Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan, akifungua Kongamano la kimataifa la Uwekezaji katika Sekta ya Madini lenye lengo la kutangaza fursa za Uwekezaji katika Sekta za Madini ziliopo Nchini na kuwaunganisha pamoja Wachimbaji na watoa huduma kwenye Shughuli mbalimbali zinazofanyika Migodini. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini -Wizara ya Madini)
IMEELEZWA kuwa Wizara ya Madini katika mwaka huu wa fedha (2020/2021) imepangiwa kukusanya jumla ya Sh Bilioni 526.72, ambapo katika kipindi cha kuanzia Julai mwaka jana hadi Januari mwaka huu, tayari wizara hiyo imekusanya Sh Bilioni 360.7 sawa na asilimia 117.4.
Hayo yameelezwa leo Februari 22, 2021 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan wakati akifungua rasmi Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini kwenye ukumbi wa kituo cha kimataifa cha mikutano Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.
Makamu wa Rais amesisitiza kuwa makusanyo hayo ni ishara kwamba lengo la makusanyo yaliyopangwa kukusanywa kupitia sekta ya madini kwa mwaka huo wa fedha litafikiwa, huku akibainisha kuwa ifikapo mwaka 2025, mchango wa Sekta ya madini kwenye pato la taifa utapaa na kuchangia asilimia 10 tofauti na sasa ambapo inachangia asilimia 5.2.
"Tumeshuhudia ukuaji wa sekta ya madini ukiongezeka mwaka hadi mwaka na mchango wa sekta katika pato la taifa umeongezeka kutoka asilimia 3.4 mwaka 2015 hadi 5.2 kwa mwaka 2019.
"Sekta ya madini imeongoza kwa ukuaji kwa asilimia 17.7 ikilimganishwa na sekta nyingine za kiuchumi nchini," amesema
Ameeleza kuwa mabadiliko ya sheria ya madini ya mwaka 2017 yalilenga katika kuhakikisha wazawa wananufaika na rasilimali madini zilizopo nchini tofauti na ilivyokuwa awali ambapo sekta ya madini haikuonesha kuwa na manufaa yeyote kwa taifa na wananchi kwa ujumla.
Ambapo, moja kati ya hatua zilizochukuliwa ni pamoja na kuimarisha ushiriki wa nchi na wananchi katika mnyororo wa madini, kuzuia usafirishaji wa madini ghafi nje ya nchi na badala yake kuhamasisha uongezaji thamani wa madini kufanyika nchini.
"Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Joseph Pombe anaendelea kusisitiza kuwa, tumechelewa sana kunufaika na rasilimali madini ambazo tumejaaliwa na mwenyezi Mungu. Tunapaswa kushirikiana na wadau wengine, tuendelee kuchukua hatua madhubuti kuhakikisha kuwa sekta ya madini inaendelea kuwa na mchango mkubwa katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii," ameeleza.
Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Doto Biteko kuwa uwepo wa mkutano huo ni matokeo ya mkutano mkubwa uliowakutanisha wadau wa madini nchini na Rais Magufuli mwaka 2019 uliopelekea kutambua mchango mkubwa wa mikutano kama hii katika kutatua changamoto mbalimbali za kisekta.
"Kongamano hili litaweka jukwaa la kujadili mafanikio ya Sekta ya Madini, fursa zilizopo, changamoto na kutafuta masuluhisho chanya ya mikwamo katika uendelezaji wa sekta. Mikutano hii inalenga katika kuifanya sekta hii kuwa na mchango mkubwa katika taifa na kujenga mahusiano thabiti kati ya wadau wa shughuli za madini na jamii," amesema.
Mkutano huo wa siku tatu wa kimataifa wa uwekezaji katika Sekta ya Madini unalenga kutangaza fursa za uwekezaji katika Sekta za Madini ziliopo nchini na kuwaunganisha pamoja Wachimbaji na watoa huduma kwenye shughuli mbalimbali zinazofanyika migodini.
Mkutano huo umebeba kauli mbiu ya "Sekta ya Madini kwa Uchumi Imara na Maendeleo Endelevu" unafanyika katika Kituo cha mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Nyerere JNICC Jijini Dar es salaam.