EWURA YADHIBITI UCHAKACHUAJI MAFUTA KUTOKA 80% HADI 4%, MATUMIZI GESI ASILIA YAFIKIA TANI 189,509

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Mhandisi Godfrey Chibulunje akifafanua mambo mbalimbali yanayoihusu mamlaka hiyo na udhibiti wa mamlaka mbalimbali zilizo chini ya Ewura, leo jijini Mwanza katika kikao cha pamoja na waandishi wa habari Kanda ya Ziwa

Na Damian Masyenene, Mwanza
MAMLAKA ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) imesema kuwa tangu kuanza kwa udhibiti wa umeme, petroli, gesi asilia na maji mwaka 2016, imeweza kudhibiti mfumuko wa bei kiholela na kuboresha utendaji kazi wa mamlaka mbalimbali zilizo chini yake.

Ambapo katika sekta ya mafuta, EWURA imeweza kuchangia jumla ya Sh Bilioni 67.6 katika mfuko mkuu wa serikali tangu mwaka 2017, huku wakifanikiwa kupunguza uchakajuaji wa mafuta kutoka asilimia 80 mwaka 2017 hadi asilimia nne mwaka 2020, huku wakiendelea kupambana ili kumaliza kabisa changamoto hiyo.

Hayo yameelezwa leo na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Mhandisi Godfrey Chibulunje wakati wa kikao na waandishi wa habari kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa (Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Geita na Mara) kuelezea majukumu, mafanikio na changamoto za mamlaka hiyo.

Mhandisi Chibulunje ameeleza kuwa kutokana na kuanzishwa kwa mfumo wa matumizi ya vinasaba kwenye mafuta, imesaidia ongezeko la mapato ya Serikali Sh Bilioni 468.50 mwaka 2014, huku tangu kuanza kwa udhibiti wa bei za mafuta mwaka 2009 umesaidia kudhibiti upandishwaji kiholela wa bei na kuongezeka kwa kipato cha mwananchi jumla ya Sh Bilioni 445.5 mwaka 2009 hadi 2010 na kuongezeka pato la Serikali Sh Bilioni 49 tangu Julai 2009 hadi Juni 2010.

Kaimu Mkurugenzi huyo amebainisha kuwa hadi mwaka 2020, jumla ya leseni 1,515 zimetolewa na EWURA katika sekta ya mafuta na mafundi 3,500 wamepewa leseni za kuunganisha nyaya za umeme wa majumbani, huku matumizi ya gesi asilia yakiongezeka na kufikia tani 189,509 mwaka 2019/2020 kutoka tani 10,000 mwaka 2016.

"Hadi kufikia Juni 30, mwaka jana kampuni 470 zilihorodheshwa na wazawa kushika madaraka katika kampuni za gesi asilia na tunasimamia na kudhibiti mamlaka 25 za maji za mikoa, 61 za wilaya na miradi nane ya kitaifa. Kumekuwa na matokeo chanya ya udhibiti katika sekta ya maji ambapo mamlaka 84 kati ya 130 zimeweza kuandaa mipango ya biashara, zingine 39 zimeweza kuwa na bei za maji zinazozingatia mipango ya biashara ya miaka mitatu.

"Asilimia 60 ya malalamiko tunayoyapokea yanahusu mamlaka za maji na asilimia 75 ya hizo ni kuhusu ankara za maji. Ndiyo maana kwa sasa tumesitisha michakato yote ya upandishaji wa bei za maji kwenye mamlaka zote za maji nchini hadi tutakapojiridhisha na changamoto zilizopo," amefafanua.

Akielezea mafanikio ya jumla ya mamlaka hiyo, Mhandisi Chibulunje amesema kuwa ni pamoja na kutatua migogoro kwa kushamirisha uwazi na kulinda walaji, ambapo migogoro mingi inahusu usahihi wa ankara za umeme na maji, kuchelewesha kuunganishiwa huduma na kuuziwa mafuta machafu.

"EWURA ni miongoni mwa wadhibiti wa mfano katika bara la Afrika na mamlaka nyingi za ndani na nje ya nchi zimekuwa zikijifunza kupitia Ewura, pia tumesaidia kuzuia mfumuko wa bei na kuimarisha mamlaka za maji nchini," ameeleza.

Kwa upande wake, Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, George Mhina amewahimiza waandishi wa habari kuitumia elimu waliyoipata kuwa msaada wa kuongeza ufahamu wa masuala mbalimbali yanayohusu mamlaka hiyo na kuwa mabalozi kwa wengine kwani itawasaidia kupata taarifa sahihi kuhusu Ewura na udhibiti kwa ujumla, huku akiwaomba waandishi hao kuendelea kushirikiana na kufanya kazi kwa ukaribu.

Baadhi ya Waandishi wa habari wakichangia hoja katika kikao hicho, wamehoji namna ambavyo mamlaka mbalimbali zilizo chini ya Ewura zinavyowajibika katika kulipa fidia, udhibiti wa bei, ubora wa huduma hususan Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) limekuwa likilalamikiwa kwa huduma isiyo ya uhakika katika baadhi ya mikoa ya Kanda ya Ziwa.

Mmoja wa Waandishi hao, Novatus Lyaluu ambaye pia ni Katibu Mtendaji wa Klabu ya Waandishi wa habari mkoa wa Geita, alipendekeza mamlaka kuwa na udhibiti katika huduma za uunganishaji umeme kwa mafundi wa majumbani kwani kumekuwa na bei holela, huku Constantine Mathias kutoka Simiyu akihoji juu ya adhabu (faini) zinazotozwa na mamlaka mbalimbali juu ya ucheleweshaji wa malipo ya Ankara kama zinathibitiwa na EWURA.

Naye Josephine Charles kutoka Shinyanga ambaye ni Mwanachama wa Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Shinyanga (SPC) alihoji juu ya kwanini kumekuwa na utofauti wa bei elekezi katika bidhaa ya mafuta ya petroli kwenye mikoa mbalimbali.

Mwenyekiti wa Klabu ya Waadishi Mkoa wa Mwanza, Edwin Soko akitoa shukrani kwa niaba ya waandishi wa habari amesema kuwa wanahabari wanalo jukumu la kufanya kazi kwa ushirikiano mkubwa na wadau wote wa maendeleo, nafasi hiyo ya kuwakutanisha Ewura na wanahabari ni hatua kubwa kwa mamlaka hiyo, huku akiiomba kuendeleza ushirikiano huo mara kwa mara.

"Kwa wenyeviti wenzangu wa klabu za waandishi wa habari sisi ni jeshi kubwa na tuna kazi ya kuongoza wenzetu katika kufanya kazi kwa ustadi mkubwa kwa kuwaunganisha na kushirikiana na wadau mbalimbali...Tunawaomba wenzetu wa EWURA wazidi kutuunga mkono na tunatamani mwaka ujao hafla hii iwe kubwa zaidi na iwe ya kitaifa," amesema. 
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Mhandisi Godfrey Chibulunje akwasilisha mambo mbalimbali yanayoihusu mamlaka hiyo mbele ya Waandishi wa habari kutoka mikoa ya Kanda ya Ziwa, leo jijini Mwanza
Meneja wa EWURA Kanda ya Ziwa, George Mhina akizungumza katika kikao hicho
Mkuu wa kitengo cha Mawasiliano na Mahusiano EWURA, Titus Kaguo akieleza namna ambavyo mamlaka hiyo imekuwa na ushirikiano na waandishi wa habari na kufanya kazi kwa ukaribu
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa EWURA, Mhandisi Godfrey Chibulunje (kulia) akitoa ufafanuzi wa hoja mbalimbali zilizowasilishwa na wanahabari
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Mwanza, Edwin Soko akitoa neno la shukrani kwa niaba ya waandishi wa habari waliohudhuria hafla hiyo
Waandishi wakifuatilia kikao hicho kwa umakini
Waandishi wa habari wakiendelea kufuatilia hoja mbalimbali zilizokuwa zikiwasilishwa katika kkao hicho
Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC), Greyson Kakuru (wa kwanza kulia) akiwa ni sehemu ya kikao hicho
Kikao kikiendelea
Washiriki wakiendelea kuchukua dondoo za mawasilisho mbalimbali katika kikao hicho
Mwakilishi wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC), Josephine Charles akifuatilia kikao
Kikao kikiendelea
Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya Waandishi wa Habari Mkoa wa Shinyanga (SPC), Patrick Mabula akifuatilia kikao kwa ukaribu
Kikao kikiendelea
Mtangazaji wa Faraja FM ya Shinyanga, Josephine Charles akichangia hoja kwenye kikao hicho
Katibu Mtendaji wa Klabu ya Waandishi wa habari Mkoa wa Geita, Novatus Lyahuu akichangia hoja

Mwandishi wa habari gazeti la Uhuru mkoani Simiyu, Costantine Mathias akichangia hoja kwenye kikao hicho
Baadhi ya wawakilishi kutoka Klabu ya Waandishi wa habari mkoa wa Mwanza (MPC) wakiwa sehemu ya kikao hicho
Mwandishi Sitta Tuma wa EATV mkoani Simiyu naye akichangia hoja katika kikao hicho
Mkurugenzi wa Malunde 1 Blog, Kadama Malunde akiwa sehemu ya kikao hicho

Picha zote na Marco Maduhu

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464