Kikosi cha Yanga kilichotwaa ubingwa wa Kombe la Mapainduzi leo visiwani Zanzibar
Na Damian Masyenene
HATIMAYE! Timu ya Yanga SC ya Jijini Dar es Salaam ndiyo mabingwa wapya wa Kombe la Mapinduzi Zanzibar Mwaka 2021, ukiwa ni ubingwa wao wa pili katika historia ya michuano hiyo.
Wananchi Yanga wametwaa ubingwa huo baada ya kuibuka wababe wa 'derby' ya Kariakoo, wakiwanyuka watani wao wa jadi Simba SC waliokuwa wapinzani wao wkenye mchezo huo wa fainali kwa mikwaju 4-3 katika mchezo huo uliofanyika leo Januari 13 kwenye dimba la Aman visiwani Zanzibar.
Licha ya majaribio ya mara kwa mara kutoka kwa timu zote kujaribu kutafuta mabao, lakini mchezo huo ulioshuhudiwa na Rais wa nane wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar, Dk. Hussein Ally Mwinyi ulimaliza dakika 90 bila timu hizo kufungana.
Hivyo, kulazimika kwenda kwenye hatua ya mikwaju ya Penalti, ambapo Yanga SC walipata penalti nne kupitia kwa Tuisila Kisinda, Shaibu Ninja, Zawadi Mauya, Saidoo Ntibazonkiza, huku kiungo Mukoko Tonombe akikosa baada ya mkwaju wake kuokolewa na mlinda mlango wa Simba, Beno Kakolanya.
Simba SC walipata penalti zao tatu kupitia kwa Francis Kahata, Chris Mugalu na Gadiel Michael, huku wachezaji Meddie Kagere na Joash Onyango wakikosa baada ya mikwaju yao kuokolewa na Mlinda mlango wa Yanga, Farouk Shikalo.
Katika mchezo huo wa fainali, Beki wa Kimataifa wa Simba SC, Joash Onyango amechaguliwa kuwa mchezaji bora wa fainali hiyo, huku Miraji Athuman wa Simba akiibuka mfungaji bora wa mashindano kwa kupachika mabao manne, Francis Kahata wa Simba akiibuka mchezaji bora wa mashindano na Golikipa wa Yanga, Farouk Shikalo akichaguliwa kuwa mlinda mlango bora.
Picha za matukio mbalimbali kwenye mchezo huo
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464