Mwenyekiti wa Mtaa wa Dome uliopo Kata ya Ndembezi manispaa ya Shinyanga, Solomon Najulwa akizungumza na wananchi wake katika mkutano wa mtaa huo kwa ajili ya kuhamasisha uchangiaji wa ujenzi wa vyumba vya madarasa
Na Suzy Butondo, Shinyanga
Mwenyekiti wa mtaa wa Dome uliopo kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga, Solomon Najulwa amewataka wananchi wa mtaa huo kuchanga Shililingi 13,000 kwa ajili ya kununua nondo za kujengea madarasa ya shule ya sekondari ya Mazinge ili wanafunzi waliofaulu waweze kukuta madarasa na kuendelea na masomo.
Agizo hilo amelitoa jana kwenye mkutano wa kutoa taarifa kwa kazi walizozifanya kwa muda wa mwaka mmoja ambapo aliwaomba wazazi na walezi kuchangia fedha za kununulia nondo kwa ajili ya kujengea madarasa ambayo yanamaliziwa kujengwa kwa ajili ya wanafunzi waliofaulu kidato cha kwanza.
Najulwa alisema madarasa hayo ya shule ya Mazinge sekondari iliyopo kata ya Ndembezi tayari yameshajengwa bado kazi ndogo tu ya kumalizia, hivyo ni vizuri mzazi kuchangia na kujitoa kwenda kusaidia mafundi wanaoendelea kujenga mahali pale kubeba zege mchanga ili kufanikisha ujenzi wa madarasa hayo kwa wakati unaotakiwa.
Pia Najulwa alisema katika kipindi cha mwaka mzima wamefanikiwa kuwatambulisha wazee saba kwa ajili ya kupata msamaha wa matibabu na wazee 13 wamewatambulisha TRA kwa ajili ya kupata msamaha wa kulipa kodi ya majengo.
"Katika kuendelea kuimarisha mtaa wa Dome tumefanikiwa kukaa na wazazi wenye watoto watukutu na watoto wao na watoro shuleni na kuwaonya waache tabia ya utukutu na utoro shuleni na sasa wameacha, na wanafunzi wanahudhulia vizuri darasani"alisema Najulwa.
Aidha alisema wamebaini walengwa wapya wa Tasaf 2020 na wameitisha mkutano wa mtaa kwa mujibu wa sheria, pia wamehamasisha vijana kina mama na watu wenye ulemavu kuunda vikundi ili wapewe mkopo manispaa usio na riba na kuhamasisha vijana kutumia vipaji vyao mbalimbali kufanya michezo.
Najulwa amesema wamesimamia usalama katika mtaa na kuondoa viashiria vilivyokuwa vinajitokeza vya vibaka, na wamefanikiwa kupitisha barua za mikopo ya mashirika mbalimbali ya kifedha kwa wakazi wa mtaa wa Dome idadi yao 168.
Pia wamefanikiwa kusuruhisha migogoro midogo midogo nakupatanisha watu 18 na kuishi kwa amani na kuwatambulisha wakazi 132 kuomba vitambulisho vya Uraia Nida.
Wameimalisha vikundi vya kina mama kuhusu utumiaji wa vyoo safi na kuweka ndoo chooni ya kutunza taka, na pia ofisi ilipokea mradi wa barabara kutoka serikalini ya kilomita 2.6 ambayo tayari ilishakwanguliwa na kufunguliwa njia zingine ambazo zilikuwa hazipitiki.
Katika mkutano huo pia walifanikisha kutambulisha kamati ya usafi na mazingira mpya (WES) ambayo itasimamia usafi wa mtaa na kuendelea kuimalisha usafi nyumba kwa nyumba.
Mwenyekiti huyo aliwatambulisha kamati ya mazingira kuwa ni Josephine Charles, Amina Mjange, Dorcas Matete, Baraka Charles, Samson Jeremiah.
Kasmili Almack ambaye alikuwa Katibu wa Kamati ya WES alisema amefanya kazi hiyo kwa muda wa miaka mitano lakini wananchi bado hawajaelimika katika kufanya usafi wa mazingira hivyo inatakiwa manispaa kutoa elimu kwa viongozi waliochaguliwa ili wakaelimishe wananchi wa mtaa wa Dome.
Mwenyekiti Najulwa akiendelea kuzungumza na wananchi wake katika kikao hicho
Wananchi wa mtaa wa Dome wakifuatilia maagizo ya mwenyekiti wao
Vijana waliohamasishwa kufanya michezo mbalimbali na kuonyesha vipaji vyao katika mtaa wa Dome wakiendelea kuonyesha michezo katika mkutano huo