MFUKO WA MAWASILIANO KWA WOTE KUWEZESHA HOSPITALI KUANZA KUTIBU KWA MTANDAO


Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile akizungumza wakati wa Semina ya kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu majukumu ya UCSAF iliyofanyika Bungeni Dodoma. Wa kwanza kulia ni Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Selemani Kakoso na wa kwanza kushoto ni Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Kundo Mathew
Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Justina Mashiba akiwasilisha taarifa ya majukumu ya Mfuko huo katika semina ya kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iliyofanyika Bungeni Dodoma.
Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso akitoa maoni yake baada ya Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Dkt. Faustine Ndugulile (hayupo pichani) kuwasilisha majukumu ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kwa wajumbe wa Kamati hiyo, Bungeni, Dodoma. Kushoto ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Anne Kilango Malecela.
Naibu Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhandisi Kundo Mathew akifafanua jambo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu kuhusu majukumu ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote, Bungeni, Dodoma. Kutoka kushoto ni Waziri wa Wizara hiyo, Dkt. Faustine Ndugulile, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Selemani Kakoso na Makamu Mwenyekiti wake, Anne Kilango Malecela.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa, Humphery PolePole (aliyeinama) akimsikiliza Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba (hayupo pichani) wakati akiwasilisha majukumu ya Mfuko huo kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Bungeni, Dodoma. Kulia ni Mbunge wa Jimbo la Monduli Frederick Lowassa

 ****
Na Celina Mwakabwale, UCSAF
Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (USCAF) umesema umeanza kutekeleza wa mradi wa tiba mtandao huduma ambayo itawawezesha madaktari bingwa walio katika hospitali za mijini kutoa huduma kwa njia ya mtandao kwa wananchi wanaoishi maeneo ya Vijijini na pembezoni mwa Tanzania.

Hayo yamebainishwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Justina Mashiba wakati akiwasilisha taarifa ya majukumu ya Mfuko huo katika semina ya kuwajengea uwezo wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu iliyofanyika Bungeni Dodoma.

Ameeleza kuwa huduma hiyo ya kimtandao itaunganisha hospitali zilizoko mijini na zile za vijijini na pembezoni ili wananchi katika maeneo hayo waweze kupata huduma za madaktari bingwa wakiwa katika maeneo yao pasipo kusafiri kwa ajili ya kufanyiwa uchunguzi na vipimo mbalimbali vya kiafya.

“Kwa huduma hii mtu aliyeko Kigoma hatalazimika tena kusafiri kwenda Muhimbili, tunataka teknolojia itusaidie ili kwamba daktari aliyeko Muhimbili aweze kumtibu mgonjwa aliyeko pembezoni”, alisema Mashiba.

Kwa upande wake Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Dkt. Faustine Ndugulile amesema kwa sasa dunia inaongelea uchumi wa kidigitali na kuongeza kuwa Tanzania kama nchi zingine haiwezi kulikwepa hilo. Dkt Ndugulile amesisitiza kuwa Wizara yake itahakikisha kuwa inaratibu masuala yote ya TEHAMA ndani ya Serikali ili kuwawezesha wananchi kupata huduma kwa wakati na kuchangia katika pato la taifa.

“Majukumu yetu ni kuhakikisha kwamba ndani ya miaka 5 tunafikisha huduma ya Mkongo wa Taifa ambayo ndio njia kuu ya mawasiliano kufikia asilima 80 ya nchi yetu”,amesema.

Naibu Waziri wa Wizara hiyo, Mhandisi Andrea Kundo amesisitiza kuwa Wizara itaendelea kushirikiana na UCSAF, makampuni ya simu pamoja na wadau wengine katika kuboresha huduma za mawasiliano kwenye maeneo mbali mbali nchini ikiwa ni pamoja na kuongeza uwezo wa minara ya mawasiliano ili kutoa huduma bora inayoendana na ukuaji wa sasa wa kiteknolojia.

Nae Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu, Selemani Kakoso ameupongeza Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kwa kazi nzuri ya kuhakikisha unafikisha huduma za mawasiliano vijijini, kutoa vifaa vya TEHAMA katika shule za UMMA pamoja na kutoa mafunzo ya TEHAMA kwa walimu wa shule hizo.

Humphrey Polepole ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Utawala na Serikali za Mitaa ambaye pia alishiriki semina hiyo, ameipongeza UCSAF kwa kujenga vituo vya TEHAMA Visiwani Zanzibar ikiwa ni moja ya utekelezaji wa miradi yake huku akishauri kuwa vituo kama hivyo vijengwe pia Tanzania Bara.

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote ulianzishwa kwa Sheria ya Bunge namba 11 ya mwaka 2006 Sura ya 422 kwa lengo la kufikisha huduma za Mawasiliano ya simu, Radio, Runinga pamoja na huduma za Posta katika maeneo ya Vijijini na Mijini kusiko na huduma hiyo au yenye mawasiliano hafifu.

Hadi sasa Mfuko umefanikiwa kufikisha huduma mbalimbali za mawasiliano ikiwa ni pamoja na kuwasha minara katika kata 633 zenye vijiji 2,320, kuunganisha mtandao wa intaneti na kutoa vifaa vya TEHAMA kwa shule 711, kutoa mafunzo ya TEHAMA kwa walimu 2,213 wa shule za UMMA kutoka Mikoa yote ya Tanzania Bara pamoja na kujenga vituo 10 vya TEHAMA visiwani Zanzibar.

Imetolewa na kitengo cha Mawasiliano, UCSAF


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464