NDOA ZA MITAALA CHANZO CHA UTELEKEZAJI FAMILIA SHINYANGA, MKE ASIMULIA ALIVYOTELEKEZWA KISA GUNIA 50 ZA MCHELE


Pete

Salvatory Ntandu - Shinyanga
Imebainishwa kuwa uwepo wa ndoa za wanawake wengi (mitaala) zinazopendwa na jamii ya wafugaji na wakulima katika kata ya Salawe halmashauri ya wilaya ya Shinyanga mkoani hapa zimetajwa kuwa chanzo cha utelekezaji wa familia na kusababisha wanawake wengi hasa wa vijijini kuishi maisha duni na watoto wao kutopata mahitaji ya msingi.

Kauli hiyo imetolewa jana na Afisa Maendeleo ya Jamii Kata ya Salawe katika halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, Magesa Michael wakati akizungumza na Shinyanga Press Club Blog kwa lengo la kufahamu mambo mbalimbali ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto katika eneo hilo kwa usimamizi wa Shirika la Women Fund Tanzania (WFT) ili kutokomeza matukio hayo kwenye jamii.

Alisema kuwa kwa siku moja wanapokea kesi zaidi ya tano zinazohusiana na  vipigo kwa wanawake au kutelekezewa watoto na wenzi wao, kutokana na uwepo wa ndoa hizo hususani unapoanza msimu wa mavuno wanaume wengi huawacha wake zao na kuoa mabinti wengine hali ambayo imekuwa ikisababisha migogoro ya kifamilia.

“Tumepanga mkakati wa kutenga siku mbili kila wiki kwaajili ya kusikiliza kesi hizo na tutatembelea vijiji vyote vinavyounda kata ya salawe ili kutoa elimu kwa wanaume kuhusiana na tatizo la utelekezaji wa familia ambao umekuwa ukisababisha watoto kushindwa kupata haki zao za msingi kama vile chakula, malazi, afya na elimu,” alisema Michael.

Mmoja wa wahanga wa tatizo la kutelekezewa familia, Bahati Bundala mkazi wa Kijiji cha Salawe alisema kuwa mume wake alimwachia watoto wanne na kwenda kuoa mwanamke mwingine baada ya msimu wa mavuno wa mwaka jana ambapo walipata gunia 50 za mpunga hali ambayo imesababisha kuishi maisha ya shida na kushindwa kuihudumia familia yake.

“Nililazimika kuhama katika nyumba yangu na kwenda kupanga sehemu nyingine kutokana na vurugugu nilizokuwa nafanyiwa na mume wangu ,ugomvi ulianza baada ya kuuza mapunga alichukua fedha zote na kwenda mjini na kisha kuoa mwanamke mwingine na kututelekeza huku kijijini,” alieleza.

Aliongeza kuwa endapo elimu juu ya athari za ukatili wa kijinsia ilitolewa kwenye jamii itasaidia kuondoa unyanyasaji kwa wanawake na watoto wanaofanyiwa na wanaume kutokana na kuendekeza mila na desturi potofu za ndoa za mitara ambazo kwa sasa zinaweza kuwa chanzo cha magonjwa ya ngono.

Naye Kaimu Mtendaji wa kata hiyo, Eward Nestory alisema kuwa kwa kushirikiana na ofisi ya dawati la jinsia la polisi katika kituo kidogo kilichopo katika eneo hilo kimesaidia kusikiliza kesi nyingi za ukatili wa kijinsia husuani vipigo,utelekezaji wa familia, mimba na ndoa za utotoni na hatua mbalimbali zimeanza kuchukuliwa kwa wahusika wanaotekeleza vitendo hivyo.

“Wakazi wengi wa kata hii wameanza kupata mwamko wa kuripoti matukio ya ukatili wa kijinsia kwa viongozi wa ngazi za chini kuanzi mabalozi wa nyumba 10,wenyeviti wa vitongoji, vijiji, maafisa maendeleo na watendaji wa kata na vijiji,hivyo kuturahisishia sisi kama serikali kuchukua hatua stahiki haraka kwa kushirikiana na jeshi la polisi," alisema.

Sambamba na hilo Nestory alisema kuwa mbali na kupokea kesi hizo pia bado kunatatizo la ndoa za utotoni ambazo wahanga wake wakubwa ni wanafunzi wa shule za msingi na sekondari hivyo kusababisha wengi wao kutoendelea na masomo baada ya kupata mimba.

“Huku vijijini wanafunzi wanakatiza masomo kwa kupata mimba weingine wanaozeshwa kinyemela kwa wanaume wenye umri mkubwa,tunaendelea kuwachukulia hatua kali za kisheria wanaobainika kuetekeza matukio haya,niiombe jamii ibadilike na iachana na vitendo hivi ambavyo vinaathari kubwa kwa watoto wetu wakike kwa kuwakatisha ndoto zao kielimu Nestory,” alisema.


Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464