AFUKUZWA NA MUMEWE KWA KUCHELEWA KUPATA MTOTO NDANI YA MWAKA MMOJA


       Mage Masanja mkazi wa Kijiji cha Ishinabulandi halmashauri ya Wilaya ya Shinyanga ambaye alifanyiwa ukatili na mume wake kwa kufukuzwa kutokana na kutozaa.

    Theleza Thomas mkazi wa Kijiji cha Ishinabulandi mamalishe ambaye anafanya kazi na Mage Masanja.

Suzy Luhende,Shinyanga Press Club Blog. 

Mage Masanja (24) mkazi wa kijiji cha Ishinabulandi kata ya Samuye halmashauri ya wilaya ya Shinyanga amefanyiwa  ukatili na mume wake baada ya  kufukuzwa kutokana na  kukaa kwa muda wa mwaka mmoja bila kupata ujauzito . 

Mage amesema aliishi na mme wake kwa mwaka mmoja, lakini hakufanikiwa kupata ujauzito ndipo mwanaume huyo alianza kubadilika na kuanza kumtolea lugha za udharirishaji pamoja na kipigo hali kisha kuwasiliana na wanawake wengine mbele ya mke wake. 

"Kwa kweli nilivumilia sana ndani ya miezi sita nilikuwa nafanyiwa mambo mengi ya ukatili, wakati mwingine mme wangu alikuwa anakuja na wanawake nyumbani na mimi nafukuzwa chumbani na kwenda kulala sebuleni lakini alipoona kwamba siteteleki ndipo aliamua kunipiga na kunifukuza kabisa niliondoka na kurudi nyumbani kwetu "amesema Mage.

Amesema alivyokuwa akiona wanawake wengine wanaletwa nyumbani kwake aliumia na kuamini kuwa  ipo siku Mungu atampa mtoto na kuondokana na mateso anayopitia na kupelekea afya yake kudhoofika.

Theleza Thomas ambaye ni mmiliki wa mgahawa alisema katika mgahawa wake wengi wanaokuja ni wale ambao wamefanyiwa ukatili na waume zao na wameachika na kubainisha kuwa vitendo hivyo  kwa sasa wanawake wengi wanafanyiwa hasa ukatili wa kimapenzi wanaume kuwaacha wake zao wakati wa mavuno na kwenda kuowa wageni wanaokuja senta.

"Mwanaume akishamuona mwanamke mpya tu kaonekana senta anamuacha hata wiki mke wake anahamia kwa mpya aliyeonekana, anauza hata baiskeli yake lakini akiishiwa anarudi kwamke kwa mke wa ndoa kumbembeleza tena huwezi jua alikokuwa anaweza akawa hata na magonjwa,"amesema Thereza.

Kwa upande wake Aisha Omary ambaye ni ofisa maendeleo ya jamii halmashauri ya wilaya ya Shinyanga amesema

wanaendelea kuelimisha jamii ili iweze kuelewa na kuachana na ukatili wa kijinsia ikiwa ni pamoja na mila potofu zilizopo katika jamii. 

Kamanda wa jeshi la polisi mkoa wa Shinyanga Debora Magiligimba aliwataka wanawake wote ambao wamekuwa wakifanyiwa ukatili kufika kufika kwenye madawati ya jinsia ambayo yapo katika vituo vya polisi kwa ajili ya kutoa malalamiko yao na kuweza kupata haki yao.

Naye ofisa ustawi wajamii mkoa wa Shinyanga Lyidia Kwesigabo amesema kwa ujumla mkoa wa Shinyanga bado tatizo la ukatili wa kijinsia lipo na kuitaka jamii kutoa ushirikiano ili kuondokana na ukatili kwa kina mama na watoto kunyanyaswa na kupigwa.

Mwisho.

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464