wa msingi katika shule ya sekondari Ngokolo
Msingi utakaojengwa chumba kimoja cha darasa katika shule ya sekondari Ndala
Msingi utakaojengwa darasa lenye vyumba viwili katika shule ya msingi Ushirika
Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Shinyanga Mjini, Abubakar Gulam akiwa amebeba ndoo yenye mchanga kwa ajili ya kuujaza kwenye msingi unaojengwa chumba kimoja cha darasa katika shule ya msingi Neghezi
Mkuu wa shule ya sekondari Masekelo, Stephen Mihambo akitoa taarifa ya ujenzi wa vyumba vya madarasa shuleni hapo
Naibu Waziri Katambi akitoa maelekezo kwa Mkuu wa Shule ya Sekondari Mwasele, Suzana Manoni (kulia) wakati wa ziara yake shuleni hapo

Katambi akifurahia jambo na wanafunzi wa shule ya sekondari Ibinzamata
Ukaguzi ukiendelea
Ukaguzi ukiendelea


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464