WAZIRI AWESO ATOA MWEZI MMOJA WANANCHI WA SHIRATI-RORYA WAPATE MAJI

Waziri wa Maji, Jumaa Aweso akizungumza na wakazi wa Shirati wilayani Rorya wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maji wilayani humo

Na Mohamed Saif, Rorya
Waziri wa Maji Jumaa Aweso ametoa siku 30 kwa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Musoma (MUWASA) kuhakikisha wananchi wa Mji wa Shirati wanapata huduma ya maji.

Ametoa maelekezo hayo Januari 6, 2021 wilayani Rorya alipotembelea mradi huo akiwa ameambatana na Mbunge wa Jimbo la Rorya, Jafari Chege na Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Simon Odunga ili kujionea hali halisi sambamba na kuzungumza na wanufaika.

Ilielezwa kwamba mradi ulisimama kutoa maji tangu mwaka 2016 baada ya mtambo wa kusukuma maji kuharibika na kwamba hadi hivi sasa hakuna hatua iliyochukuliwa.

Hata hivyo, Waziri Aweso alibainisha kwamba alikwishatoa maelekezo kwa MUWASA kufanya tathmini ya gharama zinazohitajika ili mradi wa Shirati uanze kazi.

Alimpigia simu Mkurugenzi Mtendaji wa MUWASA, CPA Joyce Msiru mbele ya msafara alioambatana nao ili kupata mrejesho wa tathmini ya gharama ya uhuishaji wa mradi ambapo alielezwa kuwa kiasi cha shilingi milioni 247 kinahitajika ili uweze kutoa maji.

Mara baada ya kuzungumza na CPA Msiru, Waziri Aweso alihoji kiasi cha fedha kilichopo kwenye akaunti ya Wakala wa Majisafi na Usafi wa Mazingira (RUWASA) Wilayani Rorya.

“RUWASA Rorya tueleze ulipokea shilingi ngapi kutekeleza miradi kwenye eneo lako na hadi hivi sasa kuna kiasi gani kwenye akaunti,” alihoji Waziri Aweso.

Akijibu swali hilo la Waziri Aweso, Meneja wa RUWASA wilayani Rorya, Mhandisi Evaristo Mgaya alisema kwamba alipokea kiasi cha shilingi bilioni 1.3 na kwamba hadi hivi sasa kiasi kilichopo kwenye akaunti ya RUWASA Rorya ni shilingi milioni 290.

Suala hilo lilimshangaza na lilimkera Waziri Aweso na hivyo alielekeza fedha hiyo badala ya kuendelea kukaa benki itumike kufanya ukarabati wa mradi wa Shirati na kwamba fedha nyingine italetwa.

“Inashangaza sana unayo fedha kwenye akaunti halafu watoto wanalala njaa hii haijakaa sawa hata kidogo; wananchi hapa kipindi chote hiki wanateseka hawana maji halafu fedha ipo tu benki imekaa haitumiki kama ilivyokusudiwa,” alisema Waziri Aweso.

Aliongeza “hili eneo lipo chini yako wananchi hapa wana shida ya maji lakini wewe unakaa na fedha na haitumiki kwa shughuli iliyokusudiwa maana yake ni kwamba majukumu haya uliyopewa yamekushinda,” Waziri Aweso alimueleza Mhandisi Mgaya.

Mara baada ya mahojiano na Mhandisi Mgaya, Waziri Aweso akiwa hapohapo kwenye eneo la mradi alimpigia simu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji, Mhandisi Anthony Sanga na kumuelekeza fedha zilizopo kwenye akaunti ya RUWASA Rorya zitumike kutekeleza mradi wa Shirati.

“Wape maelekezo kwamba hizo fedha milioni 290 zitumike na kama kuna maeneo mengine ambayo inahitajika fedha utawaletea lakini hizi zisiendelee kukaa kwenye akaunti huku wananchi wakiendelea kuteseka; kwahiyo waelekeze MUWASA waje kufanya kazi hii kesho,” Waziri Aweso alimuelekeza Katibu Mkuu Sanga.

Waziri Aweso aliisisitiza MUWASA kukamilisha mradi kwa kipindi walichokubaliana na alisema hatokubali kisingizio chochote hasa ikizingatiwa fedha yote inayohitajika inatoka leo hii yaani Januari 6, 2020.

Aliwakumbusha watendaji kwenye Sekta ya Maji kuepuka kuzoea shida za wananchi badala yake wajikite kuwatatulia kero ya maji na alibainisha kwamba kutokana na changamoto alizozishuhudia wilayani humo amejiridhisha kwamba Meneja wa RUWASA Rorya hana uwezo wa kutosha kutatua changamoto zilizopo.

Waziri Aweso alielekeza meneja huyo apatiwe majukumu mengine na kwamba apelekwe mtaalam mwingine atakayekuwa na uwezo wa kutatua changamoto zilizopo wilayani hapo.
Wakazi wa Shirati wilayani Rorya wakimsikiliza Waziri wa Maji, Jumaa Aweso (hayupo pichani) wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maji wilayani humo.
Eneo la chanzo cha maji mradi wa Shirati ambao umesimama kutoa maji tangu mwaka 2016


Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Simon Odunga akizungumza mbele ya Waziri wa Maji, Jumaa Aweso wakati wa ziara kwenye mradi wa maji wa Shirati
Mbunge wa Jimbo la Rorya, Jafari Chege akimkaribisha Waziri wa Maji, Jumaa Aweso kuzungumza na wakazi wa Shirati (hawapo pichani)


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464