Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi Mkoa wa Shinyanga, Dk. Peter Mlacha akitoa taarifa ya hali ya maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi kwa mkoa huo, wakati wa maadhimisho ya siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika jana Desemba Mosi halmashauri ya Ushetu.
Na Josephine Charles - Ushetu
Wananchi mkoani Shinyanga hususani wanaume wameshauriwa kujitokeza kwa wingi katika zoezi la upimaji Virusi Vya Ukimwi (VVU) kila mara pamoja na kufanyiwa tohara kinga ili kujua mienendo ya afya katika miili yao.
Ushauri huo umetolewa na Katibu Tawala Wilaya ya Kahama, Timoth Ndanya ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI Duniani ambayo kwa Mkoa wa Shinyanga yalifanyika kwenye viwanja vya kijiji cha Mapamba katika Halmashauri ya Wilaya ya Ushetu wilayani Kahama.
Hayo yamejiri baada ya kugundulika kuwa wanaojitokeza kwa wingi katika zoezi la upimaji Virusi vya Ukimwi ni wanawake, hivyo wanaume wametakiwa kuambatana na wenza wao kwenda kupima na kuhudhuria clinic pindi wanapogundulika kuwa na VVU.
Katibu Tawala huyo ameihimiza jamii kuachana na mila potofu ambazo ni moja ya vyanzo vya maambukizi ya VVU, pia amewashauri watoto wa kike wakatae ulaghai unaofanywa na baadhi ya wanaume hususani wababa ili waweze kutimiza ndoto zao pasipokupata maambukizi ya VVU.
Kwa Upande wake Mratibu wa Kudhibiti Ukimwi Mkoa wa Shinyanga, Dk. Peter Mllacha amezungumzia changamoto ya idadi ndogo ya vituo vya Kutolea huduma za tiba na matunzo ambapo amesema kwa sasa vituo vilivyopo ni 85 sawa na asilimia 34.5 huku wakiwa na upungufu wa asilimia 68.3 wa Vituo hivyo.
Aidha Dk. Mlacha ameitaja takwimu ya mkoa wa Shinyanga kuanzia mwezi Jan-Nov 2020 kuwa na Idadi ya watu waliopimwa kuwa ni 170,168, waliokutwa na VVU ni 8,452 sawa na asilimia 5.9 na waliounganishwa na Vituo vya Tiba na Matunzo ni 8320, ambapo Idadi hiyo imepelekea Mkoa wa Shinyanga kushika nafasi ya 6 kitaifa ktk maambukizi ya mapya ya VVU ambayo ni sawa na asilimia 7.
Ambapo kiwango hicho kimeshuka kutoka asilimia 7.4 hadi 5.9 kwa mkoa wa Shinyanga.
Takwimu ya Halmashauri ya wilaya ya Ushetu kuanzia mwezi Jan-Nov 2020,waliopimwa ni zaidi ya watu 32,000 waliokutwa na VVU ni 1,200 sawa na asilimia 3.8.
Hata hivyo Mbunge wa Jimbo la Ushetu, Mhe. Elias Kwandikwa ambaye naye alihudhuria maadhimisho hayo, ameishukuru serikali ya Tanzania kwa Miradi mbalimbali ambayo inaendelea kutolewa kwa wananchi katika Kupambana na VVU pamoja na kuwepo kwa Vituo vya Afya ambavyo vinazidi kuboreshwa miundo mbinu yake.
Kwa Upande wao wananchi maonesho hayo wamesema kupitia maadhimisho hayo wamejifunza mengi ikiwemo kupata Elimu ya kuacha kufanya ngono zembe sambasamba na kutumia kinga ili kujikinga na VVU.
Maadhimisho haya yameenda sambasamba na uchangishaji wa Kituo cha Tiba na Matunzo kwa waishio na VVU cha Kijiji cha Mapamba halmshauri ya wilaya ya Ushetu ambapo kiasi cha zaidi ya Sh. Milioni 6 zilichangwa.
Maadhimisho ya Ukimwi Duniani ambayo hufanyika Decemba Mosi kila Mwaka kwa hapa Tanzania Kitaifa yamefanyika Mkoani Kilimanjaro na Mkoani Shinyanga yamefanyika wilaya ya Ushetu yakiongozwa na Kauli Mbiu isemayo "MSHIKAMANO WA KIMATAIFA TUWAJIBIKE KWA PAMOJA"
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464