Shughuli za utengenezaji Dhahabu zikiendelea
Na Mwandishi Wetu
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita, Daniel Mapunda amesema kuwa katika kipindi cha nusu mwaka wa fedha 2020-2021 ofisi yake ilifanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 120 ikiwa ni asilimia 60 ya lengo la makusanyo ya mwaka husika ambalo lilikuwa ni kukusanya shilingi bilioni 200.
Mapunda ameyasema hayo jana kwenye mahojiano maalum na waandaaji wa kipindi cha Tunatekeleza kinachorushwa na Shirika la Utangazaji la Taifa (TBC) katika eneo la machimbo ya Nyarugusu Wilayani Geita Mkoani Geita.
Alisema kuwa kasi ya ukusanyaji wa maduhuli imechangiwa na maboresho ya Sheria ya Madini, uimarishaji wa usimamizi kwenye miradi ya uchenjuaji wa madini inayofanywa na wachimbaji wadogo wa madini pamoja na masoko ya madini na vituo vya ununuzi wa madini vilivyoanzishwa mkoani Geita.
Akielezea mwenendo wa makusanyo ya maduhuli kwa miaka ya nyuma, Mapunda alisema kuwa katika mwaka wa fedha 2018 -2019 ofisi yake ilipangiwa lengo la kukusanya shilingi bilioni 85 na kufanikiwa kukusanya shilingi bilioni 128 na mwaka 2019-2020 ofisi ilipangia lengo la kukusanya shilingi bilioni 156 na kufanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 206.
"Kama Ofisi ya Madini Geita katika mwaka wa fedha 2020-2021 tumeweka lengo la kukusanya zaidi ya shilingi bilioni 200" alisema Mapunda.
Aliendelea kufafanua kuwa katika kuhakikisha lengo linafikiwa na kuvukwa ofisi imeweka mikakati mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuendelea kusimamia kwa karibu miradi ya uchejuaji wa madini inayomilikiwa na wachimbaji wadogo (mialo),soko la madini na vituo vya ununuzi wa madini huku ikiimarisha udhibiti wa utoroshaji wa madini kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama.
Katika hatua nyingine akielezea mafanikio ya Soko la Dhahabu Geita, Mapunda alisema kuwa kabla ya kuanzishwa kwa soko hilo, Ofisi ya Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita ilikuwa ikikusanya chini ya shilingi bilioni moja kwa mwezi na kuendelea kufafanua kuwa mara baada ya kuanzishwa kwa Soko la Madini Geita, Ofisi yake imekuwa ikikusanya wastani wa shilingi bilioni nne kwa mwezi kutoka kwa wachimbaji wadogo wa madini.
Afisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Geita, Daniel Mapunda
Shughuli za kuandaa taarifa za maduhuli zikiendelea
Mmoja wa wachimbaji akiendelea kusafisha Dhahabu
Wachimbaji wakitoka shimoni kwa ajili ya uchimbaji wa Dhahabu
Usafishaji wa Dhahabu ukiendelea
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464