HIFADHI YA BONDE LA KILOMBERO NI MUHIMU KWA MAISHA, ACHENI KUFANYA SHUGHULI ZA KIBINADAMU DPP BISWALO

 Mkurugenzi wa Mashtaka Bw.Biswalo Mganga akihutubia wageni walioshiriki katika hafla ya uzinduzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wilaya ya Kilombero uliofanyika tarehe 15 Februari,2021

NA OFISI YA TAIFA YA MASHTAKA-MOROGORO.

Mkurugenzi wa Mashtaka Bw Biswalo Mganga amewataka Wananchi wanaofanya shughuli za kilimo katika maeneo ya hifadhi kusitisha shughuli hizo  na kwenda kutafuta sehemu nyingine za kuendeshea shughuli zao ili kulinda mazingira.

Akizungumza wakati wa hafla ya ufunguzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Kilombero alisema wakati wote maslahi ya Taifa yanatangulia maslahi binafsi hivyo ulinzi wa hifadhi ni jambo.muhimu katika kulinda maslahi mapana ya  Taifa.

Alisema bonde la Kilombero ni eneo linalotegemewa sana katika mradi wa Umeme wa Mwalimu Nyerere unaojengwa Rufiji Pwani hivyo uharibifu wa maliasili katika bonde hilo haukubaliki hata kidogo.

Alisema mpaka hivi sasa bado wapo watumishi wa Serikali wanaenda kulima na kufuga katika maeneo ya Bonde la mto Kilombero  ninawataka waache kufanya hivyo kwa kuwa wanaharibu mazingira.

"Sitaangalia sura ya mtu, awe mbunge,mwanasiasa, kiongozi wa dini katika kulinda bonde hili.nitachukua hatua kwakuwa maslahi binafsi hayawezi kuzidi maslahi ya Watanzania Milioni Sitini." Alisisitiza Mkurugenzi wa Mashtaka Mganga.

Alisema Serikali imewekeza fedha nyingi katika mradi wa Umeme wa Mwalimu Nyerere na Bwawa hilo kwa kiasi kikubwa linategemea maji kutoka Kilombero hivyo uharibifu ukitokea halafu maji yakikosekana   Taifa litakuwa limepoteza fedha nyingi, lakini tukizembea fedha za Taifa zitakuwa zimepotea. 

Aidha, alisema kuwa  muendelezo wa shughuli za kilimo kwenye maeneo hayo   husababisha nchi yetu itaendelea kuagiza umeme kutoka nje ya nchi, viwanda vyetu vitaendelea kukosa umeme wa uhakika.

Nikiwa mimi DPP  sitaangalia sura ya mtu, Maslahi ya Mbunge au diwani tunaweka pembeni wakati wote tunatanguliza maslahi ya Taifa kwa kuwa hatuwezi kuona mradi wa umeme wa Mwalimu Nyerere unaharibika kwa sababu ya maslahi ya watu wachache.

Niwaombe  Wakuu wa Wilaya msirudi nyuma kuhakikisha mnazuia shughuli za kibinadamu katika eneo hilo  na kuhakikisha  Sheria zibafuatwa, pia wananchi wahakikishe wanatafuta maeneo mengine ya kulima. Alisisitiza Mkurugenzi wa Mashtaka.

Mkurugenzi wa  Mashtaka nchini DPP Biswalo Mganga akiwa pamoja na wakuu wa Wilaya za Kilombero Mhe.Ismail Mlawa  na Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Stephano Kaliwa wakielekea eneo la tukio kwa ajili ya ufunguzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wilayani Kilombero.
Viongozi wa dini mbalimbali, watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero na wananchi wakimsikiliza Mkurugenzi wa Mashtaka (hayupo pichani) wakati akihutubia katika hafla ya uzinduzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wilaya ya Kilombero iliyofanyika mjini Ifakara  tarehe 15 Februari, 2021.
Baadhi ya Wafanyakazi wa Ofisi ya Taifa ya  Mashtaka Mkoani Morogoro wakiwa wameketi kwa pamoja wakiendelea kufautilia hotuba za viongozi wa wilaya.
Viongozi mbalimbali wakiwepo Wakuu wa Wilaya na Viongozi wa dini wakiongozwa na Mkurugenzi wa Mashtaka Bw. Biswalo Mganga wakikata utepe kuashiria ufunguzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Kilombero uliofanyika  tarehe 15 Februari,2021.
Mkurugenzi wa Raslimali Watu na Utawala Bw. Seushi Mburi akitoa neno la shukrani wakati wa hafla ya ufunguzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka wilayani Kilombero uliofanyika  tarehe 15 Februari,2021
Mkuu wa Wilaya ya Kilombero Mhe.Ismail Mlawa akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Kilombero uliofanyika  tarehe 15 Februari,2021 mjini Ifakara


Mkuu wa Wilaya ya Malinyi Mhe. Stephano Kaliwa akihutubia katika hafla ya ufunguzi wa Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Wilaya ya Kilombero uliofanyika tarehe 15 Februari,2021 mjini Ifakara.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464