Na Catherine Ngowi, Kishapu
Shirika la OPE (Organization of People Empowement) limefanya tathmini juu ya Mradi wa Kutokomeza mimba na ndoa za utotoni wilayani Kishapu Mkoa wa Shinyanga, huku likieleza kuwepo kwa matokeo chanya kwa jamii kubadilika na kutoa taarifa na ushahidi wa vitendo hivyo.
Tathmini hiyo imefanyika leo Februari 4, 2021 katika ukumbi wa halmashauri ya wilaya Kishapu ikiongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa halmashauri hiyo, Joseph Swalala.
Mradi huo unaotekelezwa katika kata ya Busangwa wilayani Kishapu ulianza mwaka 2015 ukiwa na lengo la kuijengea jamii uelewa wa kutambua mila kandamizi zinazochangia mimba na ndoa za utotoni kupitia mikutano ya hadhara kutoa elimu kwa wanajamii kupinga mila potofu zinazochangia mimba na ndoa za utotoni.
Akifungua kikao cha tathmini, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kishapu, Joseph Swalala amesema kuwa jamii inahitaji elimu ya kutosha juu ya masuala ya ukatili na ndoa za utotoni, ambapo ameliomba Shirika la OPE kuendelea kuielimisha jamii juu ya masuala ya kupinga mimba na ndoa za utotoni.
Kaimu Mkurugenzi huyo amelipongeza Shirika la OPE kwa kazi wanayoifanya ya kuhakikisha mimba na ndoa za utotoni katika wilaya hiyo zinatoweka na kusisitiza walezi na maafisa maendeleo ya Jamii ngazi ya kata kufuatilia maendeleo ya klabu ‘mashuleni ili kuwapa elimu juu ya madhara ya mimba na ndoa za utotoni.
“Nawaomba Shirika la OPE kuendelea na harakati hizi za kuoa elimu kwa jamii juu ya mila kandamizi zinazopelekea mimba na ndoa za utotoni kwa kushirikiana na Maafisa Maendeleo ya Jamii Kata,” amesema Swalala.
Akitoa tathimini hiyo, Afisa Miradi wa Shirika la OPE, Joseph Kasya amesema kupitia mradi wa Kutokomeza Mimba na Ndoa za Utotoni kuna mafanikio makubwa kwani jamii inatoa taarifa na ushahidi juu ya unyanyasaji wa kijinsia na ukatili kwa watoto pamoja na mimba na ndoa za utotoni.
Ameongeza kwa kueleza kuwa wazazi na walezi wamepata uelewa mzuri wa malezi ya watoto wao hivyo kupelekea kupungua kwa mimba na ndoa za utotoni.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa OPE, William Pius Shayo amewataka wazazi na walezi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na dawati la jinsia kuhakikisha kwa pamoja wanasimama kuwalinda watoto ili kuepuka kukatisha ndoto na malengo yao.
“Sisi kama jamii tuna wajibu mkubwa wa kuhakikisha watoto wetu wanatimiza ndoto zao kwa kupinga mila kandamizi zinazopelekea mimba na ndoa za utotoni hivyo tuendelee kushirikiana kwa pamoja kutekeleza hilo. Pia natoa shukrani zangu kwa ofisi ya mkurugenzi kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na dawati la jinsia kwa ushirikiano mkubwa wanaoendelea kutupatia” amesema Shayo.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464