UTUPAJI TAKA HOVYO DAMPO LA BUSOKA WATAJWA KUHATARISHA AFYA ZA WANANCHI, MKURUGENZI AELEZA MIKAKATI

 Muonekano wa dampo la Busoka lililopo mjini Kahama, ambapo taka zimekuwa zikitupwa hovyo jirani na makazi ya watu kutokana na miundombinu ya kuingia katika dampo hilo kuharibika.

Na Salvatory Ntandu -Kahama
Wakazi wa Kata ya Busoka halmashauri ya Mji Kahama mkoani Shinyanga wamelalamikia utupaji holela wa taka katika Dampo la Busoka lililopo karibu na makazi yao, hali ambayo inaweza kukaribisha magonjwa ya mlipuko kutokana na baadhi ya magari yanayokwenda kutupa taka kutozifikisha katika eneo hilo.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti na Shinyanga Press Club Blog, baadhi ya wakazi hao akiwemo Ladislaus Msomi Mkazi wa Busoka amesema kuwa magari yanayokusanya taka yamekuwa hayazifikishi taka hizo katika eneo lililotengwa na badala yake wamekuwa wakizimwaga karibu na makazi yao hali ambayo inaweza kusababisha kutokea kwa magonjwa ya mlipuko.

“Dampo hili linahatarisha usalama wa afya za wakazi wa Busoka kutokana na kutokuwa na usimamizi mzuri wa utupaji wa taka,haiwezekani taka zimwagwe pembezoni mwabarabara ambayo inatumiwa na wakazi wengi,tunaiomba halmashauri iwadhibiti madereva wa magari hayo ambao hawazingatii sheria,”amesema.

Naye Magasha Paulo ambaye ni mkazi wa kata hiyo, amesema kuwa endapo hatua za haraka zisipochukuliwa Dampo hilo linaweza kusababisha madhara kwa wakazi hao kutokana na baadhi ya wananchi kwenda katika eneo hilo kuokota baadhi ya taka ambazo wanaziona ni fursa jambo ambalo sio zuri kwa afya zao.

“Kuna athari mbalimbali za kiafya kama Dampo hili lisipokuwa na ulinzi ili kudhibiti watu wanaoingiza mifugo kwaajili ya malisho sambamba na kuokota taka kama vile chupa za maji,tunaiomba serikali ijenge uzio ili kudhibiti wimbi la wakazi wa kata hii wanaoingia katika eneo hilo,”ameeleza.

Kwa upande wake, Elizabeth Bisandi mkazi wa Manzese amesema kuwa serikali inapaswa kuongeza ulinzi katika Dampo hilo hususani uteketezaji wa taka sumu kama vile vipodozi vyenye sumu ili visilete madhara kwa wananchi wanaokwenda katika eneo hilo kuokota bidhaa zilizokwisha muda wake na kwenda kuziuza mitaani bila ya kujua athari zake kwa watumiaji wengine.

“Mwaka jana kunawatu waliokota vipodozi na kuviuza mitaani na badala yake vilianza kuleta athari kwani kila aliyetumia mafuta hayo alichubuka ngozi na kuwa mweupe hali ambavyo isipodhibitiwa inaweza kusababisha madhara kwa wakazi wa kata hiyo,”amebainisha.

Akijibu malalamiko ya wakazi hao, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Mji Kahama, Anderson Msumba alikiri kuwepo kwa kero hizo ambazo zilichangiwa na kuharibika kwa barabara iliyokuwa inatumiwa na magari kuingia katika lango kuu la dampo hilo na kusababisha kumwaga taka hizo pembezoni mwa barabara.

“Tumeshapeleka mkandarasi katika eneo hili na anaendelea na zoezi la ukusanyaji wa taka hizo,tunaendelea kuchimba mashimo makubwa kwa ajili ya kuzifukia na mpango wetu ni kulijenga dampo hili liwe la kisasa sambamba na kujenga uzio ili kuzuia watu kuingia katika eneo hilo,”amefafanua.

Ameongeza kwa kueleza kuwa eneo hilo litajengwa kwa viwango vya kimataifa ya uhifadhi na uteketezaji wa taka kwani sasa wanasubiria mkopo wa ufadhili kutoka benki ya dunia ambao utakuwa suluhisho la wakazi wa eneo hilo kulalamikia utupaji holela wa taka karibu na Makazi yao na kutoa rai wa wananchi kuingiza mifugo, na kutokwenda kuokota chupa katika eneo hilo kwaajili ya kulinda afya zao.

 Mlundikano wa taka katika dampo hilo na kusababisha zizagae hovyo katika makazi ya watu na kuzua hofu ya magonjwa ya mlipuko ikiwemo Kipindupindu




 Hali ilivyo katika dampo la Busoka




Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464