Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Blasius Chatanda
MKAZI wa Kitongoji cha Kwesalaka wilayani Kilindi, mkoani Tanga, Seif Hatibu, anatuhumiwa kumuua kaka yake Mahimbo Hatibu kwa madai ya ugomvi wa deni la Sh. 13,000.
Tukio hilo lilitokea juzi saa 1:30 usiku na inadaiwa kuwa Mahimbo alikwenda kwa Seif ambaye ni mdogo wake, kumdai kiasi hicho cha fedha.
Imedaiwa katika kudaiana kulitokea mabishano baina ya wawili hao na wakati Mahimbo akiendelea na shughuli zake, Seif alimvamia na kumpiga na fimbo sehemu ya kichwa na kuanguka.
Majirani walioshuhudia tukio hilo, walipiga kelele kuomba msaada na watu walifika kutoa huduma ya kwanza kabla ya kumpeleka hospitalini.
“Tulisikia kelele ya kuomba msaada, tulipofika Mahimbo alikuwa amelala chini akivuja damu sehemu ya kichwani, tukaanza kumsaidia kupunguza kasi ya uvujaji wa damu na kumkimbiza hospitalini,” alieleza mkazi mmoja ambaye hakutaka kuandikwa jina gazetini kwa madai kuwa siyo msemaji.
Nipashe lilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Blasius Chatanda, kuzungumzia tukio hilo na kukiri kulipata na kwamba anasubiri taarifa kamili kutoka kwa maofisa wake ambao wameenda eneo la tukio.
Kamanda Chatanda alisema:
“Ngoja tunaendelea na taarifa kwa muda huu na mimi nitazungumza nikishapata taarifa kamili.”