WATUMISHI 5 HOSPITALI YA UKEREWE WASIMAMISHWA KAZI KUPISHA UCHUNGUZI SAKATA LA WIZI WA DAWA ZA SH. MILIONI 200

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima

Na WAJMW-UKEREWE
Watumishi watano wa Hospitali ya Wilaya ya Nansio Ukerewe mkoani Mwanza wamesimamishwa kazi kupisha uchunguzi wa vyombo vya maadili ya utumishi wa umma pamoja na maadili ya mabaraza na bodi za kitaaluma.

Watumishi hawa ni wale sita (6) waliokuwa wamefikishwa mahakamani kujibu tuhuma za wizi wa dawa zenye thamani zaidi ya Shilingi Milioni 200 ambapo mmoja wao alikiri na kuhukumiwa kulipa milioni 100 na waliobakia walirejeshwa kazini.

Watumishi hao wamesimamishwa kazi kufuatia agizo la Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Dorothy Gwajima alipofanya ziara katika Hospitali hiyo hivi karibuni ambapo, alielezwa na Mkuu wa Wilaya ya Ukerewe Bw. Cornel Magembe kuwa naye hakuridhishwa na watumishi hao kurejeshwa kazini kwani hawaaminiki tena kwenye utumishi wa umma na kamwe haiwezekani haieleweki inawezekanaje mtumishi wa umma aibe halafu akishalipa anarejeshwa kazini.

Mara baada ya Dkt Gwajima kutembelea Hospitali ya Halmashauri ya Nansio alijionea kuendelea kuwepo kwa viashiria vya udanganyifu katika mfumo mzima wa ugavi wa dawa hivyo kukubaliana na maelezo ya Mhe Mkuu wa Wilaya kuwa bado kuna tatizo kama alivyoeleza. Hivyo, alimuagiza Mkurugenzi wa Wilaya ya Ukerewe Bi. Esther Chaula kuwasimamisha kazi watumishi hao na kuwafikisha kwenye kamati ya maadili ya utumishi wa umma, mabaraza na bodi za kitaaluma na vyama vyao ili waone kama kweli hao watumishi bado wanastahili kuaminika tena kwa mujibu wa sheria za utumishi wa umma, mabaraza na bodi za kitaaluma pia maadili ya vyama vyao vya kitaaluma.

"Mahakama imefanya maamuzi kwa mujibu wa sheria wakalipa, hata hivyo naagiza Mkurugenzi kama tulivyokubaliana uendelee kusimamia hatua za kinidhamu na kiutumishi pia uwafikishe kwenye mabaraza na bodi zao za taaluma pamoja na vyama vyao vya taaluma ili nao wawachunguze na kuwachukulia hatua. Alisema Dkt. Gwajima.

Kwa mujibu wa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dkt. Thomas Rutachunzibwa amesema watumishi hao ambao ni wataalamu wa maabara, Famasi na Daktari wameshasimamishwa kazi huku hatua zaidi za kinidhamu, maadili na kiutumishi zikiendelea kuchukuliwa dhidi yao sambamba na uchunguzi wa mabaraza na bodi za kitaaluma.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464