Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga (RAS), Albert Msovela
Na Damian Masyenene, Shinyanga
ILI Kuhakikisha wanatekeleza kwa asilimia 100 agizo la Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa la kuitaka mikoa yote nchini kuhakikisha kwamba watoto wote walioandikishwa darasa la kwanza na waliofaulu kwenda kidato cha kwanza mwakani lazima waingie darasani, Mkoa wa Shinyanga tayari umeanza utekelezaji kwa kuziagiza halmashauri zote za mkoa huo kutatua changamoto za miundombinu ya shule ikiwemo upungufu wa vyumba vya madarasa na madawati.
Jumla ya wanafunzi 26,382 wamefaulu mtihani wa kumaliza darasa la saba mkoa wa Shinyanga ikiwa na ongezeko ikilinganishwa na wanafunzi 23,634 sawa na asilimia 77.76 waliofaulu mwaka jana, ambapo mkoa huo umejipanga kuhakikisha kuwa ifikapo Januari 10, mwakani vyumba vyote vya madarasa vinavyojengwa viwe tayari kutumika kwa wanafunzi na kuanza masomo, pia ujenzi wote wa miundombinu hiyo utumie mfumo wa False Akaunti na mwishoni mwa Desemba, mwaka huu tatthmini itafanyika kuona utekelezaji umeendaje.
Hayo yameelezwa leo Desemba 14, 2020 na Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela wakati akifanya mahojiano maalum na waandishi wa habari ofisini kwake mjini Shinyanga, huku akibainisha kuwa tayari wameziagiza halmashauri kufanya tathmini ya mahitaji na mapungufu ya miundombinu hiyo ili yaweze kushughulikiwa, ambapo tayari baadhi ya halmashauri zimeanza utekelezaji kwa kujenga maboma.
RAS Msovela amesema utekelezaji huo wa ujenzi wa vyumba vya madarasa unatazamiwa walau kufika Januari 10, mwakani uwe umefikia hatua kubwa kuhakikisha kuwa vyumba vinavyovijenga watoto waweze kuvitumia, ambapo Sekretariet ya mkoa inategemea baada ya wiki moja kutoka sasa ianze kufanya ukaguzi wa utekelezaji wa majukumu hayo katika halmashauri.
“Kama mkoa tumejipanga vizuri kuona watoto wote walioandikishwa darasa la kwanza na kujiunga na kidato cha kwanza wote wanakwenda shule, hilo halina wasiwasi na pia tutafuatilia kuhakikisha watoto wote watakaochaguliwa wanakwenda shule,” amesisitiza.
Kwa mujibu wa Kaimu Afisa Elimu wa Mkoa wa Shinyanga, Dedan Rutazika, ambaye pia ni Afisa Elimu ya watu wazima mkoani Shinyanga, amebainisha kuwa kiwango cha ufaulu kimeongezeka kutokana na Serikali kuboresha maslahi ya walimu, miundombinu, kuongeza vitabu shuleni pamoja na jitihada binafsi za walimu.
Hata hivyo, inaelezwa kuwa kuwa mkoa wa shinyanga unayo mahitaji ya vyumba 528 vya madarasa, huku vilivyopo vikiwa 387 na upungufu ukiwa ni vyumba 141.