TUME YA MADINI YASAINI MKATABA NA MCB-MUST UJENZI WA OFISI DODOMA



Leo tarehe 07 Januari, 2021 Tume ya Madini imesaini mkataba na kampuni ya MCB - MUST kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi za Makao Makuu yake jijini Dodoma.

Mkataba huo umesainiwa na Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini kwa niaba ya Tume ya Madini na Mkurugenzi wa MCB Company Limited- MUST, Ivor Ndimbo ambapo mradi wa ujenzi utasimamiwa na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA).

Walioshuhudia utiaji saini wa mkataba huo ni pamoja na Mkurugenzi wa Huduma za Sheria wa Tume ya Madini, Ayub Mwenda, Meneja Utawala na Rasilimaliwatu wa Tume ya Madini, Gift Kilimwomeshi, Kaimu Mkurugenzi wa Manunuzi, Jeremiah Mwakipesile na watendaji wengine kutoka Tume ya Madini, Wakala wa Majengo Tanzania (TBA), na MCB Company Limited.

Akizungumza kabla ya kusaini mkataba huo, Kaimu Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Venance Kasiki ameitaka kampuni hiyo kuhakikisha inakamilisha ujenzi kabla ya wakati.

"Nia yetu kama Tume ya Madini ni kuhakikisha ujenzi unakamilika mapema iwezekanavyo, ili wadau wa madini waendelee kupata huduma bora katika mazingira ambayo ni mazuri zaidi," amesema.

Kasiki amefafanua kuwa ujenzi huo ni mkakati wa Serikali katika uboreshaji wa Sekta ya Madini kwa kuhakikisha inaboresha mazingira ya kazi sambamba na utoaji wa vitendea kazi.

Katika hatua nyingine, Tume ya Madini imekabidhi eneo kwa kampuni ya MCB -MUST.



Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464