Mkaguzi wa Pamba Wilaya ya Kishapu na Shinyanga, Thomas Tiluhongelwa akishuhudia masanduku ya viuadudu yakipakiwa kwa ajili ya kusambazwa kwa wakulima wa Pamba wilayani Kishapu
Suzy Luhende na Damian Masyenene –Shinyanga
BODI ya Pamba Tanzania imeanza kusambaza viuadudu kwa wakulima wa zao hilo katika wilaya ya Kishapu Mkoani Shinyanga kwa ajili ya kuanza upuliziaji wa dawa kwenye Pamba iliyolimwa mwanzoni.
Zoezi hilo la kukabidhi viuadudu hivyo limefanyika leo Desemba 30, 2020 katika ofisi za bodi hiyo, ambapo jumla ya masanduku 24,305 yenye viuadudu yamekabidhiwa kwa ajili ya wilaya ya Kishapu ili kuanza mapema upuliziaji.
Akizungumza na Shinyanga Press Club Blog ofisini kwake baada ya kukabidhi viwatilifu hivyo, Mkaguzi wa Pamba Wilaya ya Kishapu na Shinyanga, Thomas Tiluhongelwa amesema kuwa matarajio ni kusambaza masanduku 400,000 kwa wakulima wilayani Kishapu kulingana na mwitikio wa kilimo cha Pamba.
Tiluhongelwa amebainisha kuwa katika msimu huu wa kilimo cha Pamba, wilaya hiyo imejiwekea malengo ya kulima ekari 200,000 na mahitaji ya mbegu za zao hilo (zisizo na manyoa) yakiwa ni Kilo 1,000,000, huku wakiwa wamekwishasambaza Kilo 1,300,000, huku Wilaya ya Shinyanga ikijiwekea lengo la kulima ekari 11,317 na mahitaji ya mbegu zisizo na manyoa yakiwa kilo zaidi ya 56,000 na tayari wamepeleka tani 152.6.
Licha ya jitihada hizo za upelekaji wa mbegu, bado wakulima wamekuwa wakilalamikia uhaba wa mbegu, ambapo Tiluhongelwa ameeleza kuwa hali hiyo inasababishwa na mbegu nyingi kuoza katika maeneo ya mbugani kutokana na uwepo wa maji mengi msimu huu wa mvua na wadudu kushambulia mbegu zilizokuwa zimeota.
Pia ameongeza kwa kuelezea kuwa changamoto hiyo imekuwa ikisababishwa na wizi wa mbegu, ambapo baadhi ya viongozi wasio waaminifu wa Vyama vya Msingi vya Wakulima (AMCOS) wamekuwa wakifanya dili na wenye viwanda vya kukamua mafuta ya Pamba na kuwauzia mbegu hizo, jambo ambalo limekuwa likifanywa pia na wakulima.
“Tumeamua kufanya uhakika wa kila mkulima na eneo lake la kilimo, kwa sababu kumekuwa na udanganyifu, mtu anakuwa na ekari tatu Lakini anaomba mbegu za kukidhi ekari 46. Kwahiyo, wakati mwingine kumekuwa na mchezo mchafu baina ya watumishi, AMCOS na wakulima kuuza mbegu,” amesema.
“Changamoto nyingine zinazosumbua ni ukosefu wa uaminifu na usimamizi mzuri wa AMCOS, mvua ambazo hazitabiriki na kuleta usumbufu pamoja na wakulima kuwa wagumu kukata miti ya pamba (masalia) na kusababisha wadudu kuzaliana kila mwaka,” amebainisha.
Katika kuhakikisha wanakabiliana na changamoto mbalimbali na kufikia malengo ya msimu huu wa kilimo cha Pamba, Tiluhongelwa amesema kuwa wanaendelea kutoa mafunzo na elimu kwa wakulima juu ya matumizi sahihi ya viuatilifu na vinyunyizi, pia mafunzo ya kuongeza tija kwa wakulima kupanda mbegu kwa nafasi na AMCOS kusimamia usafi na ubora wa Pamba.
Akizungumzia madeni ya wakulima wa Pamba katika wilaya za Kishapu na Shinyanga, Tiluhongelwa ameweka wazi kuwa tayari wakulima wote wamelipwa madai yao, ambapo kwa halmashauri ya wilaya ya Kishapu jumla ya Sh 363,624,750 zimelipwa, halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Sh 46,302,700 zimelipwa na Sh 24,834,900 zimelipwa katika Manispaa ya Shinyanga.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Pamba Tanzania (TCB), Marco Mtunga katika mahojihano yake na gazeti la Mwananchi Novemba 12, mwaka huu, uzalishaji wa pamba msimu wa kilimo 2020-21 nchini unatarajia kufikia tani 400,000 za pamba mbegu sawa na robota za pamba nyuzii zaidi ya 700,000.
Msimu wa pamba ulitarajiwa kuanza Novemba 15, mwaka huu kwa mujibu wa kalenda ya pamba kwa Kanda ya Magharibi inayojumuisha mikoa 12 inayozalisha takribani asilimia 99 ya pamba yote nchini.
Mkaguzi wa Pamba Wilaya ya Kishapu na Shinyanga, Thomas Tiluhongelwa akizungumza na waandishi wa habari hii (hawapo pichani) ofisini kwake
Mkaguzi wa Pamba Wilaya ya Kishapu na Shinyanga, Thomas Tiluhongelwa akionyesha sehemu ya dawa masanduku 24,305 yaliyokuwa yakipakiwa kwenye roli kwa ajili ya kuyasambaza kwa wakulima wilayani Kishapu
Sehemu ya shehena ya dawa za viuadudu vya Pamba ikiwa imehifadhiwa katika ofisi za Bodi ya Pamba mkoa wa Shinyanga
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464