Mkuu wa Majeshi nchini Tanzania (CDF) Venance Mabeyo
Mkuu wa Majeshi nchini Tanzania (CDF) Venance Mabeyo amemhakikishia Rais Samia Suluhu Hassan kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vitamtii na kutekeleza majukumu yake kama ilivyoainishwa kwenye Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Amesema vyombo hivyo vitaendelea kuonyesha uadilifu, utiifu na uaminifu kwake kama ilivyokuwa kwa awamu za uongozi zilizopita.
Akizungumza katika ibada ya mazishi ya Rais wa Awamu ya Tano Hayati John Magufuli leo Ijumaa Machi 26, 2021 wilayani Chato Mkoa wa Geita kwa niaba ya wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, Mabeyo ameeleza kuwa hali ya nchi ni shwari na wataendelea kuimarisha ulinzi.
“Ulinzi wa nchi na mipaka yake ni salama na vyombo vitaendelea kukulinda kama rais, kukutii kama amiri jeshi mkuu na kutekeleza majukumu yetu kama ilivyoainishwa kwenye katiba.”
“Vyombo vya ulinzi na usalama vinakuhakikishia utiifu, uadilifu na uaminifu mkubwa kama ilivyo mila na desturi kwa majeshi yetu katika awamu zote zilizopita,” amesema.
Mabeyo ametumia fursa hiyo kumualika Rais Samia kuwatunuku nishani askari wanafunzi waliotakiwa kutunikiwa nishani hizo Machi 10, 2021.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464