Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akizungumza kwenye kikao cha bodi ya barabara mkoani Shinyanga na kulalamikia mashimo katikati ya barabara mjini Shinyanga.
Na Marco Maduhu, Shinyanga
WAKALA wa Barabara Tanzania (TANROADS) na Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) mkoani Shinyanga, wamelalamikiwa na viongozi wa Serikali mkoani humo kwa kukithiri ubovu wa miundombinu ya barabara, ambayo imejaa mashimo na kukwamisha ujenzi wa shule ya Sekondari Mwasubi na kupelekea wanafunzi kushindwa kwenda shule.
Malalamiko hayo yametolewa leo kwenye kikao cha bodi ya barabara mkoani Shinyanga, kuwa mkoa huo unakabiliwa na miundombinu mibovu ya barabara zilizopo mijini na vijijini, na barabara kuu na kusababisha adha kwa watumiaji wa miundombinu hiyo wakiwamo wanafunzi kushindwa kwenda shule hasa kipindi hiki cha mvua.
Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, akizungumza kwenye kikao hicho, amesema kuna ulazima wa haraka baadhi ya barabara za mjini Shinyanga na barabara kuu zifanyiwe matengenezo, ambapo zimejaa mashimo na ni hatari kusababisha ajali.
Amesema hata zile barabara ambazo zilizibwa kwa viraka, nazo zimeharibika, na hivyo kuwataka Tarura na Tanroads wanapokuwa wakitoa kazi hizo, wawape Wakandarasi ambao wanauwezo mzuri wa kutengeneza barabara ili ziwe za kiwango na kudumu kwa muda mrefu.
“Barabara za Shinyanga ni mbovu zimejaa mashimo na zile ambazo zilizibwa kwa viraka nazo zimeharibika, ikiwamo na barabara ya kutoka Tinde kwenda Nzega, zifanyieni matengenezo ya haraka ili zisisababishe ajali. Pia nawapongeza Tanroads kwa kujenga barabara vizuri ya Mwakitolyo na Salawe,” amesema Mboneko.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kishapu, Nyabaganga Talaba, amesema kutokana na ubovu wa miundombinu ya barabara wilayani humo, umesababisha hata wananchi kushindwa kujenga Shule ya Sekondari Mwasubi, sababu ya barabara kutopitika eneo hilo hasa katika kipindi hiki cha mvua.
Amesema pia wanafunzi katika Shule ya Sekondari Igaga wilayani humo, wamekuwa wakishindwa kwenda shule kwenye kipindi hiki cha mvua sababu ya ukosefu wa daraja, na kusababisha kukosa vipindi vya masomo.
Aidha Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela, akizungumza wakati wa kufungua kikao hicho akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack, amemtaka Meneja wa TANROADS na Mratibu TARURA, kuwa na mikakati endelevu ya ujenzi wa barabara mkoani humo, ili ihudumie wananchi kwa mwaka mzima na kutoharibu shughuli zao za kiuchumi, pamoja na wanafunzi kushindwa kwenda shule.
Pia amezitaka mamlaka hizo kuhakikisha zinazimamia vizuri sheria za barabarani kwa kuzuia wananchi kufanya shughuli za kibinadamu kandokando ya barabara, pamoja na kuwachukulia hatua wale ambao wanakaidi, ili kutoendelea kutumia fedha nyingi za matengenezo ya barabara kila mwaka, huku akiwataka TANROADS waweke pia alama za usalama barabarani kwenye barabara ambazo hazina alama hizo.
Aidha Meneja wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoani Shinyanga, Mhandisi Mibara Ndirimbi, amesema changamoto ya ubovu wa miundombinu ya barabara zote mkoani Shinyanga zinafanyiwa kazi, ambapo katika mwaka wa fedha (2020-2021) kimeshatengwa kiasi cha fedha Shilingi Bilioni 13.4 kwa ajili ya matengenezo ya barabara, madaraja na makalavati.
Kwa upande wake Mratibu wa Wakala wa Barabara Mijini na Vijijini (TARURA) Mkoani Shinyanga Mhandisi Dastani Kishaka, alisema katika bajeti yao ya matengezo ya barabara na makalati, katika mwaka wa fedha (2020-2021) wametenga kiasi cha Shilingi Bilioni 7.6 ili kumaliza changamoto hiyo.
TAZAMA PICHA HAPA CHINI
Muonekano wa mashimo katikati ya barabara mjini Shinyanga.
Hali inavyoonekana katika moja ya barabara za mitaa mjini Shinyanga, hali ambayo imewakera viongozi wa Serikali akiwemo Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga, Jasinta Mboneko ambaye amezitaka wakala wa barabara kumaliza changamoto hiyo
Katibu Tawala Mkoa wa Shinyanga, Albert Msovela, akizungumza kwenye kikao cha bodi ya barabara mkoani Shinyanga.
Mkuu wa wilaya ya Kishapu Nyabaganga Taraba, akizungumza kwenye kikao cha bodi ya barabara na kulalamikia ubovu wa barabara wilayani humo, ambao umesababisha kukwamisha ujenzi wa shule ya Sekondari Mwasubi.
Meneja wakala wa barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Shinyanga Mhandisi Mibara Ndirimbi, akiwasilisha taarifa ya (TANROADS) kwenye kikao hicho cha bodi ya barabara juu ya matengenezo ya barabara ambazo ni mbovu.
Mratibu wakala wa barabara mijini na vijijini (TARURA) Mkoani Shinyanga Mhandisi Dastan Kishaka, akiwasilisha taarifa ya TARURA kwenye kikao hicho cha bodi ya barabara, ikiwamo bajeti ya matengezo ya barabara ambazo ni mbovu.
Wajumbe wakiwa kwenye kikao cha bodi ya barabara mkoani Shinyanga.
Wajumbe wakiwa kwenye kikao cha bodi ya barabara mkoani Shinyanga.
Wajumbe wakiwa kwenye kikao cha bodi ya barabara mkoani Shinyanga.
Wajumbe wakiwa kwenye kikao cha bodi ya barabara mkoani Shinyanga.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Ngassa Mboje, akichangia mada kwenye kikao hicho cha bodi ya barabara na kulalamikia naye ubovu wa barabara.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Kishapu Emmanuel Johnson, akichangia mada kwenye kikao hicho cha bodi ya barabara mkoani Shinyanga, na kulalamikia ubovu wa barabara wilayani humo.
Muonekano wa mashimo katikati ya barabara mjini Shinyanga.
Picha zote na Marco Maduhu