Faru
SHIRIKA la Hifadhi za Taifa(Tanapa) limesema hivi karibuni litaruhusu mtu yeyote anayetaka jina lake litumike kupewa mnyama faru kufanya hivyo, lakini baada ya kulipia kiwango fulani cha fedha.
Kwa sasa Tanapa inakamilisha boma la kuwahifadhi faru katika Hifadhi ya Taifa ya Mkomazi mkoani Kilimanjaro na mkoani Tanga. Baada ya kukamilisha taratibu za kuwahifadhi hapo, watu wataruhusiwa kuwapa majina yao.
Hayo yamebainika wakati wa uwasilishwaji wa mada kwenye mkutano wa mwaka wa wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari na Tanapa, uliofanyika mwishoni mwa wiki jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi KItengo cha Ulinzi na Mikakati ya Kiusalama wa Tanapa, John Nyamhanga, suala hilo la kutoa majina ya watu kwa faru, linafikiriwa na litaanza baada ya kukamilisha kuwajengea boma wanyama hao ambao ni miongoni mwa walio hatarini kutoweka duniani kutokana na kuwindwa na majangili.
“Kwa sasa muda si mrefu tutakuwa tumekamilisha kujenga boma kwa ajili ya faru pale Mkomazi. Hii itawafanya watu wanaokwenda pale waweze kuwaona kwa urahisi faru. Lakini pia tunafikiria kuwa na utaratibu wa watu wanaotaka kuwapa majina yao faru hao. Tutaweka utaratibu na watu watalipia,” alisema Nyamhanga.
Watanzania katika miaka ya karibuni, wamekuwa wakisikia majina mbalimbali waliyopewa faru kama vile Faru John, Faru Fausta na Faru Ndugai anayehusishwa na jina alilotoa Spika wa Bunge, Job Ndugai.
Kwa upande wake, Ofisa Mwandamizi wa Uhifadhi ambaye pia ni Mratibu wa Faru Kitaifa, Philbert Ngozi, alisema licha ya kupewa majina hayo, lakini faru atatambulia pia kwa namba yake ambayo itakuwa ni rahisi kwa askari wa uhifadhi kuwatambua wanapowafuatilia kwa vifaa maalumu walivyofungwa ili kudhibiti ujangili.
Ngozi alieleza kuwa hadi kufikia Machi mwaka huu, Tanzania ilikuwa na faru 190. Wanyama hao wamekuwa wakiongezeka baada ya awali kupungua kwa kasi katika miaka ya 1990 kutokana wimbi kubwa la ujangili.
Faru hao wanajulikana kwa jina la Faru wa Mashariki. Katika miaka ya 1970 Tanzania ilikuwa na wanyama hao 10,000 na ilikuwa nchi ya nne kwa Afrika kwa kuwa na idadi kubwa, lakini walipungua katika miaka ya 1990, kisha mwaka 2018 walikuwa faru 161.
“Lakini habari njema ni kuwa tangu mwaka juzi (2018) hakujatokea kifo chochote cha faru kutokana na ujangili, zaidi ya kifo cha faru fausta aliyekufa mwaka jana kutokana na ugonjwa. Hivyo hii ni habari njema kwa nchi,” alisema Ngozi na kubainisha kuwa kwa Mkomazi, wako faru wa porini na wale wa kutunzwa kwenye bustani ya wanyama.
Septemba mwaka jana, Tanzania ilipokea faru tisa kutoka Afrika Kusini ambao walipelekwa katika Pori la Akiba la Ikorongo linalopatikana wilaya za Serengeti na Bunda mkoani Mara.
Ngozi alibainisha kuwa serikali imeunda Mkakati wa Kuhifadhi Faru unaotekelezwa kuanzia mwaka 2019 hadi 2023, kuhakisha wanyama hao wanaongezeka na wanalindwa ili wasitoweke. Mkakati huo unagharimu Sh bilioni 60.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464