Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo (aliyesimama)
Na Angela Msimbira, NJOMBE
Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Selemani Jafo amewaagiza wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini kujitathmini juu ya ukusanyaji wa mapato na usahihi wa utumiaji wa rasilimali fedha zitokanazo na mapato hayo
Waziri Jafo ametoa kauli hiyo leo wakati akizungumza na watumishi wa Halmashauri ya Mji wa Njombe na kusema kuwa lazima mapato hayo yanayokusanywa yatumike kwa usahihi katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo
“Nataka Halmashauri zote zikusanye mapato, awali ukusanyaji wa mapato ulikuwa hafukii asilimia 72, katika kipindi cha miaka mitano chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli Halmashauri zote nchini zimeweza kukusanya mapato kwa asilimia 94” amesema Waziri Jafo
Waziri Jafo amesisitiza kuwa Serikali ilijiwekea mkakati kuwa ifikapo Disemba 2020 halmashauri zote ziwe zimekusanya mapato si chini ya asilimia 50 , suala la ukusanyaji wa mapato ni la muhimu katika Halmashauri zote nchini.
“Nitakapotoa ripoti ya miezi sita ya hali ya ukusanyaji wa mapato katika Halmashauri zote nchini mnamo tarehe 15/1/2021 nataka halmashauri zote ziwe zimefikia si chini ya asilimia 50 ” amesisitiza Waziri Jafo
Amesema kuwa Halmashauri zote ambazo hazitafikia asilimi 50 ya ukusanyaji wa mapato Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo lazima ajitathmini kama anafaa kuendelea kushika nafasi au hatoshi na atolewe ili awekwe mwingine ambaye atakayeweza kukusanya mapato
Waziri Jafo amesema Serikali haitashughulika na Wakurugenzi pekee bali itawachukulia hatua waweka hazina na maafisa mipango wa Halmashauri ambao wameshindwa kukusanya mapato.
Aidha Waziri Jafo ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Njombe ambapo walijiwekea malengo ya kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 2.3 na hadi kufikia tarehe 21/12/2020 wameweza kukusanya kiasi cha shilingi 1.7 sawa na asilinia 72 wakati Halmashauri ya mwisho kwa ukusanyaji wa mapato ni Halmashauri ya Wilaya ya Makete iliyokusanya kiasi cha shilingi milioni 599 sawa na asilimia 25
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464