Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez na Kocha Mkuu mpya Didier Gomes Da Rosa wakionyesha mkataba baada ya kusaini (Picha na Simba SC)
Na Damian Masyenene
BAADA ya kimya cha muda mrefu na usiri mkubwa, hatimaye Wekundu wa Msimbazi Simba SC wamemtambulisha rasmi Kocha wao Mkuu atakayekinoa kikosi hicho kinachokabiliwa na mashindano mbalimbali makubwa ikiwemo kuutetea ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara.
Kocha huyo mpya wa Simba atakayerithi mikoba ya Sven Vandenbroeck ni Didier Gomes Da Rosa raia wa Ufaransa.
Wakimtambulisha leo mbele ya waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mabingwa hao watetezi wa Tanzania wamesema
"Ni Mwamba hasa wa soka la Afrika akiwa na uzoefu mkubwa wa mashindano makubwa katika bara hili, huku akiwa ameshinda mataji kadha wa kadha.
"Mwalimu huyu ana leseni A ya Uefa inayomfanya awe kocha wa daraja la juu duniani. Karibu Simba Kocha Didier na utapata ushirikiano kutoka kwa klabu na Wanasimba wote kwa ujumla. #NguvuMoja,"
Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez akimkabadhi jezi ya mabingwa wa nchi Kocha Mkuu mpya Didier Gomes Da Rosa
Mtendaji Mkuu, Barbara Gonzalez na Kocha Mkuu mpya Didier Gomes Da Rosa wakisaini mkataba mbele ya waandishi wa habari
Akizungumza mara baada ya kutambulishwa, kocha huyo mpya amesema “Nina furaha sana kuwa hapa na tuna nafasi ya kufanya mengi pamoja mbeleni. Timu niliyoondoka niliamua mwenyewe. Nataka kuwepo Simba kwa muda mrefu.”- Kocha Mkuu mpya, Didier Gomes Da Rosa
Katika hatua nyingine, jana Klabu hiyo ilimtambulisha kocha wao mpya wa makipa kutoka nchini Brazil, Milton Nienov, ambaye amewahi kuwa kocha wa makipa katika klabu za Polokwane City, Lamontville Golden Arrows FC, Super Eagles FC, Free State Stars FC za Afrika Kusini na Club de Regatas Vasco da Gama, Sport Club Recifie na Figueirense FC za Brazil.
Picha zote na Simba SC Tanzania
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464