Mratibu wa mafunzo hayo kutoka shirika la kimataifa la Pathfinder international, Meshack Molel akitoa mafunzo kwa waandishi wa habari jijini Mwanza
Na Salvatory Ntandu, Mwanza
Baraza la Habari Tanzania(MCT) kwa kushirikiana na Shirika la kimataifa la Pathfinder limetoa mafunzo kwa waandishi wa habari 30 kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa kuhusiana na namna bora ya kuandika habari zinazohusiana na mgawanyo wa watu na faida zake.
Akifungua mafunzo hayo ya siku moja jana kwa niaba ya baraza hilo, Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza (MPC), Edwin Soko alisema kuwa MCT kwa kushirikiana na shirika hilo wameamua kuwajengea uwezo wa kuandika habari hizo kwa weledi ili kuleta tija kwa taifa.
Alisema kuwa MCT kwa kushirikiana na Pathfinder imeona ipo haja ya waandishi wa habari nchini kuandika taarifa zinazohusiana faida za kiuchumi zitokanazo na ongezeko la watu ili kuleta matokeo chanya pindi mamlaka zinapotaka kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo.
"Fanyeni kazi kwa weledi,maarifa na tangulizeni uzalendo,mafunzo haya ni muhimu kwenu,yatumieni kuleta mabadiliko katika utendaji kazi wenu wa kila siku ili kuongeza ufanisi na tija katika lengo lililokusudiwa,"alisema Soko.
Kwa upande wake Mratibu wa mafunzo hayo kutoka shirika la kimataifa la Pathfinder International, Meshack Molel alisema kuwa wamezinfua mwongozo maalum utakaowawesha wanahabari kuripoti habari zinazohusiana na mgawanyo wa idadi ya watu(Demographic dividend)
"Tutawajegea uwezo wanahabari kuhusiana na kuwapa mbinu zitakazo wawezesha kuandika habari kuhusiana na jinsi gani mgawanyo wa idadi ya watu na faida zake kiuchumi,elimu,afya na kiutawala," alisema Moleli.
Nae Paul Malimbo mwezeshaji kutoka (MCT) alitoa rai kwa wanahabari hao kuzingatia mwongozo huo ili habari watakazo ziandika ziweze kuleta tija kwa wananchi na mamlaka zinazohusika na utungaji wa sera ambazo zitasaidia kuhamasisha kuendelea kwa shughuli za maendeleo na kupunguza hali ya utegemezi.
Glory Kiwia ni mmoja wa washirika wa mafunzo hayo na Mwandishi wa kutoka Jembe Fm aliishukuru MCT na Pathfinder international kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yanafaida kubwa kwao pindi yakitelezwa kikamilifu.
"Tunawaahidi kuuzingatia mwongozo huu,na pia tutakuwa mabalozi kwa wenzetu ambao hawajapata mafunzo hayo tunaomba MCT iendelee kutoa mafunzo mbalimbali kwetu ili kuhakikisha taaluma hii inasonga mbele," alisema Kiwia.
Mafunzo hayo yamehusisha waandishi wa habari 30 kutoka mikoa ya Shinyanga,Mwanza,Geita,Simiyu,Kagera na Mara.
Mmoja wa washiriki wa mafunzo hayo, Josephine Charles akitoa maelezo juu ya masuala mbalimbali