Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Dorothy Gwajima
TAARIFA KWA UMMA
TAMKO LA KUONGEZA KASI YA UTEKELEZAJI WA HATUA ZA KUJIKINGA NA MAGONJWA YA KUAMBUKIZA NA YASIYOAMBUKIZA NCHINI.
Dodoma, Jumatano 24 Februari, 2021.
Ndugu Wananchi, kila mwaka kipindi cha Novemba hadi Machi wimbi la magonjwa hususan yale yanayoathiri mifumo ya upumuaji na chakula huongezeka. Hii hutokana na mabadiliko ya hali ya hewa na mvua nyingi ambazo huendelea kunyesha kipindi hiki.
Magonjwa haya yanaweza kusababishwa na vimelea vya bakteria, virusi na fangasi huambukiza kutoka kwa mtu mmoja kwenda mwingine kwa njia mbalimbali ikiwemo hewa, kula au kunywa kitu ambacho siyo kisafi na salama. Mifano ya magonjwa haya ni pamoja homa za mapafu (Nimonia), mafua, malaria, kuhara, kuhara damu, kipindipindu typhoid, dengue, na mengine mengi. Baadhi ya magonjwa ya kuambukiza yanaenda na vipindi vya majira ya mwaka au kutokea kama mlipuko.
Ndugu Wananchi, tukiacha mwenendo huu wa magonjwa kila mwaka, kipindi hiki pia tumeshuhudia Dunia ikipambana na wimbi la pili la mlipuko wa ugonjwa wa COVID- 19. Kwa msingi huu tunahitaji kuongeza kasi zaidi ya kuchukua tahadhari dhidi ya mwenendo huu wa magonjwa yote haya kwenye kipindi hiki kama Wizara ya Afya tunavyoelekeza.
Ndugu Wananchi, Wizara ya Afya inayo miongozo ya kutosha ambayo imekuwa ikisambazwa na kuelimishwa na wataalamu wetu kupitia mifumo ya afya kuanzia ngazi ya taifa hadi ngazi ya kijiji. Miongozo hii imetamka bayana uhusika wa wadau wote wa sekta na wizara zote, Tawala za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, Taasisi za Umma na Binafsi kuwa nani anahusika wapi katika kila mkakati wa udhibiti wa magonjwa haya. Hivyo, kila mmoja kwa nafasi yake sasa achukue hatua na atimize wajibu wake.
Ndugu Wananchi, Mheshimiwa Rais na Waziri Mkuu wameshafanya kazi kubwa na nzuri ya kutoa matamko ya kukumbusha na kuelimisha taifa juu ya mwelekeo wa tahadhari za kuchukua ili kuepuka mlipuko wa ugonjwa wa COVID-19. Vilevile, Viongozi wa Wizara ya Afya tumetoa matamko mbalimbali ya kuwakumbusha na kuwaelimisha wananchi kuchukua tahadhari.
Ndugu Wananchi, Jukumu la kinga dhidi ya magonjwa yote yakiwemo ya kuambukiza na yasiyoambukiza ni la kila mmoja wetu. Aidha, niwakumbushe viongozi wa Serikali na sekta binafsi, Viongozi wa Kijamii, Viongozi wa Dini wa Madhehebu mbalimbali ngazi zote tuache kusubiri matamko zaidi bali tuamke tuwajibike kila mmoja kwa nafasi yake.
Ndugu Wananchi, Napenda kurudia kuelimisha na kufafanua tena juu ya mambo muhimu ya kuzingatia katika kutekeleza hatua za tahadhari za kujikinga na magonjwa ya kuambukiza na milipuko kwa ujumla wake ikijumuisha na tahadhari dhidi ya tishio la mlipuko wa COVID-19 kama ifuatavyo;
Kwanza tuondoe hofu zinazojengwa bila sababu wala nia njema kwa sababu hofu inaleta madhara zaidi kiafya.
Tuendeleze tabia ya kunawa mikono mara kwa mara kwa maji safi tiririka na sabuni. Iwapo maji tiririka na sabuni hakuna, tumia vipukusi (sanitizer). Namuelekeza Mfamasia Mkuu wa Serikali kuendelea kutoa elimu ya jinsi gani tunaweza kutengeneza vipukusi vyetu vya ndani ya nchi ili kuwezesha wananchi kupata kwa bei nafuu.
Vaa barakoa safi na salama ambayo umetengeneza mwenyewe au umenunua kwa watengenezaji wa ndani waliothibitishwa na Wizara ya Afya mfano Bohari ya Dawa, taasisi zetu za afya na watengenezaji wengine ambao tumewathibitisha.
Naelekeza Mfamasia Mkuu wa Serikali tangaza orodha ya watengenezaji wa barakoa ambao tumeshawathibitisha, pia elimisha jinsi ya kutengeneza barakoa binafsi. Vaa barakoa kwa kuzingatia muongozo uliotolewa na Wizara hususan katika maeneo ya msongamano. Naelekeza elimu juu ya uvaaji wa barakoa iendelee kutolewa na wataalamu wa Afya.
Fanya mazoezi mara kwa mara. Kumbuka mazoezi yapo ya aina nyingi na unaweza kuchagua kutegemeana na hali ya afya yako na mazingira yako siku hiyo. Baadhi ya mazoezi rahisi ni kama vile kutembea kwa kasi siyo chini ya dakika 30 au zaidi walau utoke jasho, kuruka kamba, kukimbia mwendo unaoona unakufaa na kufanya zoezi la kusimama-kaa nk. Naelekeza Mwongozo wa Mazoezi utolewe.
Fanya mabadiliko ya tabia ya lishe unayotumia kwa kuhakikisha unapata lishe bora ikiwemo matunda na mbogamboga kwa gharama nafuu kulingana na mazingira ya vyakula vya asili katika eneo lako. Naelekeza Wataalamu wa lishe ngazi zote kuandaa daftari la orodha ya vyakula vya asili vinavyopatikana eneo husika na kutoa elimu ya milo ipi iandaliwe kama kielelezo cha lishe bora. Tuache kuamini kuwa lishe bora ni vyakula vya kisasa vya biashara na vya bei ghali.
Tambua afya yako jilinde tukulinde. Wito huu unahusu makundi maalumu ya watu wakiwemo wenye umri mkubwa (wazee), watu wenye uzito uliopitiliza (wanene) na watu wenye magonjwa sugu (muda mrefu) mfano Pumu, Shinikizo la juu la Damu, Kisukari, Magonjwa ya Moyo na Figo. Kundi hili mara nyingi huathirika zaidi na magonjwa ya kuambukiza kutokana na hali ya kinga zao kuwa haiko imara zaidi hivyo, naelekeza wataalamu wa Afya muendelee kutoa elimu zaidi mkiwashirikisha Wahudumu wa Afya ngazi ya Jamii.
Pia, naelekeza kundi hili liwekewe mazingira mazuri ya kupata huduma za afya kwenye vituo vyetu ikiwemo kuruhusu baadhi ya dawa za kutibu magonjwa sugu kupatikana kwenye vituo vya afya na zahanati ili kuwapunguzia kwenda mara kwa mara kwenye hospitali kubwa za halmashauri au mkoa. Vilevile Mfamasia Mkuu wa Serikali na Mkurugenzi wa Tiba msimamie mwongozo wa huduma kwa makundi maalum. Madirisha ya huduma za afya kwa wazee yaimarishwe sambamba na kliniki za magonjwa sugu.
Tumia tiba asili za kunywa na kujifukiza zilizosajiliwa na Baraza la Tiba Asili kama inavyoelimishwa na wataalamu husika. Tangu tarehe 21 Februari, 2021 Wizara inatekeleza wiki nne za elimu ya tiba asili kwa kurusha vipindi mbalimbali vya redio na televisheni. Elimu hii itawafikia wananchi wa makabila yote kwa lugha zao. Kilele cha zoezi hili kitafanyika hapa Dodoma ambapo, wataalamu wote wa huduma ya tiba asili watakuwepo kufanya maonesho na utaratibu huu utakuwa unafanyika kila baada ya siku 90 kwa mzunguko kila Kanda.
Hivyo, natoa wito kwa wananchi kufuatilia vipindi vya elimu hii. Naagiza waratibu wa tiba asili ngazi zote za mkoa na halmashauri nao waende kwenye redio za maeneo yao watoe elimu kama hii tunayotoa ngazi ya taifa.
Aidha, narudia tena kuzitaja bidhaa za tiba asili ambazo tulizitaja awali kuwa zimeshasajiliwa na baraza la tiba asili kwa ajili ya magonjwa yanayohusu mfumo wa hewa kuwa ni pamoja na bidhaa dawa (COVIDOL, NIMRCAF, PLANET++, BINGWA, COVOTANXA), Mafuta tete (UZIMA HERBAL DROPS, BUPIJI, EUCALYPTUS OIL, LEMONGRASS ESSENTIAL OIL). Bidhaa zingine zitaendelea kutajwa na Baraza la Tiba-Asili kadri zinavyoendelea kusajiliwa.
Habari njema ni kuwa, tumeshakaa na wamiliki wa bidhaa hizi na kuweka utaratibu zipatikane nchi nzima kwa bei nafuu kuanzia kwenye maeneo ya vituo vya kutolea huduma za afya na kwenye maduka mbalimbali ya dawa . Tunawashukuru wadau wote kwa ushirikiano wao wa kusogeza huduma hizi karibu na wananchi.
Epuka misongamano isiyo ya lazima ikiwemo kwenye vyombo vya usafiri. Wizara husika isimamie kwa kurejea mwongozo wa afya eneo husika.
Wahi kituo cha kutolea huduma za afya mara uonapo dalili za maradhi ili watoa huduma wapate nafasi nzuri zaidi ya kutibu. Aidha, jenga tabia ya kupima afya yako mara kwa mara angalau mara 1 kwa mwaka hata kama huumwi.
Niwatake Maafisa Afya wanaotoa huduma mipakani kuendelea kuimarisha udhibiti wa magonjwa katika maeneo ya mipakani kwa mujibu wa miongozo husika
Ndugu Wananchi, kwa maelezo haya niwasihi tena wadau wote kuwa sasa ni wakati wa kujikita kwenye kutekeleza yaliyotamkwa, kufafanuliwa na kuelimishwa kwa kushirikiana na viongozi na wataalamu wetu ngazi zote za mfumo wa Serikali. Niwaombe Viongozi wote kuanzia Waheshimiwa Mawaziri, Manaibu Mawaziri, Waheshimiwa Wakuu wa Mikoa na Wakuu wa Wilaya, Makatibu Wakuu na Manaibu Katibu Wakuu, Makatibu Tawala wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri, Wataalamu wote Afya na Sekta zote sasa tubebe silaha zetu za miongozo ya afya, uzalendo, uthubutu na ujasiri twendeni tuongeze kasi zaidi ya utekelezaji kila mmoja kwa kadri ya eneo lake.
Kwa kutekeleza mikakati niliyoeleza hapo juu tutakuwa tunajikinga na kutibu hata magonjwa yasiyoambukiza hivyo, miili yetu itaziidi kuwa imara zaidi dhidi ya magonjwa ya kuambukiza.
Ndugu Wananchi, Napenda kuwakumbusha kuwa, kama taifa tunazo ajenda nyingi za kufanyia kazi ili kuchochea kasi ya maendeleo. Hivyo tushikamane kutekeleza yale tuliyokwisha pokea kutoka kwa viongozi wetu . Mheshimiwa Rais wetu kila siku anatukumbusha kuwa tuko kwenye vita ya uchumi hivyo tusimame imara kulinda Afya zetu kwa maendeleo ya Taifa letu.
Ndugu Wananchi, Adui maradhi tunamjua na silaha za kumpiga tunazo na mara nyingi tulishampiga na tukamshinda hivyo tubebe silaha twende mstari wa mbele tukampige tena. Silaha zetu ni kuzingatia miongozo yetu ya Afya na umoja wetu wa kuwajibika kwenye utekelezaji wa miongozo hiyo kila mmoja kwa nafasi yake. Ni katika umoja wa kitaifa kwenye kukabiliana na changamoto mbalimbali ndiyo tutashinda. Tubebe maono, uthubutu na ujasiri wa Mheshimiwa Rais wetu tuondoe hofu tuchape kazi huku tukichukua tahadhari.
Ndugu Wananchi, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto iko kwenye mwelekeo wa kuimarisha zaidi misingi ya afya bora kwa kujenga ushirikiano wa karibu zaidi na imara zaidi na sekta zote zinazobeba ajenda ya afya kwenye utekelezaji wao. Lengo ni kumkabili adui maradhi kwa kusuka upya na kuimarisha zaidi mifumo na mikakati ya kudhibiti magonjwa yote ya kuambukiza na yasiyoambukiza bila kusahau nafasi ya tiba asili. Mwelekeo huu ni wa uwekezaji wa afya kwa vizazi vingi vijavyo katika taifa hili ambapo mtoto wa shule ya msingi anaanza kujengewa uwezo wa kupambanua changamoto za afya na mikakati ya kujikinga na maradhi.
Ndugu Wananchi, Nachukua fursa hii kuwapongeza Wizara na sekta zote pamoja na Wadau wote wakiwemo wananchi kwa kushirikiana vyema kwenye kuchochea na kuleta mabadiliko endelevu ya tabia kuelekea kwenye kulinda na kuimarisha afya. Tuzidi kushirikiana daima. Nawapongeza Wataalamu wetu wa afya kwa kujitoa kwao daima katika kutetea afya za watanzania.
Kwenu Wajumbe wa Chama cha Wataalamu wa Maendeleo ya Jamii (CODEPATA), nyie ndiyo nguzo ya maendeleo ya jamii kwa kuwa mnazo funguo za kubadilisha fikra za jamii. Twendeni mstari wa mbele kwenye kuifikia jamii na kuchochea mabadiliko ya fikra ili wapokee miongozo ya afya na kuitekeleza bila kusukumwa. Mnayo nafasi yenu kwenye kufikia malengo ya afya ngazi zote.
Ndugu Wananchi, Viongozi na Wadau wote kwa ujumla, Wataalamu wa Wizara ya Afya kwa ushirikiano na sekta zote kuanzia leo hii muda huu wataanza kufanya ufuatiliaji wa kina wa utekelezaji wa matamko, miongozo na maelekezo yote ambayo yamekuwa yakitolewa. Pale ambapo utekelezaji uko vizuri tutapongeza hadharani na pale ambapo utekelezaji uko dhaifu bila sababu za msingi tutachukua hatua stahiki za uwajibikaji kwa mujibu wa sheria, taratibu na kanuni. TUKO KWENYE VITA YA MARADHI YANAYOATHIRI UCHUMI NA VITA SIKU ZOTE SI LELEMAMA. HIVYO KILA MMOJA ASIMAME KWA NAFASI YAKE.
Mwisho, niwatakie watanzania wote ari na kasi zaidi katika kushikamana kwenda mstari wa mbele kutekeleza mikakati ya kujikinga na kujilinda na magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza ili kuendelea kuimarisha afya zetu na kuilinda nchi yetu dhidi ya magonjwa ya milipuko inayozuilika.
Imetolewa na:
Dkt. Dorothy Gwajima (Mb)
WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII,
JINSIA, WAZEE NA WATOTO
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464