Wachezaji wa timu ya Yanga wakishangilia baada ya kufuzu hatua ya fainali kwa kuwatoa Azam FC kwa mikwaju ya Penalti 5 kwa 4 leo katika uwanja wa Aman Zanzibar. (Picha na Yanga SC)
Na Damian Masyenene
SASA ni rasmi! Fainali ya michuano ya Kombe la Mapinduzi Zanzibar mwaka 2021 itawakutanisha miamba wawili wa soka nchini, Watani wa Jadi Yanga na Simba wenye maskani yao Kariakoo Jijini Dar es Salaam.
Fainali hiyo itapigwa Januari 13, mwaka huu katika Uwanja wa Amani Zanzibar, huku Simba wakiwa na Kumbukumbu ya kucheza fainali msimu uliopita dhidi ya Mtibwa Sugar na kupoteza kwa bao 1 kwa 0.
Yanga ndiyo walikuwa wa kwanza kufuzu fainali hiyo mapema leo mchana baada ya kuichapa Azam FC kwa mikwaju ya penalti 5 kwa 4 kwenye mchezo wa nusu fainali baada ya kumalizika kwa sare ya bao 1 kwa 1 katika dakika 90 za kawaida.
Nayo, Simba SC imetinga hatua ya fainali usiku huu baada ya kuifunga Namungo FC mabao 2 kwa 1 katika mchezo wa nusu fainali ya pili iliyopigwa kwenye uwanja wa Aman Zanzibar.
Mabao ya Simba SC katika mchezo huo yamefungwa na Meddie Kagere na Miraji Athuman 'Sheva' ambaye anafikisha goli la nne na kumfanya kuwa kinara wa ufungaji katika michuano hiyo hadi sasa, huku bao pekee la Namungo FC likiwekwa nyavuni na Steven Seyi katika dakika za lala salama.
Mshambuliaji wa Simba SC, Meddie Kagere na wenzake wakishangilia baada ya kuipatia timu yake bao la kuongoza dhidi ya Namungo FC (Picha na Simba SC)
Mshambuliaji wa Simba, Miraji Athuman akiifungia timu yake bao la pili katika mchezo wa nusu fainali dhidi ya Namungo FC (Picha na Simba SC)
Wachezaji wa Yanga wakijipongeza baada ya kufuzu hatua ya fainali ya michuano ya kombe la Mapinduzi
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464