MBUNGE LUHAGA MPINA AMKUMBUKA JPM, AMPA NENO RAIS SAMIA


Mbunge wa Jimbo la Kisesa, wilayani Meatu mkoa wa Simiyu, Luhaga Mpina akizungumza na waandishi wa habari muda mfupi baada ya mazishi ya Hayati Dkt. John Magufuli.

Na Mwandishi wetu
MBUNGE wa Jimbo la Kisesa, Luhaga Mpina amemlilia aliyekuwa Rais wa Tanzania, Dk. John Pombe Magufuli akimtaja kama kiongozi wa mfano na kielelezo barani Afrika katika kuleta maendeleo na kushughulikia kero na matatizo ya wananchi yaliyoshindikana kwa miaka mingi.

Mpina ambaye katika kipindi cha miaka mitano ya Rais Magufuli aliwahi kuwa Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira na baadae kuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi.

Akizungumza mara baada ya kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa Marehemu, Dk. Magufuli kwenye uwanja wa Magufuli mjini Chato, Mpina alisema taifa limepata pigo kubwa kwa kuondokewa na kiongozi makini na shujaa ambaye alitumia muda wake wote wa uongozi kusaka maendeleo ya nchi huku akikomesha na kumaliza dhuluma na vikwazo vilivyokuwepo dhidi ya ustawi wa jamii, uchumi na maendeleo ya nchi yetu.

“Nilizipokea taarifa za kifo cha Mhe. Rais Dk. Magufuli kwa huzuni na majonzi makubwa nililia kwa kupaza sauti zaidi ya saa moja na baadae machozi yaliendelea kutiririka kama maji nikiwa sijui hata la kufanya jitihada za kuninyamazisha na kufuta machozi hazikuwezekana,"

"Tangazo la kifo cha kiongozi huyu ilikuwa ni mkuki uliochoma moyo wangu na kuujeruhi sana, Kiongozi nimpendaye mchakapazi na hodari asiyeyumba wala kuyumbishwa katika maamuzi asiyechoka kupambania taifa lake na asiye na rekodi ya kushindwa jambo lolote kweli ndio hatunaye tena” alisema Mpina.

Mpina alibanisha kuwa kabla ya Rais Magufuli mauaji ya vikongwe na albino yalikithiri kila kona ya nchi na kufanya kundi la wananchi hao kuishi kwa hofu na fedheha kubwa ndani ya nchi yao ambapo kwa muda mfupi wa uongozi wake vitendo hivyo vimekomeshwa na sasa makundi haya yanaishi kwa amani na kushiriki shughuli za kiuchumi bila wasiwasi wowote .

Kutokana na jitihada hizo Mpina alisema ukusanyaji wa mapato ya kodi kwa mwezi umeongezeka kutoka wastani wa shilingi bilioni 850 mwaka 2015 hadi wastani wa shilingi trilioni 2 kwa mwezi mwaka 2020. Kwa ujumla mapato ya ndani yameongezeka kutoka trilioni 11 mwaka 2015 hadi kufikia trilioni 18.5 mwaka 2019.

Mpina alibainisha kuwa katika kipindi cha Magufuli alifanikiwa kumaliza tatizo la uvuvi haramu ambapo tulishuhudia wingi wa samaki pamoja na Samaki wakubwa kupatikana mfano sangara kwenye Ziwa Victoria waliongezeka kutoka tani 417,936 mwaka 2016 hadi tani 816,964 mwaka 2020, na urefu wa sangara umeongezeka kutoka wastani wa sentimeta 16 hadi sentimeta 25.2.

Mpina alisema pia Rais Magufuli alikuwa mtetezi wa wanyonge ambapo katika kipindi cha miaka mitano iliyopita aliyakumbuka makundi ambayo yalikuwa hayathaminiwi na kufanyiwa kila aina ya dhuluma na baadhi ya watendaji wa Serikali kama Mama ntilie, Bodaboda na Machinga ambapo dhuluma zilikomeshwa kwa kutengewa maeneo biashara na kuondolewa mzigo mkubwa wa ushuru uliokuwa unawaelemea kila uchao kwa kutengenezewa vitambulisho vya wajasiriamali.
Mbunge wa Jimbo la Kisesa, wilayani Meatu mkoa wa Simiyu, Luhaga Mpina akifuatilia kwa makini ibada ya mazishi ya aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli nyumbani kwake Chato mkoani Geita. (Picha zote kutoka Ofisi ya Mbunge Mpina)

Kama una Taarifa, Habari, Tangazo n.k Wasiliana nasi kupitia shinyapress@gmail.com au +255 788 469 464