WAFANYABIASHARA WA PUNDA NCHINI WALIOKWAMA SHINYANGA KWA SIKU 40 WAMLILIA RAIS MAGUFULI

Sehemu ya Punda 2,000 walioletwa na wafanyabaishara kutoka maeneo mbalimbali nchini ili kukiuzia kiwanda cha machinjio ya nyama ya Punda cha Fanghua cha mjini Shinyanga, lakini wameshindwa kununuliwa baada ya kiwanda hicho kusistisha uzalishaji.

Na Damian Masyenene, Shinyanga 
WAFANYABIASHARA wa Punda nchini wanaokiuzia Kiwanda cha machinjio ya bidhaa hiyo cha Fanghua kilichopo mjini Shinyanga, wamejikuta katika hali ya sintofahamu na changamoto kubwa wakikwama mjini humo kwa siku zaidi ya 40 baada ya kufikisha mifugo yao kiwandani hapo na kushindwa kupokelewa kwa kile kinachoelezwa kuwa kiwanda kimesitisha uzalishaji kwa muda usiojulikana. 

Kiwanda cha Fanghua ndicho kiwanda pekee cha machinjio ya Punda nchini, ambapo Wafanyabaishara hao kutoka mikoa mbalimbali nchini ikiwemo Mbeya, Dodoma na Manyara hununua mifugo hiyo kwenye minada na kukiuzia kiwanda hicho kulingana na uzito wa kila Punda, ikitajwa kuwa kila kilo moja ni Sh 2,000. 

Wafanyabiashara hao ambao wako kwenye vikundi zaidi ya 100 walifika mkoani Shinyanga na Punda zaidi ya 2,000 wakiwaleta kiwandani hapo tangu Oktoba 24, mwaka huu, lakini walishindwa kuwauza baada ya uongozi wa kiwanda kuwaambia kuwa hawachukui tena bidhaa hiyo, hali ambayo iliwaweka katika wakati mgumu wakihaha huku na kule kupata muafaka na kujua hatma yao. 

Wakizungumza na Shinyanga Press Club Blog nje kidogo ya mji wa Shinyanga walikohifadhi Punda hao, Wafanyabiashara hao wameiomba Serikali hususan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli kuingilia kati na kuwanusuru na mateso wanayopitia kwa zaidi ya siku 40. 

Mmoja wa Wafanyabiashara hao, Selina Amon kutoka mkoani Manyara amesema kuwa baada ya kiwanda hicho kufungwa, wanyama hao wamekosa malisho na kupelekea baadhi ya Punda kufa kwa njaa kali, magonjwa na kushambuliwa na wanyama, huku akieleza kuwa baada ya kuuona uongozi wa wilaya ya Shinyanga walijibiwa kuwa jambo hilo liko juu ya uwezo wao na hawana msaada wowote. 

“Tuna Mikopo, tunaishi kwa tabu watoto shuleni wamerudishwa na familia zinatutegemea…Tulinunua punda tukaleta kiwanda kimesema hawanunui tena sasa tunashindwa tufanyeje tuko ugenini hapa kwa siku 40 sasa, kila siku tunababaishwa mara subirini kidogo,” amesema. 

Naye Yohana Lucas ambaye ni mfanyabiashara kutoka Manyoni mkoani Singida, ameeleza kuwa baada ya kukosa msaada ngazi ya mkoa wa Shinyanga waliamua kwenda Dodoma wizarani ambako pia hawakupata maelezo yanayojitosheleza, huku akibainisha kuwa wamekosa sehemu ya kuishi na malisho ya Punda hao zaidi ya 2,000 ambapo wamekuwa wakifukuzwa kwenye mashamba ya watu wanakoenda kujaribu kuchunga mifugo hiyo. 

“Tumekuja hapa (Shinyanga) kufanya biashara ya Punda lakini tumefika hapa na kuambiwa tusubiri, tumekata mitaji hatuna la kufanya tunaishi kwa tabu. Tunaomba viongozi watusaidie, tunamuomba Rais wetu atusaidie tuendelee kufanya biashara hii ambayo ilikuwa mkombozi kwetu,” ameeleza. 

Akizungumza kwa njia ya simu kueleza sababu za kiwanda kusitisha kupokea bidhaa hiyo, Meneja wa Kiwanda hicho Alice Mingyang Yan amesema kuwa wamesitisha kupokea bidhaa hiyo tangu Oktoba 24, 2020 na kwamba usumbufu ulianza tangu Julai, mwaka huu kwa kile wanachoeleza kuwa ni mamlaka za Serikali kutojali hoja zao wanazoziwasilisha. 

Alice amebainisha kuwa kwa sasa anaendelea kulifuatilia suala hilo kwa mamlaka za serikali kupata muafaka ili warejeshe shughuli za uzalishaji, huku akiwataka wafanyabiashara hao wa Punda kupeleka kilio chao kwa serikali. 

Akitolea ufafanuzi wa sakata la Wafanyabaishara hao, Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko amefafanua kuwa tatizo hilo uongozi wa wilaya na mkoa wa Shinyanga wanalifahamu na kwamba uongozi wa kiwanda cha Fanghua tayari umechukua hatua za kulifuatilia ngazi za juu. 

DC Mboneko amesisitiza kuwa jambo hilo mwenye kiwanda alitakiwa awajulishe wafanyabiashara mapema ili wasipate changamoto hiyo, huku akibainisha kuwa suala lao Wizara ya Mifugo na Uvuvi pamoja na EPZA wanalishughulikia na matumaini yake ni kwamba litapata ufumbuzi mapema. 

“Nawaomba sana kwa sasa kiwanda kimesistisha shughuli kwahiyo wasilete tena punda kuendelea kupata hasara. Taarifa za punda kufa sidhani kama ni la kweli, kwani punda hata watano wakifariki tu hakutakalika, na hatujapokea taarifa hizo wala kushuhudia sehemu waliyozikwa, shughuli zilisistishwa toka mwezi wa tisa kwahiyo wafanyabishara wasubiri mpaka jambo hili litatulike shughuli zianze ndiyo waendelee kuleta bidhaa hiyo,” amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko

Mmoja wa Wafanyabiashara hao, Selina Amon kutoka mkoani Manyara akiwa na wenzake wakizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani)
Wafanyabiashara hao wakiwachunga Punda waliowaleta kuwauza

Punda hao wakiendelea kuchungwa nje kidogo ya mji wa Shinyanga
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464