Mtuhumiwa akionyesha namna alivyokuwa amewahifadhi kwenye mabegi kobe hao kwa ajili ya kuwasafirisha
JESHI la Polisi mkoani Simiyu limemkamata mtu mmoja (jina lake limehifadhiwa) mwenye umri wa miaka 35, mkazi wa Wilaya ya Bunda mkoani Mara akiwa na mabegi matatu yaliyokuwa yamebeba kobe hai wapatao 438 wenye thamani ya shilingi milioni 71.1.
Mtuhumiwa amekamatwa na kobe hao akiwa amewahifadhi ndani ya mabegi matatu katika standi ya mabasi ya Dutwa wilayani Bariadi.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Simiyu, Richard Abwao, amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa mwishoni mwa wiki iliyopita majira ya saa mbili usiku akiwa katika standi hiyo akisubiri usafiri ili kuendelea na safari yake ambapo hakutaka kueleza wapi alikuwa anawapeleka .
Kamanda Abwao amesema kobe hao wote wamewakabidhi kwa Maafisa Maliasili kwa ajili ya hifadhi na kwamba mtuhumiwa yuko mahabusu na atafikishwa Mahakamani mara upelelezi utakapokamilika.
Aidha, kamanda Abwao ametoa wito kwa wananchi kujiepusha na umiliki wa nyara za serikali kinyume na sheria kwani kufanya hivyo ni kosa la jinai, na pia amewaomba Wananchi kuendelea kutoa taarifa za wahalifu katika maeneo ya makazi yao ili kuendelea kuufanya Mkoa kuwa mahali salama.
Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464