WANAFUNZI 26,382 SHINYANGA WAPANGIWA SHULE KIDATO CHA KWANZA, 234 WABAKI, 108 WAPELEKWA BWENI.....RAS AZITAKA HALMASHAURI KUKAMILISHA MIUNDOMBINU JAN 28

Katibu Tawala mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela akitangaza matokeo ya ufaulu wa darasa la saba na wanafunzi wa waliochaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mkoani humo, leo katika kikao kilichowakutanisha wadau mbalimbali wakiwemo wakuu wa wilaya, makatibu tawala wa wilaya, maofisa elimu na wakuu wa shule

Na Damian Masyenene, Shinyanga 
JUMLA ya wanafunzi 26,382 waliofaulu mtihani wa taifa wa kumaliza darasa la saba mwaka huu mkoa wa Shinyanga, wamepangiwa wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza na kupangiwa shule, huku 234 wakiwemo wasichana 233 na mvulana mmoja wakibaki (kukosa nafasi) hadi awamu nyingine. 

Kati ya wanafunzi hao waliopangiwa shule, 108 wamechaguliwa kwenda shule za bweni wakiwemo wasichana 66 na wavulana 42, huku wanafunzi 26,148 wakichaguliwa kwenda shule za kutwa. 

Akitangaza matokeo hayo , Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga (RAS), Albert Msovela, amesema wanafunzi 26,382 wamefaulu na kufanya ufaulu kwa mwaka huu kuongezeka kwa asilimia 1.14 na mkoa huo kushika nafasi ya 17 kitaifa kati ya mikoa 26 kwa ufaulu wa asilimia 78.9 ikilinganishwa na wanafunzi 23,634 sawa na asilimia 77.76 wa mwaka jana. 

Ambapo, jumla ya shule 603 za mkoa huo zilizoshiriki mtihani wa darasa la saba na wanafunzi 33,767 walisajiliwa kufanya mtihani huo wavulana wakiwa 15714 na wasichana 18053, huku akibainisha kuwa wanafunzi waliokosa nafasi za kupangiwa shule za kidato cha kwanza watapangiwa kadri ujenzi wa madarasa utakapokamilika. 

“Tunaamini wote watakwenda shule kadri tutakapokamilisha miundombinu, kama ambavyo serikali ilielekeza ifikapo Februari 28, mwakani miundombinu ya madarasa iwe imekamilika, na sisi kama mkoa tumejipangia ifikapo Januari 28, mwakani tuwe tumekamilisha ujenzi wa madarasa na watoto wote waende shule,” amesisitiza. 

“Tuweke mikakati thabiti itakayowezesha wanafunzi wote waliotangazwa wanaripoti shuleni na kumaliza kidato cha nne. Wale wote watakaopelekea wanafunzi kukatiza masomo yao, wachukuliwe hatua, kama wazazi na walimu tuweze kufuatilia mienendo yao kuhakikisha ndoto zao zinatimia na kuhitimu kidato cha nne,” ameeleza. 

Amefafanua kuwa katika matokeo hayo, Manispaa ya Shinyanga imekuwa ya kwanza kimkoa huku ikishika nafasi ya 17 kitaifa, Halmashauri ya Kahama Mji ni ya pili na ya 84 kitaifa, Msalala ya tatu na ya 138 kitaifa, Kishapu ya nne na ya 140 kitaifa, Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ya tano na ya 151 kitaifa, huku Ushetu ikishika mkia ngazi ya mkoa kwa kushika nafasi ya sita na ya 169 kitaifa. 

Kwa upande wake, Afisa Elimu Mkoa Shinyanga, Mohamed Kahundi amesema kuwa mkoa huo unazo shule 638 za msingi lakini 603 ndizo zilizofanya mtihani huo zikiwemo 580 za serikali na 58 za binafsi, ambapo jumla ya wanafunzi 42,867 waliandikishwa darasa la kwanza mwaka 2014 lakini ni wanafunzi 33,367 pekee waliosajiliwa kufanya mtihani wa darasa la saba mwaka 2020, huku zaidi ya wanafunzi 9,000 sawa na asilimia 21.2 wakipotelea njiani kwa kukatisha masomo kwa sababu mbalimbali ikiwemo utoro na mimba. 

Kahundi amewataka viongozi ngazi zote kuendelea kuhamasisha wanafunzi kuipenda elimu ili kupunguza ili anguko, kwani linasababisha wanafunzi kuhitimu wachache na kusababisha mkoa huo kukosa nafasi nyingi za bweni na kupangwa shule za kitaifa. 

“Bado tuna changamoto kubwa hasa elimu ya msingi, tunao upungufu vyumba vya madarasa 5881, upungufu walimu 4830, upungufu wa matundu ya vyoo 14,376, upungufu wa madawati 16,672. Halmashauri mtenge shule walau mbili maalum mfano shule ya sekondari ya wasichana Kishapu ambayo ni Maalum kwa ajili ya wasichana ili kuwanusuru na changamoto ya mimba, kubakwa na ndoa za utotoni, na mwaka huu katika uchaguzi huu wa wanafunzi wamepata wanafunzi 80,” amesema. 

Wakitoa mapendekezo na kutoa ushauri namna ya kuboresha elimu na kumaliza changamoto, mmoja ya wadau waliohudhuria kikao hicho, Katibu Tawala Wilaya ya Kahama, Timoth Ndanya alishauri uandaliwe utaratibu wa kisheria, kesi zinapotokea za kukatisha masomo ya wanafunzi hususan wa kike ziwe na ukomo wa kuendeshwa ili zimalizike kwa wakati na hatma ya mwanafunzi ijulikane mapema. 

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba akijibu hoja hiyo ameeleza kuwa katika kikao cha wadau wa kupinga ukatili wa kijinsia mkoa wa Shinyanga kilichofanyika Desemba 15, mwaka huu, kiliazimia kwamba kesi zote zinazofika mahakamani siku hiyo hiyo shahidi awepo na zianze kushughulikiwa (kusikilizwa) kabla ya pande zote hazijarudi nyumbani na kuanza kumalizana/ kuelewana. 

Hata hivyo, Mkuu wa shule ya Sekondari Busangi iliyopo Msalala, Martin Ndola akizungumzia changamoto ya uwepo wa idadi ya wanafunzi wanaoshindwa kumaliza darasa la saba, amesema kuwa tatizo hilo kwa kiasi Fulani linachangiwa na wazazi ambao huwahimiza Watoto kusema kwamba hawana akili na kuwaachisha masomo na wanapofuatilia kwenye vyombo vya sheria hatua hazichukuliwi, hivyo akashauri mkoa kuja na hatua ambayo itawabana na kuwawajibisha wazazi katika hilo. 

Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba amesema kuwa kwa sasa idadi kubwa ya wanafunzi wanaokatisha masomo ni wavulana akitolea mfano wa shule moja wilayani humo ambayo darasani kulikuwa na mwanafunzi mmoja tu wa kiume, huku akishauri kuwa msisitizo umewekwa sana kwa wanafunzi wa kike na kuwasahau wavulana, hivyo akapendekeza nao watazamwe na kurejeshwa shule na kuwasihi wadau wote kulichukulia kwa uzito mkubwa suala la ukamilishaji wa miundombinu ya shule. 

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha amewatupia lawama wazazi ambao licha ya serikali kujenga mabweni kwa ajili ya wanafunzi lakini hawajahamasika kuwapeleka na badala yake kuwapangisha kwenye vyumba mitaani katika mazingira hatarishi ambayo hukatiza ndoto za wanafunzi. 

“Kwenye hili la wanafunzi kutokukamilisha masomo, nadhani pia changamoto imekuwa kwenye utekelezaji wa majukumu watu wanasubiri mpaka Mkuu wa wilaya afanye ziara ndiyo wanatoa taarifa. Pia mivutano baina ya maafisa elimu ngazi ya Kata na wakuu wa shule, kila mmoja anataka kuonyesha nani mkubwa! Kwahiyo watu watimize wajibu wao wawafuatilie na kutoa taarifa mapema Wasitegeane,” ameeleza.

Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela akisisitiza jambo wakati akizungumza na baadhi ya wakuu wa wilaya, makatibu tawala wa wilaya, maofisa elimu na wakuu wa shule wakati wa hafla ya utangazaji matokeo na uchaguzi wa wanafunzi watakaojiunga na kidato cha kwanza, leo katika ukumbi wa mkuu wa mkoa wa Shinyanga
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela akitangaza matokeo hayo mbele ya wadau wa elimu mkoa wa Shinyanga
Afisa Elimu Mkoa wa Shinyanga, Mohamed Kahundi akitoa taarifa ya elimu na namna uchaguzi wa wanafunzi hao ulivyofanyika

Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha akichangia hoja na kutoa ushauri juu ya changamoto mbalimbali za elimu mkoani Shinyanga
Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba akizungumza katika kikao hicho
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba akichangia hoja namna wanavyoshiriki kukomesha vitendo vya kukatisha masomo wanafunzi
Mkuu wa Takukuru Mkoa wa Shinyanga, Hussein Mussa akizungumza katika kikao hicho
Mstahiki Meya wa Manispaa ya Shinyanga, David Nkulila (kushoto) na Mkurugenzi wa manispaa hiyo, Geofrey Mwangulumbi wakifuatilia utangazaji wa matokeo
Mkuu wa wilaya ya Kahama, Anamringi Macha (kushoto) na Mkuu wa wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba wakifuatilia kikao hicho
washiriki wakifuatilia kikao
Washiriki wa kikao hicho wakifuatilia kwa makini wakati wa kutangaza wanafunzi waliochaguliwa
Wadau wa elimu wakifuatilia zoezi hilo
Sehemu ya viongozi wa Manispaa ya Shinyanga wakifatilia zoezi hilo
Kikao kikiendelea
Washiriki wakifuatilia zoezi hilo
Mkuu wa Wilaya ya Kahama, Anamringi Macha akisoma makabrasha ya taarifa za uchaguzi huo wa wanafunzi
sehemu ya maofisa wa tehama katika idara ya elimu mkoa wa Shinyanga
Viongozi wa meza kuu katika kikao hicho
maofisa wa sekretarieti ya kikao hicho
washiriki wa kikao hicho wakifuatilia yanayojiri
Wadau wa elimu wakiendelea kufuatilia zoezi la utangazaji wa matokeo na uchaguzi wa wanafunzi
Washiriki wakiendelea kufuatilia zoezi hilo


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464