Mhe. Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Dkt Eliezer
Mbuki Feleshi amewataka mahakamu wapya 70 kuhakikisha wanatoa haki kwa wote na
kwa wakati. Pia amewataka mahakimu hao kwenda kuwa mwarobaini wa kutoa
suluhisho kwenye maeneo ambayo yamekuwa yakilalamikiwa na wananchi katika
mahakama za mwanzo, hasa mashauri ya mirathi.
Mhe. Jaji Dkt Feleshi aliyasema hayo kwenye hotuba yake
iliyosomwa na Mhe. Dkt. Paul Faustin Kihwelo, Jaji wa Mahakama Kuu na Mkuu wa
Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) wakati wa kufungua semina hii
elekezi kwa Mahakimu Wakazi wapya 70.
Mhe.
Jaji Kiongozi aliongeza kuwa, mafunzo watakayopewa ni muhimu na yamelenga
kuwapa mbinu na nyenzo sahihi za kuweza kukabiliana na changamoto mbalimbali
wakati wa kuamua mashauri yatakayoletwa mbele yao ili waweze kuyashughulikia
kwa mujibu wa mipaka ya kisheria.
Aidha
Mhe. Dkt. Feleshi aliwasisitizia juu ya umuhimu wa kujinoa katika matumizi ya
TEHAMA ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya kiteknolojia katika utoaji wa haki
kwa wakati.
“kwa kuwa tunaishi katika mapinduzi ya nne ya
viwanda mnasisitizwa kujinoa zaidi kwenye matumizi ya TEHAMA na mifumo ya
kielektroniki tuliyonayo mahakamani ili tuweze kuendana na kasi ya mabadiliko
ya kidunia hivi sasa “
Hata hivyo hakusita kuwakumbusha juu ya kuzingatia
matumizi sahihi ya lugha katika utendaji wao wa kazi ikiwa ni sanjari na uwepo
wa uhitaji wa matumizi ya lugha ya Kiswahili ambayo itatumiwa Mahakamani na
kuwahimiza kujisomea stadi za lugha ili kuongeza misamiati ya kisheria kwani
itatoa wigo mpana katika kukuza lugha ya Kiswahili cha kisheria.
Kwa upande wake, Mhe. Wilbert Chuma, Msajli Mkuu wa Mahakama ya Tanzania
aliwakumbusha mahakimu hao wapya kufanya kazi kwa uadilifu na weledi ili
kujiepusha na mazingira ya rushwa ili kulinda heshima ya Mahakama.
Mahakimu
hao waliaapishwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma Februari
26, 2021 katika Viwanja vya Karimjee Jijini Dar es salaam.