Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba
Na Damian Masyenene
MTOTO mmoja (jina linahifadhiwa) mwenye umri wa miaka 9 mkazi wa kata ya Usule halmashauri ya wilaya ya Shinyanga ambaye ni mwanafunzi wa darasa la tatu amefanyiwa vitendo vya ukatili kwa kujeruhiwa kwa kuchomwa na moto sehemu mbalimbali za mwili wake na wazazi wake ambao walimtuhumu kuiba karanga.
Mwanafunzi huyo alikutwa na mkasa huo Februari 7, mwaka huu saa 7 mchana katika kijiji na kata ya Usule wilayani hapa mkoa wa Shinyanga, ndipo Mwenyekiti wa kitongoji hicho, Peter Mahona (45) alipomgundua mtoto huyo na kuziharifu mamlaka.
Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga linawashikilia wazazi wa mtoto huyo, ambao ni Christina Mwagi (29) ambaye ni mama mzazi na Yohana Michael (34) ambaye ni baba wa kambo wakituhumiwa kuhusika na ukatili huo.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa leo na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga, ACP Debora Magiligimba, majeruhi wa tukio hilo anaendelea kupatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa mkoa wa shinyanga na hali yake ni mbaya.
Kamanda Magiligimba amebainisha kuwa watuhumiwa watafikishwa mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.
Hata hivyo, ACP Magiligimba ametoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuendelea kutoa taarifa za ukatili dhidi ya watoto kwa jeshi la polisi ili kukomesha vitendo hivyo.
Muonekano wa majeraha mbalimbali kwenye miguu ya mtoto huyo yaliyotokana na kuunguzwa moto (Picha na: Marco Maduhu)