Wanafunzi wahitimu wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari KOM iliyopo Manispaa ya Shinyanga wakiingia ukumbini wakati wa mahafali yao ya 12 iliyofanyika shuleni hapo Desemba 5, mwaka huu
Na Suzy Luhende, Shinyanga
Afisa Elimu wa Mkoa wa Shinyanga, Mohamedi Kahundi amewataka wazazi na walezi kuacha kuwaozesha watoto wa kike wanaohitimu kidato cha nne badala yake wawalee vizuri wakati wakisubiri matokeo ili waweze kuendelea na masomo ya juu.
Pia amewaomba wazazi wasiwaachie waende sehemu ambazo hazifai maana kuna wazazi wengine wanaona kwamba wamemaliza shule hivyo kuwaruhusu kwenda mahotelini, kutembea hovyo bila sababu, walindeni ili waweze kuendelea na masomo ya juu wasiishie njiani.
Hayo ameyasema leo kwenye mahafali ya 12 ya shule ya Kom iliyofanyika katika shule hiyo iliyoko manispaa ya Shinyanga mkoani hapa, ambapo aliwataka wazazi na walezi kipindi hiki cha kusubiri matokeo waache kuwaozesha watoto wa kike, badala yake wawalee vizuri na kuwafundisha kazi za nyumbani huku wakisubiri matokeo yao.
"Nawaombeni sana wazazi wenzangu hawa watoto bado wanafunzi msije mkawaona weupe hivi mkaanza kuhesabu mahali, waacheni wasubiri matokeo yao ili waweze kusonga mbele, kwani kwa sasa bado watoto wadogo na msiwaruhudu kutembea tembea hovyo muwalonde"amesema Kahundi.
"Wazazi wengine wamekuwa wakiwaacha watoto wadogo wanaenda kwenye mahoteli makubwa na wanakuja na fedha na wazazi mnatumia bila kuuliza mnazitoa wapi, msipende hela za watoto pendeni elimu,kama mtoto atakushinda tafuta vyombo vya ulinzi vikulindie asitoke hovyo mtoto wa kike,na nyinyi watoto wa kike mnatakiwa kuwa watiifu kwa wazazi wenu," amesisitiza.
Pia amewataka watoto wa kiume wasijiunge na makundi ambayo sio mazuri ambayo yanaweza kuwaharibu na huku wamemaliza wakiwa wanatabia nzuri.
Aidha amewataka wanafunzi wanaobaki waendelee kusoma kwa bidii ili waweze kufaulu vizuri wawe watoto wanaoipenda elimu na wahakikishe wanaondoa ziro.
"Nawapongeza sana walimu mlioajiliwa hapa kwani mnasifa nzuri ya ufundishaji ndio maana watoto wanafaulu vizuri, kwani mnafanya jitihada kubwa ya kufundisha watoto, nampongeza mkurugenzi wa shule hii Jakton Koyi anaajili walimu wanaojitoa vizuri na wana wito"amesema Kaundi.
Kwa upande wake Mkuu wa Shule hiyo, Mwita Warioba wakati akisoma taarifa ya shule amesema shule hiyo ilisajiliwa Januari 2006 ikiwa na jumla ya wanafunzi 88 wa kidato cha kwanza ikiwa na walimu watano na wafanyakazi wasio walimu sita na kwa sasa ina jumla ya wanafunzi 563 kati ya hao 309 ni wavulana na 254 ni wasichana na ina jumla ya walimu 37 ambapo 27 ni wanaume na 10 ni wanawake, wafanyakazi wasio walimu 18 ambapo 10 ni wanaume na saba wanawake jumla ya watumishi wote 55.
Hivyo uwiano wa mwalimu na mwanafunzi ni mwalimu mmoja kwa wanafunzi 10 na tano, na dira ya shule ni kutoa elimu iliyobora kwa vijana wote bila kujali itikadi zao za kidini, kisiasa, kabila ama rangi, na azima ya shule hiyo ni kuandaa mazingira mazuri ya kijifunza na yanayomwezesha mwanafunzi kujifunza vizuri na kuweza kukabiliana na changamoto za baadae.
Warioba amesema changamoto inayowakabili ni gharama kubwa za uendeshaji ambazo kwa kiasi kikubwa zinazosababishwa na mfumko wa bei na kupanda kwa gharama za maisha kwa ujumla, pia zingineni baadhi ya wazazi kutolipa ada kwa wakati na hivyo kuwafanya watoto wachelewe kufika shuleni kwa wakati pindi shule inapofunguliwa ambapo hali hii huwaathili sana wanafunzi katika maendeleo yao kitaaluma.
Mkurugenzi wa shule hiyo, Jackton Koyi amesema anawaomba wazazi wawe wanawawahisha watoto shuleni kwa ajili ya kuendelea na masomo, wanapowachelewesha wanakuwa wanapitwa na masomo.
Mmoja wa wanafunzi wahitimu wa shule hiyo Phinias Denisi amesema anaamini atafaulu vizuri kwa sababu alikuwa anafundishwa vizuri na kusimamiwa vizuri na walimu wake, hivyo amewaomba na wanafunzi wanaobaki wawasikilize walimu ili waweze kufaulu vizuri.
TAZAMA PICHA CHINI
Mgeni rasmi wa mahafari hayo, ambaye ni Afisa Elimu wa Mkoa wa Shinyanga Mohamed Kahundi akizungumza na wahitimu pamoja na wageni mbalimbali waliofika kushuhudia
Mkurugenzi wa shule ya Kom Jackton Koyi akizungumza kwenye Mahafali ya 12 ya kidato cha nne
Mkurugenzi wa shule ya sekondari Kom iliyoko manispaa ya Shinyanga, Jackton Koyi akimkabidhi zawadi mgeni rasmi ambaye ni Afisa Elimu wa Mkoa wa Shinyanga Mohamed Kahundi
Mmoja wa wanafunzi wahitimu wa kidato cha nne, Finias Denis akikabidhiwa cheti na Afisa elimu wa Mkoa wa Shinyanga, Mohamedi Kahundi
Wazazi wakiwa kwenye mahafari ya watoto wanaohitimu kidato cha nne shule ya Kom sekondari
Wanafunzi wanaohitimu kidato cha nne wakimsikiliza Afisa elimu akiwataka wakatulie kusubiri matokeo wasikimbile kuolewa
Wanafunziwa wahitimu kidato cha nne wakiingua ukumbini
Wanafunzi wa shule ya msingi Kom wakiimba kwenye sherehe ya mahafari ya kidato cha nne katika shule ya sekondari Kom
mkurugenzi msaidizi wa shule ya kom akifurahia baada ya kuimba vizuri watoto wa shule ya msingi kom
Wanafunzi wahitimu wakisoma Risala katikamahafari ya 12 ya kidato cha nne katika shule ya Kom sekondari