SIMBA YAMSAJILI CHIKWENDE, YANGA NAYO YAMSHUSHA MRUNDI


Mshambuliaji mpya wa Wekundu wa Msimbazi, Perfect Chikwende kutoka FC Platinum ya Zimbabwe akitambulishwa usiku wa kuamkia leo.

Na Damian Masyenene
MIAMBA ya soka nchini, Simba SC na watani wao wa jadi, Yanga SC wameendelea kuimarisha vikosi vyao kwa kuongeza majina mapya ya washambuliaji ili kuongeza nguvu kwenye safu zao za upachikaji mabao.

Baada ya kumsajili kiungo mkabaji, Thadeo Lwanga kwa ajili ya michuano ya Klabu Bingwa Afrika, Mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Wekundu wa Msimbazi wameshusha jembe lingine kutoka Zimbabwe, Perfect Chikwende wa FC Platinum kwa ajili ya kuongeza nguvu kwenye eneo la ushambuliaji.

Simba wamemtambulisha Chikwende usiku wa kuamkia leo Januari 16, 2021 kupitia kurasa zao za Instagram na kuandika ujumbe uliosomeka "Perfect Chikwende rasmi ni Mwekundu mwenzetu, tunasajili kwa ajili ya malengo makubwa ya klabu hii kubwa na hiyo ndio maana ya NEXT LEVEL. Karibu kundini Chikwende 'BULL' #NguvuMoja,".

Picha na Simba SC

Nao Mabingwa wapya wa Kombe la Mapinduzi Zanzibar, Yanga SC wamesajili mshambuliaji mpya wanaouita 'Mtambo wa Mabao' kutoka nchini Burundi akiungana na mwenzake Saidoo Ntibazonkiza ambaye ameleta uhai kwenye kikosi hicho siku za karibuni.

Mshambuliaji huyo mpya wa Yanga, Fiston Abdoul Razak ametambulishwa jana kwenye kurasa za klabu hiyo na kuandika "Karibu Jangwani, Karibu Timu ya Wananchi Fiston Abdoul Razak mtambo wa mabao, fundi wa mpira. Timu ya Wananchi imenoga msimu huu moto,".

Picha na Yanga SC

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464