MAMA SAMIA MGENI RASMI MKUTANO WA KIMATAIFA WA UWEKEZAJI SEKTA YA MADINI

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan

Tito Mselem na Steven Nyamiti, Dar es Salaam
MAKAMU wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mama Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kesho katika Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini kwa Mwaka 2021 wenye lengo la kutangaza fursa za uwekezaji katika Sekta ya Madini zilizopo nchini.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Madini, Doto Biteko leo wakati akizungumza na Wahariri wa vyombo vya habari kwenye kikao kilichofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar Es Salaam.

Waziri Biteko amesema kuwa mkutano huo wenye kauli mbiu ya 'Sekta ya Madini kwa Uchumi Imara na Maendeleo Endelevu' utaanza kesho Februari 21, 2021, ambapo utahusisha washiriki mbalimbali, viongozi na wataalam wa Madini kutoka nchi mbalimbali na makampuni ya Madini kutoka ndani na nje ya nchi.

Pia, Waziri Biteko amesema mkutano huo utakwenda sambamba na maonesho ya shughuli za utafutaji, uchimbaji, Uongezaji thamani, biashara ya madini na namna ya uchakataji wa Madini ya Ujenzi na ya Viwandani.

“Pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji tulizonazo kwenye Sekta ya Madini ambao utasaidia kupata wawekezaji katika shughuli za madini, kongamano linaloanza tarehe 21 pia litasaidia kupata maoni kutoka kwa wachimbaji na wadau wengine namna ya kuboresha zaidi usimamizi wa Sekta, Kuwaunganisha kati ya watumiaji wa madini hususan wenye viwanda na wachimbaji wa madini” ameeleza Biteko.

Akiwaeleza Wahariri na Wanahabari kuhusu Mkutano unaoanza tarehe 21, Waziri Biteko amesema kwa Mwaka huu, Wizara ya Madini imeandaa tuzo kwa wadau waliofanya vizuri katika kutekeleza Sheria zinazosimamia Sekta ya Madini kwa kutambua mchango wa mlipa kodi mzuri na wadau walioshiriki vizuri kwa jamii (CSR) hapa nchini.

“Ili kuhamasisha masuala ya uongezaji thamani madini nchini ikiwemo kuwafanya watanzania kutumia bidhaa za mapambo ya madini ya vito yanayopatikana hapa nchini, tumeandaa maonesho maalum ya bidhaa hizo za mapambo ili kueleza kuwa, vitu kama hivi vipo na vinatengenezwa na watanzania hapa hapa nchini,” amesisitiza Biteko.

Pia, Biteko amesema kuwa Mkutano huu utakaoanza tarehe 21 una lengo la kuwaunganisha pamoja Wachimbaji na Watoa huduma katika shughuli mbalimbali zinazofanyika migodini, kuutangazia ulimwengu kuwa Tanzania kuna mazingira mazuri ya uwekezaji sambamba na uwepo wa madini mbalimbali.

Waziri Biteko ametumia nafasi hiyo kuwakaribisha wananchi kujionea maonesho ya madini yanayoanza tarehe 21 ili watambue madini mbalimbali yanayopatikana hapa nchini, kutambua shughuli za uchimbaji madini zinazofanyika kwa kampuni kubwa zinazochimba madini, ndogo na za kati ambazo zote zinashiriki maonesho hayo.
Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumza na Wahariri wa Vyombo vya habari jijini Dare es Salaam leo katika maandalizi ya mkutano huo wa kimataifa
Mkutano wa Waziri wa Madini, Doto Biteko na wahariri wa vyombo vya habari ukiendelea kwa ajili ya maandalizi ya mkutano wa kimataifa wa uwekezaji katika sekta ya madini utakaoanza kesho jijini Dar es Salaam
Wahariri wa vyombo vya habari wakinakili vitu muhimu wakati wa mkutano wao na Waziri wa Madini, Doto Biteko leo Jijini Dar es Salaam
Mabango yanayotangaza rasilimali za Tanzania yakiwa tayari kwa ajili ya kupamba mkutano huo
Sehemu ya maandalizi ya mkutano huo utakaoanza kesho


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464