Wachezaji wa Kikosi cha timu ya Taifa “Taifa Stars” wakiwa kwenye mazoezi ya mwisho yaliyofanyika Uwanja wa Centenary,Limbe kuelekea mchezo wa pili wa Kundi D mashindano ya CHAN dhidi ya Namibia utakaochezwa leo saa 4 usiku Uwanja wa Limbe,Cameroon (Picha na TFF)
Na Damian Masyenene
TIMU ya Soka ya Tanzania (Taifa Stars) leo itakuwa uwanjani tena kucheza mchezo wake wa pili wa michuano ya Mataifa Afrika kwa wachezaji wanaocbheza ligi za Ndani (CHAN) yanayofanyika nchini Cameroon.
Stars itakuwa uwanjani kuwavaa Namibia katika uwanja wa Limbe mjini Buea nchini Cameroon saa 4:00 usiku.
Mchezo huo utakuwa muhimu kwa timu zote mbili kwani zilipoteza michezo yao ya kwanza, ambapo Stars walipoteza kwa mabao 2-0 mbele ya Zambia, huku Namibia wakichapwa mabao 3-0 dhidi ya Guinea.
Hata hivyo, kwa mujibu wa taarifa zilizotolewa na Shirikisho la Soka nchini (TFF) ni kwamba Tanzania itawakosa wachezaji watatu ambao ni Erasto Nyoni, John Bocco na Ibrahim Ame ambao ni majeruhi na wapo chini ya uangalizi wa madaktari.
Wachezaji hao wote pia hawakucheza mchezo wa kwanza ambao Stars ilipoteza kwa mabao 2-0 mbele ya Zambia.
Ili kuwa na matumaini na kujiweka katika mazingira ya kusonga mbele, Taifa Stars inatakiwa kushinda mchezo huo, endapo itafungwa leo basi itakuwa kwenye hatari ya kuaga mashindano hayo.