Meneja wa Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) mkoa wa Shinyanga, Lwitiko Ndigha
Na Damian Masyenene, Shinyanga
KATIKA kuhakikisha wanaepusha usumbufu kwa wapangaji na gharama, Shirika la Nyumba la Tiafa (NHC) Mkoa wa Shinyanga limewaomba wateja (wapangaji) wake kulipa kodi kwa wakati ili kuondokana na kero mbalimbali zinazoweza kujitokeza.
Wito huo umetolewa leo na Meneja wa NHC mkoa wa Shinyang, Lwitiko Ndigha katika mahojiano yake na Shinyanga Press Club Blog ofisini kwake, ambapo ameeleza kuwa kuelekea mwisho wa mwaka na mwanzo wa mwaka ni vyema wateja wakalipa kodi zao kwa wakati ili kuepuka gharama na usumbufu wa kulimbikiza madeni sugu na hatimaye kuondolewa na kuingia gharama za kulipa faini na udalali.
Ndigha ameeleza kuwa wateja wa shirika hilo wamepewa fursa ya kulipa kidogo kidogo ndani ya mwezi husika wa kodi ili kutolimbikiza madeni, huku akibainisha kuwa wateja wanaokaidi kulipa na kuleta usumbufu hulisababishia usumbufu shirika.
“Kwetu hapa (Shinyanga) hatuna changamoto sana ya malimbikizo ya madeni (wadaiwa sugu), wengi ni wa miezi miwili na tumekuwa tukiwaandikia notisi….changamoto ya wapangaji wetu, unampa taarifa na anasaini notisi ukienda kumtoa ndiyo anaanza kulia na kuleta visingizio, kwahiyo tunawahimiza walipe kwa wakati kuepusha huu usumbufu,” ameeleza.
“Tunaendelea kutoa elimu na kuwapa taarifa kwa wakati kwa njia mbalimbali ikiwemo ujumbe mfupi, kuwapigia simu na kuwapa namba za malipo kuwakumbusha juu ya makusanyo ya kodi…..siyo kipaumbele chetu kumuondoa mpangaji kwenye pango na hilo ni suluhisho la mwisho kabisa, lengo letu ni kumfanya mteja alipe kodi yake,” amesisitiza.
NHC mkoa wa Shinyanga inao jumla ya wateja (wapngaji) 262 wa biashara na makazi, huku wakiendelea kufanya matengenezo na maboresho ya majengo yao kwa njia ya dharura na yaliyoko kwenye mpango kazi.
“Kwa mkoa wetu mwaka huu majengo yetu karibu yote tumeyaboresha kwa kupaka rangi na maboresho mengine, tutaendelea kufanya matengenezo na kutembelea majengo yote yenye changamoto ili majengo yetu yaendelee kuwa imara, kwa Shinyanga sehemu kubwa ya changamoto zilizobaki ni paa ambazo baadhi zinavuja,” amefafanua.
Katika hatua nyingine, Ndigha ameeleza kuwa shirika hilo linatambua changamoto za makazi kwa watumishi wa umma katika halmashauri mpya za Ushetu na wilaya ya Shinyanga ambazo watumishi wanalazimika kukaa mbali na sehemu zao za kazi, hivyo tayari shirika limeanza kufanya juhudi mbalimbali ikiwemo kupata maeneo ya viwanja.
“Kuna changamoto ya nyumba za watumishi katika halmashauri za Ushetu, Manispaa ya Shinyanga na wilaya ya Shinyanga, suala hili tayari tumelitolea macho mipango ipo. Pia tunatoa fursa kwa wadau kwamba NHC pia ni wakandarasi tunajenga nyumba na majengo mbalimba, kwahiyo tunawakaribisha,” amebainisha.
Muonekano mpya wa mojawapo ya nyumba za shirika hizo iliyopo Mtaa wa Miti Mirefu mjini Shinyanga, iliyofanyiwa maboresho mwaka huu
Muonekano wa zamani wa nyumba hiyo kabla ya kufanyiwa ukarabati
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464