Mbunge wa Jimbo la Ushetu wilayani Kahama, Elias Kwandikwa (CCM) akizungumza wakati wa harambee ya kuchangia ujenzi wa kituo cha tiba na matunzo kitakachojengwa Mapamba.
Na Shinyanga Press Club Blog
JUMLA ya Sh Milioni 6,838, 100 taslimu na ahadi zimechangwa katika harambee ya ujenzi wa kituo cha tiba na matunzo kwa watu wanaoishi na maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU), ambacho kitajengwa Kata ya Mapamba halmashauri ya Ushetu wilayani Kahama.
Harambee hiyo ambayo iliongozwa na Katibu Tawala wa Wilaya ya Kahama, Timoth Ndanya iliendeshwa kwenye Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani kwa mkoa wa Shinyanga yaliyofanyika Desemba Mosi katika Uwanja wa Mapamba, Ushetu.
Ndanya alisema kuwa wameamua kuendesha harambee hiyo ili kutafuta fedha zitakazosaidia kujenga kituo hicho katika kata ya Mapamba, ambapo aliahidi kusimamia ujenzi wake.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Elias Kwandikwa (CCM) ambaye alichangia Sh Milioni 2.4, aliwashukuru wadau waliojitokeza na kuchangia katika harambee hiyo, huku Mbunge wa viti Maalum mkoa wa Shinyanga, Santiel Kilumba akitoa Shilingi 500,000 kwa ajili ya kuunga mkono jitihada za ujenzi wa kituo hicho.
Nao baadhi ya wananchi wa Kata ya Mapamba ilikofanyika harambee hiyo na kutakapojengwa kituo hicho walitoa michango wa nguvu kazi ikiwemo Kokoto,mawe na mchanga kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa kituo hicho kitakachotoa huduma katika halmashauri zote za mkoa wa Shinyanga na mikoa jirani.
Mgeni rasmi wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani, Timoth Ndanya (wa pili kushoto) akisikiliza maelezo kutoka kwa Afisa Tathmini na Ufuatiliaji Shirika la Agape, Prosper Ndaiga
Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi Mkoa wa Shinyanga, Dk. Peter Mlacha akitoa taarifa ya hali ya maambukizi mkoa wa shinyanga
Baadhi ya wanafunzi walioshiriki kwenye maadhimisho hayo
Baadhi ya wananchi wa Kata ya Mapamba halmashauri ya Ushetu wakifuatilia maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika kijijini hapo