Waziri wa Madini, Doto Biteko akiteta jambo na baadhi ya viongozi wa tume ya madini kwenye ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili kuhusu mfumo wa wazi wa mapitio na tathmini ya utendaji kazi (OPRAS) leo jijini Dar es Salaam
Na Mwandishi Wetu
WAZIRI wa Madini, Doto Biteko amewataka viongozi wa Tume ya Madini kufanya kazi kwa kujiamini huku wakifuata Sheria ya Madini pamoja na kanuni zake.
Waziri Biteko ametoa kauli hiyo leo Februari 24, 2021 kwenye ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili kuhusu mfumo wa wazi wa mapitio na tathmini ya utendaji kazi (OPRAS) yanayoshirikisha Wakurugenzi, Mameneja na Maafisa Madini Wakazi wa Mikoa wa Tume ya Madini, jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika mafunzo hayo yanayotolewa na Tume ya Utumishi wa Umma, Waziri Biteko amewataka viongozi kuhakikisha wanafanya kazi kwa kujiamini na kutatua changamoto badala ya kufanya kazi kwa kusubiri maelekezo kutoka juu.
"Ni vyema mkahakikisha mnafanya maamuzi yaliyopo ndani ya uwezo wenu kwa kuzingatia Sheria ya Madini na kanuni zake badala ya kusubiri maelekezo kutoka kwa viongozi wa juu wa Wizara," amesema Biteko
Ameendelea kusema kuwa watanzania wengi wana matarajio makubwa kwenye Sekta ya Madini na kuongeza kuwa Wizara ya Madini imejipanga katika kuhakikisha Sekta ya Madini inaendelea kukua kwa kasi huku ikiwa na mchango mkubwa kwenye ukuaji wa uchumi wa nchi.
"Nataka mfahamu kuwa kama Wizara ya Madini tunapimwa kwa ukuaji wa Sekta ya Madini, hivyo ni vyema mkahakikisha mnafanya kazi kwa kasi na ubunifu ikiwa ni pamoja na kujiamini", amesema Waziri Biteko.
Waziri Biteko akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo ya mfumo wa wazi wa mapitio na tathmini ya utendaji kazi (OPRAS) leo jijini Dar es Salaam