WAZIRI BITEKO ATETA NA VIONGOZI BARRICK, AWATAKA KUTUMIA FURSA ZA UWEKEZAJI SEKTA YA MADINI NCHINI

Picha ya pamoja ya Waziri wa Madini, Doto Biteko na Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick, Dkt. Mark Bristow wakizungumza jambo baada ya kikao kifupi kilichofanyika Februari 25, Jijini Mwanza

Na Steven Nyamiti -Mwanza
WAZIRI wa Madini, Doto Biteko, amefungua fursa za uwekezaji zilizopo hapa nchini kwa kampuni ya Madini ya Barrick kuendelea kuwekeza nchini, huku akiwasisitiza umuhimu wa kuzingatia sheria zilizopo hasa Sheria ya Madini ya Mwaka 2010 na marekebisho yake ya Mwaka 2017 sambamba na sheria zingine za nchi.

Waziri Biteko amesema hayo leo Februari 25, Jijini Mwanza alipokaribishwa na Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick, Dr. Mark Bristow kushiriki kikao chao cha Mpango Kazi katika kipindi cha miaka 10 ijayo kwenye sekta ya madini kinachofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Malaika Jijini Mwanza.

“Ni nafasi muhimu mmenipa ya kuja kuzungumza kama wadau wetu wa Sekta ya Madini ambao ni walipa kodi wetu na wabia kwenye migodi yetu ya Buzwagi, Bulyanhulu na North Mara” amesema Biteko.

Biteko ameeleza kuwa Tanzania ni mahali sahihi na salama kuendelea kuwekeza kwenye Sekta hii ya Madini na kuwataka kuondoa hofu juu ya uwekezaji wanaopanga kuutekeleza,  huku akisisitiza kuwa hata Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. John Magufuli ametoa maelekezo kwa wawekezaji wasipate usumbufu wa aina yoyote ili kuwa huru zaidi.

“Pia, Nawakumbusha kuzingatia matakwa ya kanuni ya 'local content' kushirikisha jamii zaidi, kwamba bidhaa nyingi ambazo zitanunuliwa basi zinunuliwe kupitia kampuni za ndani ya nchi. Ninafurahi kwamba zaidi ya dola za kimarekeni Milioni 290 ni manunuzi ambayo yamefaywa na kampuni za hapa ndani” ameeleza Biteko.

Kwa upande wake, Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick, Dkt. Mark Bristow ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa juhudi zinazofanyika kuendeleza Sekta ya Madini. 

Dkt. Bristow amesema kuwa katika kipindi cha miaka 10 ijayo kampuni ya Barrick itazingatia Sheria zilizopo kwenye Sekta ya Madini, kusimamia “Local content” kuleta teknolojia mpya zaidi ili kurahisisha uchimbaji na kuwa mabalozi wazuri ulimwenguni kutangaza fursa zaidi zilizopo hapa nchini.

Amesisitiza kuwa, wataboresha mahusiano yao na Serikali ya Tanzania na jamii kwa ujumla. Pia amemueleza Waziri Biteko Mipango waliyonayo sasa katika kipindi cha miaka 10 ijayo kwenye Sekta ya Madini kwa kuifanya kampuni ya Barrick kuwa bora kwenye Sekta ya Madini huku wakiendelea kufanya shughuli zao kwa uwazi zaidi, kulipa kodi kwa wakati, kuzingatia usalama wa wafanyakazi wao, kutunza mazingira kwa kuweka mipango ya muda mrefu zaidi.

Mazungumzo hayo mafupi na Kampuni ya Barrick na Waziri Biteko yamehudhuriwa na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, John Mongella, Mwenyekiti wa Tume ya Madini, Prof. Idris Kikula, Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimali watu kutoka Wizara ya Madini, Issa Nchasi, Mkaguzi wa Migodi, Dk. Abdulrahman Mwanga na watendaji wengine kutoka wizara ya madini. 

Hadi sasa Kampuni ya Barick inafanya shughuli zake zaidi ya nchi 13 duniani huku ikiwa imeajili wafanyakazi zaidi ya Elfu 42 na kuwa miongoni mwa kampuni kubwa za uchimbaji madini duniani.
Waziri wa Madini, Doto Biteko akizungumzana Watendaji wa Kampuni ya Madini ya Barrick kwenye kikao kifupi na Kampuni hiyo kilichofanyika Februari 25, Jijini Mwanza
Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Madini ya Barrick, Dkt. Mark Bristow (wa kwanza kushoto) akizungumza jambo mbele ya Waziri wa Madini, Doto Biteko Februari 25, Jijini Mwanza.
Picha ya pamoja ya Waziri wa Madini, Doto Biteko na Rais na Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya Barrick, Dkt. Mark Bristow wakizungumza jambo baada ya kikao kifupi kilichofanyika Februari 25, Jijini Mwanza
Picha ya pamoja ikiwaonyesha watendaji mbalimbali walioshiriki kikao kifupi cha Waziri wa Madini, Doto Biteko na Kampuni ya Barrick kilichofanyika Februari 25, Jijini Mwanza
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464